Tuesday, September 2, 2014
IKULU; RAIS HAKUWAOMBA UKAWA WAREJEE BUNGENI
Do you like this story?
Dodoma. Ikulu
imesema Rais Jakaya Kikwete hakuwaomba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambao
ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), warejee kuendelea na vikao
vya Bunge hilo.
Ukawa ni umoja
unaoundwa na wajumbe ambao ni wanachama wa vyama vya siasa vya Chadema, NCCR
Mageuzi na CUF waliosusia Bunge la Katiba tangu Aprili 16, mwaka huu kwa madai
ya kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo.
Mkurugenzi wa
Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu alisema suala la Ukawa kurejea bungeni
haikuwa ajenda kuu ya mkutano huo uliofanyika Ikulu ya Kilimani, mjini Dodoma
juzi na badala yake kulikuwa na majadiliano ya jumla mchakato wa Katiba.
Katika mkutano
huo ulioratibiwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), viongozi wa Ukawa
walikuwa sehemu ya ujumbe uliokutana na Rais Kikwete kwa ajili ya kuzungumzia
mambo mawili; mchakato wa Katiba na jinsi ya kuwa na uchaguzi bora wa 2015.
“Hilo suala
halikuwa ajenda ya mkutano, hivyo kusema Ukawa wamemgomea Rais siyo kweli,”
alisema Rweyemamu ambaye alikuwa akirejea habari iliyoandikwa na gazeti hili
jana kuhusu yaliyojiri katika mkutano wa Rais Kikwete na viongozi hao.
Mwenyekiti wa
TCD, John Cheyo alisema mkutano huo ulikuwa wa mafanikio makubwa na kwamba
watakutana tena na Rais Kikwete Septemba 8, 2014 baada ya kamati ndogo
iliyoundwa kukamilisha kazi yake. Kamati hiyo inawajumuisha viongozi wa vyama vya
siasa ambavyo mbali na kwamba ni wanachama wa TCD, ndivyo vimekuwa vikivutana
kuhusu mchakato wa Katiba.
Viongozi hao
ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia ambaye ataongoza kamati hiyo na
wajumbe wake ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.
Ukawa wamekuwa
katika mvutano na CCM, ambayo katika kikao cha Kamati Kuu yake wiki mbili
zilizopita, ilitoa taarifa kwamba inaridhika jinsi mchakato unavyokwenda ndani
ya Bunge Maalumu na kuwataka wajumbe walitoka nje warejee bungeni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “IKULU; RAIS HAKUWAOMBA UKAWA WAREJEE BUNGENI”
Post a Comment