Tuesday, September 16, 2014
TUSHIRIKIANE KUONDOSHA MATUMIZI YA KEMIKALI ZINAZOHARIBU TABAKA LA OZONI.
Do you like this story?
Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dar
es Salaam.
Tarehe 16 Septemba, mwaka huu
Tanzania inaungana na Jumuiya ya Kimataifa katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa
ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kama ilivyoagizwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa
Mataifa katika azimio lake la 49/114 la tarehe 19 Desemba, 1994 huku kaulimbiu
yake ikiwa ni ‘Ulinzi wa Tabaka
la Ozoni; Jitihada zinazoendelea (Ozone Layer Protection; Mission Goes On)’.
Tarehe hiyo ni kumbukumbu ya
kutiwa saini Mkataba wa Montreal (Montreal
Protocol-1987) kuhusu kemikali zinazomonyoa Tabaka la Ozoni kwa
kudhibiti utengenezaji na matumizi ya kemikali zinazoharibu Tabaka hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa
na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) zinaeleza kuwa, Mkataba huo umepata
mafanikio makubwa ya kupunguza zaidi ya asilimia 98% ambapo ni takribani tani
milioni 1.8 ya uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa
ya Ozoni.
Aidha taarifa inesema kuwa,
punguzo hilo limechangia katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi kwasababu baadhi ya kemikali zinamong’onyoa tabaka la ozoni pia
husababisha kuongezeka kwa joto duniani, mfano kiasi cha kemikali kilichoondolewa
katika matumizi ni sawa na takriban tani bilioni 135 za hewa ukaa na hivyo
kuchangia kwa kasi kubwa katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani na
mabadiliko ya tabianchi.
Matokeo ya tafiti yanathibitisha kwamba
kiwango cha kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni angani kinaendelea kupungua
na inakadiriwa kuwa iwapo jitihada za utekelezaji wa Mkataba huo zitaendelea,
Tabaka la Ozoni litarudi katika hali ya kawaida ifikapo katikati ya karne hii.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya
kitaifa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa Mkataba huo, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mhe. Mhandisi Dkt. Mahenge alisema kuwa
1996 Serikali iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya
kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni, mikakati hiyo ni pamoja kujenga
uwezo wa Taasisi zinazosimamia utekelezaji wa Mkataba, kuweka takwimu za
kemikali hizo, kutoa elimu kwa wadau na kwa umma kuhusu umuhimu wa Tabaka la
Ozoni na hatari zinazolikabili, kusambaza habari kuhusu kemikali na teknolojia
mbadala, kubadilisha teknolojia katika viwanda vinavyotumia kemikali haribifu,
kutoa mafunzo yanayolenga kuimarisha ujuzi katika sekta ya kuhudumia viyoyozi
na majokofu.
Mikakati mingine ya kitaifa ni
kuimarisha mbinu za upunguzaji wa matumizi ya kemikali husika kwa kuanzisha
mtandao wa kunasa, kusafisha na kurejeleza vipoza joto, kuhamasisha na kuhimiza
matumizi ya kemikali na teknolojia mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni pamoja
na kuweka taratibu za kudhibiti uingizaji na matumizi ya kemikali
zinazodhibitiwa na Mkataba wa Montreal.
“Hatua hizi zimewezesha Tanzania
kuondosha kemikali hizi kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa na Mkataba”, alisema
Dkt. Mwandisi Mahenge.
Dkt. Mahenge alibainisha kuwa
Chini ya Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali haribifu, serikali
iliandaa Mpango wa Usimamizi wa Vipodozi yaani (Refrigerant Management Plan) na katika utekelezaji wake,
mambo kadhaa yamefanyika ikiwemo kuandaa Kanuni za Usimamizi wa kemikali
zinazomong’onyoa tabaka la hewa ya Ozoni ambazo zilianza kutumika tarehe 7
Desemba mwaka 2007.
Pia kusambaza kwa Vitambuzi vya
kemikali hizo vipatavyo 18 kwa ajili ya vituo vilivyo mipakani mwa Tanzania,
pia kusambaza mitambo na zana za kuhudumia majokofu na viyoyozi kama vile
mashine za kunasa na kurejeleza gesi chakavu kwa vyuo vyote vinavyotoa mafunzo
ya fani ya kuhudumia majokofu na viyoyozi hapa nchini.
