Monday, September 22, 2014
RASIMU YA KATIBA MPYA ILIYOPENDEKEZWA KUWASILISHWA BUNGENI SEPTEMBA 24 MWAKA HUU.
Do you like this story?
![]() |
Katibu wa Bunge Maalum la Katiba Ndg. Yahya Khamis Hamad akielezea kuhusu mabadiliko ya ratiba ya bunge hilo. |
Na Benedict Liwenga
na Magreth Kinabo.
RASIMU ya
Katiba Mpya iliyopendekezwa inatarajiwa kuwasilishwa
katika Bunge Maalum la Katiba Septemba 24, mwaka huu.
Mabadiliko hayo
yametangazwa jana jioni na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahya Khamis Hamad
wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Aidha Katibu huyo
amesema uamuzi wa mabadiliko hayo, umetokana na kufanyika kikao baina ya Kamati
ya Uongozi wa Bunge hilo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi.
Hata hivyo Katibu
huyo amesema kuwa kazi ya uandishi wa Rasimu hiyo imeshakamilika na kazi
iliyobakia ni kuipitia kwa makini, hali iliyosababisha mabadiliko ya
uwasilishaji wa Rasimu hiyo katika Bunge hilo, uliopangwa kufanyika hapo kesho
Septemba 22, mwaka huu.
“Uwasilishwaji wa
Rasimu ya Katiba inayopendekezwa sasa utafanywa siku ya Septemba 24, mwaka huu,
” alisema Katibu wa Bunge hilo.
“Kamati ya uongozi
imeona kuwa ni busara na kupewa siku mbili kwa ajili ya kuipitia upya ile kazi
ambayo wameifanya ili kufikia tarehe 24 kutoa kitu makini, napenda
niwahakikishie wananchi kuwa kitu kizuri kinakuja.
Aliongeza kuwa Kamati
ya Uongozi ya Bunge hilo, inatarajia kukabidhiwa Rasimu ya Katiba Mpya
iliyopendekezwa tarehe 23 Septemba, mwaka huu kutoka kwa Kamati ya Uandishi wa
Bunge hilo.
Aidha, Katibu huyo
ameeleza sababu ya uairishwaji wa uwasilishwaji wa Rasimu hiyo Bungeni hapo
kutokana na ugumu, umakini na uzito wa kazi yenyewe.
“Tulikuwa tumepanga
hapo tokea awali kufanya kikao na Kamati ya Uongozi asubuhi tukafanya mchana na
hata jioni kila wakati Kamati ya Uandishi ikawa bado haijamaliza hiyo kazi na
tulivyofanya kikao cha Kamati ya Uongozi hii jioni tukamuita Mwenyekiti wa
Kamati ya uandishi akaonyesha kwamba hiyo kazi walikuwa wakiifanya usiku na
mchana na hadi sasa wamesema wamemaliza kuandika.
“Lakini kutokana na
namna walivyokuwa wakiifanya hiyo kazi kwa uharaka na ingawa walikuwa
wakiifanya kwa umakini lakini wanahitaji muda wa kuanza kuipitia kwa makini
zaidi kuanzia mwanzo mpaka mwisho hivyo wakaomba wapewe muda wa siku mbili ya
kesho na keshokutwa ili kuweza kuipitia kazi hiyo kwa umakini,”alisema.
Katibu wa Bunge hilo,
aliongeza kwamba mabadiliko hayo hayataweza kuathiri upigaji kura uliopangwa
kufanyika Septemba 29 hadi 2 Oktoba mwaka huu.
“Tumeacha siku
ya Septemba 29, mwaka huu ili iwe siku ya kuanza kupiga kura na
tumalize 2 Oktoba, mwaka huu ili tuhakikishe kwamba Oktoba 4 , mwaka
tumemaliza hili zoezi,” alisisitiza.
Aidha Katibu huyo
alifafanua kuwa ratiba kuhusiana na masuala hayo ataitoa leo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RASIMU YA KATIBA MPYA ILIYOPENDEKEZWA KUWASILISHWA BUNGENI SEPTEMBA 24 MWAKA HUU.”
Post a Comment