Monday, September 15, 2014
SERIKALI YAWEKA MAMBO WAZI, SASA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA KUFANYIKA DESEMBA 14.
Do you like this story?
KIPENGA cha kampeni za uchaguzi wa
serikali za mitaa, kinatarajiwa kupulizwa Novemba 30 mwaka huu na uchaguzi
kufanyika Desemba 14 chini ya sheria zilizopo.
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iliyotumwa katika vyombo vya habari
jana, ilifafanua kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa kuzingatia masharti ya sheria
za serikali za mitaa na kanuni za uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, sheria hizo zimetungwa na ofisi yake, baada ya
kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa vyenye
usajili wa kudumu, asasi za kiraia na wadau mbalimbali.
Kwa uamuzi huo, wagombea wa nafasi
zinazowaniwa za mwenyekiti wa mtaa, kijiji na kitongoji na nafasi za ujumbe wa
serikali za vijiji na kamati za mitaa, wametakiwa wawe wanachama na wadhaminiwe
na chama cha siasa chenye usajili wa kudumu.
Ratiba
Katika ratiba iliyotolewa sambamba na
taarifa hiyo, wasimamizi wa uchaguzi wameelekezwa kutoa tangazo la majina na
mipaka ya mitaa, vijiji na vitongoji, siku 50 kabla ya siku ya uchaguzi kwa
kuzingatia Kanuni ya 6 ya Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali
za Mitaa, ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa ya mwaka 2014.
Baada ya hatua hiyo, wasimamizi hao wa
uchaguzi watateua majina ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi mara baada ya
kusambazwa kwa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa.
Katika eneo lake, msimamizi wa uchaguzi
atatoa maelekezo ya uchaguzi siku zisizopungua 28 kabla ya siku ya uchaguzi kwa
mujibu wa Kanuni ya 7(1), 8(1) ya kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za
serikali za mitaa, ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa za mwaka 2014.
Aidha msimamizi wa uchaguzi atateua
ofisa wa umma mwenye sifa na uadilifu, atakayeandikisha na kuandaa orodha ya
wapiga kura siku 21 kabla ya siku ya uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni 8 na 9 ya
Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2014.
Uteuzi wagombea
Baada ya hatua zote hizo za awali kufanyika, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atabandika orodha ya wapiga kura mahali pa matangazo ya uchaguzi na kutunza kumbukumbu zake, baada ya kusambazwa kwa kanuni za uchaguzi na kufanya uteuzi wa wagombea siku zisizopungua 20 kabla ya siku ya uchaguzi.
Baada ya hatua zote hizo za awali kufanyika, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atabandika orodha ya wapiga kura mahali pa matangazo ya uchaguzi na kutunza kumbukumbu zake, baada ya kusambazwa kwa kanuni za uchaguzi na kufanya uteuzi wa wagombea siku zisizopungua 20 kabla ya siku ya uchaguzi.
Ratiba iliyotolewa pia inaonesha kwamba
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, katika muda wa siku mbili tangu siku ya uteuzi
kufanyika, atasikiliza na kutoa uamuzi katika muda usiozidi siku mbili kwa
mapingamizi mbalimbali, kuanzia siku ya kupokea pingamizi husika.
Aidha kutakuwepo na Kamati ya Rufaa,
ambayo wajumbe wake watateuliwa na Katibu Tawala wa Mkoa na katika uteuzi wake,
Katibu Tawala atazingatia hali halisi ya watumishi wa umma walioko katika
wilaya husika.
Kamati hiyo ya Rufaa, itateuliwa siku
saba kabla ya siku za uteuzi wa wagombea kwa mujibu wa Kanuni ya 16(4) ya
Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za mwaka 2014.
Kampeni
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kampeni za
uchaguzi zitafanyika wiki mbili za mwisho kabla ya siku ya uchaguzi na
zitafanyika kwa muda wa siku 14 na zitamalizika siku moja kabla ya siku ya
uchaguzi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2014.
Ili kufanikisha uchaguzi huo, wananchi
wametakiwa kujiandikisha katika Rejista ya Wapigakura, itakayoandaliwa siku
ishirini na moja kabla ya siku ya uchaguzi; na uchaguzi utafanywa kwa kutumia
karatasi maalumu za kupigia kura.
Aidha kura zitapigwa na kutumbukizwa
kwenye masanduku ya kupigia kura na kama kawaida, uchaguzi utafanyika katika
ngazi ya kitongoji na mitaa katika sehemu ya faragha na hakutakuwa na mikutano
ya uchaguzi katika ngazi za vijiji.
Uchaguzi uliopita
Katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa, CCM kilipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 90 ya kura zote zilizopigwa, hatua iliyochukuliwa na wachambuzi wengi kuwa ni dalili kuwa chama hicho kilikuwa kinakwenda kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa, CCM kilipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 90 ya kura zote zilizopigwa, hatua iliyochukuliwa na wachambuzi wengi kuwa ni dalili kuwa chama hicho kilikuwa kinakwenda kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Uchaguzi wa mwaka huu, mbali na
kuendelea kutumika kutoa ishara za uchaguzi mkuu ujao, pia utakuwa na umuhimu
wa ziada katika kupima uimara wa makubaliano ya vyama vikubwa vya siasa,
vilivyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakati wa mchakato wa
Katiba mpya na kukubalika kwao kwa wananchi.
Tayari viongozi wa vyama hivyo,
Chadema, CUF na NCCR Mageuzi, walishatoa kauli ya kuhoji kwa nini uchaguzi huo
unachelewa, wakihofia kuwepo wanachoita mchezo mchafu wa kuwashitukiza.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena
Nyambabe, alinukuliwa akidai Serikali imeshindwa kutangaza tarehe ya kufanyika
kwa uchaguzi huo, lakini pamoja na hitilafu hiyo, chama hicho kimeshatoa
taarifa kwa wanachama wake kujiandaa kugombea.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena
Sakaya, alinukuliwa akidai kwa kuwa uchaguzi huo hufanyika Septemba kila mara
na kwa kuwa mwaka huu kuna Bunge Maalumu la Katiba linalomalizika Oktoba,
Serikali ilitakiwa kulitambua hilo na kutoa ratiba mapema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa
Chadema, John Mnyika alisema kutokana na mchakato wa kupata Katiba mpya
kusuasua, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi vinatakiwa kushirikiana
ili kushinda viti vingi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SERIKALI YAWEKA MAMBO WAZI, SASA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA KUFANYIKA DESEMBA 14.”
Post a Comment