Wednesday, September 3, 2014
HIFADHI YA TAIFA YA KITULO ILIYOPO WILAYANI MAKETE YAZIDI KUONGEZA VIVUTIO VYA KITALII.
Do you like this story?
Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akiangalia maporomoko ya maji yaliyopo kwenye hifadhi ya taifa ya Kitulo. |
Akizungumza mbele ya kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Makete
iliyofanya ziara hifadhini humo, Kaimu mkuu wa hifadhi ya Kitulo Bw.Pius Mzimbe
amesema kwa hivi sasa wanazidi kuboresha zaidi hifadhi hiyo ambapo kwa mwaka
huu wa fedha 2014/2015 wataboresha barabara zilizopo kwenye hifadhi hiyo ili
kusaidia kufikika kirahisi kwa vivutio lukuki vinavyopatikana kwenye hifadhi
hiyo hasa kwenye maporomoko ya maji pamoja na kujionea mimea ya aina mbalimbali
iliyoota kwenye hifadhi hiyo.
"Kwa mfano kwa sasa tunajenga camp site (vituo vya kupumzikia
watalii) ambapo watalii wakiwa hapa watajionea mandhari mabalimbali ikiwemo
milima, mimea na vingine, watapanda kwenye milima na kuona maeneo ya mbali na
wakichoka watarudi hapa kupumzika na tutawawekea bafu na maliwato kwa ajili yao
pamoja na jiko kwa ajili ya kuwapikia vyakula wanavyovipenda hasa vya
asili" alisema Mzimbe.
Amesema kumekuwa na changamoto ya kutofikia baadhi ya vivutio hasa
maporomoko ya maji kutokana na ubovu wa barabara wakati wa masika hivyo kwa
kuziboresha kutasaidia barabara hizo kupitika muda wote hivyo kuongeza mapato
yatokanayo na hifadhi hiyo ya Kitulo.
Bw. Mzimbe ametoa wito kwa wananchi wa ndani na nje ya Makete kujijengea
utaratibu wa kutembelea hifadhi hiyo ili wajionee vivutio mbalimbali ikiwemo
maua, ndege, maporomoko ya maji na mimea mbalimbali ambayo ipo hifadhini humo
tu na vivutio vingine ambavyo wanavigundua siku hadi siku.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Makete ambaye pia ni mwenyekiti wa
kamati ya ulinzi na usalama wilaya Mh. Josephine Matiro amesema wilaya yake
imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya kitalii ambavyo vipo ndani ya
hifadhi ya Kitulo na vingine vipo nje hivyo wao kama serikali watahakikisha
vivutio hivyo vinaendelea kuwepo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Mh. Matiro amesema ni vyema wanamakete wakajitokeza kwa wingi kufanya
utalii wa ndani na kujionea jinsi wilaya yao ilivyobarikiwa na ni jambo la aibu
kwa watalii wa nje ya nchi kuja kutembelea hifadhi ya Kitulo ilihali wakazi wa
makete hawajawahi kuitembelea.
"Kwa mfano leo tumejionea vivutio vingi humu hifadhini, lakini
ukipita kwa gari unaishia kuona maua ama ndege lakini ukiingia humu ndani vipo
vivutio vingi vya ajabu na vya kuvutia, mimi na kamati ya ulinzi na usalama
tumeamua kuonesha mfano, tunaomba wananchi mtuunge mkono kwa kuja kuitembelea
hifadhi yetu ya kitulo" amesema Matiro.
Wakiwa hifadhini humo wajumbe wametembelea maporomoko ya maji ya
Mwakipembo na Numbwe ambayo ni marefu zaidi, pamoja na eneo ambalo linajengwa
vituo vya kupumzikia watalii na pia kujione mandhari tulivu ya hifadhi hiyo ya
Kitulo.
Hifadhi ya Kitulo ipo katika tarafa ya matamba wilayani Makete na
inasifika duniani kwa kuwa na maua na ndege na kwa hivi sasa vivutio vingine
vya utalii vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku.
Na
Edwin Moshi, Makete.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “HIFADHI YA TAIFA YA KITULO ILIYOPO WILAYANI MAKETE YAZIDI KUONGEZA VIVUTIO VYA KITALII.”
Post a Comment