Akivitaja vyuo hivyo vyenye kutoa
mafunzo ya fani hizo, Dkt. Mahenge alisema kuwa kuna Vyuo vya VETA vilivyopo
Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Kihonda Morogoro, Moshi na Kigoma, YMCA,
JKT-Mgulani, Vyuo vya uvuvi vya Mbegani-Bagamoyo na Nyegezi jijini Mwanza,
Taasisi ya Taifa ya Usafirishaji, Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam,
Taasisi ya Teknolojia ya Karume Zanzibar, Taasisi ya Sayansi na
Teknolojia-Mbeya pamoja na Chuo cha Mafunzo ya Ubaharia (DMI) kilichopo Dar es
Salaam.
“Vituo vitano vya Kikanda vya
kunasa na kusafisha gesi chakavu za Majokofu na Viyoyozi vimeanzishwa katika
vyuo vya VETA vya Mwanza, Chang’ombe-Dar es Salaam, Kigoma, Mbeya na
Mkokotoni-Zanzibar”, alitaja Dkt. Mahenge.
Dkt. Mahenge aliongeza kuwa Mtambo
wa kunasa na kurejeleza kemikali umewekwa katika Kituo cha Tanzania cha
Uzalishaji Bora na Teknolojia Endelevu (Cleaner Production Centre for Tanzania).
Katika utekelezaji huo uliofanywa
na serikali, jumla ya Maofisa Forodha na Wasimamizi wa Sheria wapatao 400
wamepatiwa mafunzo kuhusu namna ya udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka
la hewa ya Ozoni na hadi sasa Tanzania imeweza kupunguza zaidi ya tani 216 sawa
na asilimia 86% ya kiasi cha matumizi ya kemikali hizo, mwaka 1999.
Hapa nchini maadhimisho haya
yanafanyika kwa njia ya uelimishaji umma kuhusu Tabaka la Ozoni, faida zake,
madhara ya kuharibika kwa Tabaka hilo na matumizi salama ya bidhaa zenye
kemikali rafiki kwa tabaka la ozone, hivyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari
elimu hiyo itasambazwa kwa jamii ili kuongeza ushiriki katika kutekeleza jukumu
hilo muhimu la kuilinda sayari hii.
Bila shaka kila mmoja anatakiwa
kuonyesha juhudi katika kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni
yanayosababishwa na bidhaa mbalimbali tunazonunua na kutumia majumbani au
sehemu za biashara.
Katika kuhifadhi Tabaka la Ozoni
Mhandisi Dkt. Mahenge alisema kuwa kila mwananchi anatakiwa kushiriki kwa
kuzingatia mambo mbalimbali yakiwemo;-
Kuepuka kuingiza nchini gesi
zilizopigwa marufuku pamoja na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile
majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mitumba) na vipya vinavyotumia gesi
aina ya R11 na R12, kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa tabaka la
Ozoni kama vile gesi aina ya R134a, R407, R404, R600 na R717, kununua bidhaa
zilizowekwa nembo rasmi isemayo ‘Ozone
friendly’ ikiwa na maana kuwa ‘sahibu wa Ozoni’ au ‘CFC-free’
ikiashiria kuwa haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka
la Ozoni.
Tahadhari nyingine ni kuepuka
kutupa ovyo majokofu na viyoyozi chakavu ama vifaa vya kuzima moto vyenye
kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni aina ya ‘CFCs’na ‘halon’,
pia kuepuka matumizi ya kemikali aina ya ‘Methyl bromide’ kufukizia udongo na badala yake ni vema
kutumia mbinu mbadala na usalama pamoja na mbinu tungamanishi za udhibiti wa
wadudu waharibifu yaani ‘Intergrated
Pest Management’.
Mafundi wa majokofu na viyoyozi
hawanabudi kuhakikisha kuwa wananasa na kutumia tena vipoozi (refrigerants)
kutoka kwenye viyoyozi na majokofu badala ya kuviacha huru visambae anagani.
Aidha, watoe elimu ya kutosha kwa wateja wao juu ya njia rahisi za kutambua uvujaji
wa vipoozi kutoka katika majokofu na viyoyozi wanavyotumia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TUSHIRIKIANE KUONDOSHA MATUMIZI YA KEMIKALI ZINAZOHARIBU TABAKA LA OZONI.”
Post a Comment