Saturday, September 20, 2014
YANGA YA MAXIMO YACHARAZWA 2-0 NA MTIBWA SUGAR JAMHURI...JAJA AKOSA PENALTI..
Do you like this story?
MBRAZIL Marcio Maximo
amepoteza mechi yake ya kwanza akiiongoza Yanga baada ya kukubali kipigo
‘swaafi’ kabisa cha mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar, uwanja wa Jamhuri mkoani
Morogoro jioni hii.
Katika mechi hiyo ya
kukata na shoka, Mbrazil mwingine, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ naye ameweka
rekodi ya kukosa mkwaju wa kwanza wa penalti akiichezea Yanga katika mechi yake
ya kwanza ya ligi kuu.
Mabingwa hao wa 1999
na 2000 wakiongozwa na mwanafunzi wa zamani wa Maximo, Mecky Mexime, waliandika
bao la kuongoza katika dakika ya 15 kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji
wao hatari, Musa Hassan Mgossi.
Nahodha wa Yanga,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alifanya makosa ya kumsindikiza Mgosi katika eneo la
hatari akiamini kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ ataokoa, lakini hakufanikiwa na
kumpa nafasi nyota huyo wa zamani wa Simba kuandika bao kimiani .
Yondan alishindwa
kuosha mpira mrefu wa juu kwa kichwa na kuangukia eneo ambalo si mabeki wala
kipa ambaye angeweza kuokoa kiurahisi. Licha ya Oscar Joshua kuingia kusaidia
kuokoa, Mgosi alimchengua Dida aliyetoka langoni mwake na kufungwa goli hilo.
Wakati wachezaji wa
Mtibwa wakishangilia bao hilo, nyuki walipita uwanjani hapo na kusababisha
baadhi ya wachezaji wa timu zote kulala chini ili kukwepa madhara.
Dakika ya 32 Jaja
almanusura aandike bao safi kwa kichwa akiunganisha kona iliyopigwa na Haruna
Niyonzima, lakini mabeki wa Mtibwa waliondoa mpira katika mstari wa golini na
kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kwa ujumla dakika 45
za kipindi cha kwanza sola lilianza kwa presha kubwa, na kushuhudia timu zote
zikicheza mpira wa ‘butu-butu’.
Hata hivyo, Yanga
walionekana kufika mara nyingine golini na kupiga mashuti 5 yaliyolenga goli
wakati Mtibwa walipiga 2 tu.
Yanga walionekana
kutofanya vizuri sehemu ya kiungo mpaka pale kocha Marcio Maximo alipoamua
kumtoa Oscar Joshua na kumuingiza Omega Seme.
Mabadiliko hayo
yalimlazimisha Mbuyu Twite arudi sehemu ya ulinzi wa kushoto na kumpisha Seme
sehemu ya kiungo. Mabadiliko hayo yaliwapa nguvu Yanga na kutawala sehemu ya
kiungo.
Hata hivyo licha ya
kutawala sehemu ya kati na kumiliki mpira kwa asilimia 52 kwa 48 katika kipindi
hicho cha kwanza, Yanga walikosa mipango sehemu ya mwisho na kukosa
nafasi za kufunga.
Sehemu ya ulinzi ya
Yanga haikucheza vizuri katika dakika za kipindi cha kwanza na hii ilichangiwa
na sehemu ya kiungo kushindwa kufanya kazi yake vizuri.
Haruna Niyonzima na
Hassan Dilunga hawakuonekana kucheza mpira wao uliozoeleka na walitawaliwa na
viungo wa Mtibwa akiwemo Mkongwe Shaban Nditi.
Kutokana na Yanga
kufa sehemu ya kiungo, Cannavaro na Yondani walishindwa kutimiza majukumu yao
na mara kadhaa kulitokea presha kubwa langoni mwao.
Yondani alionekana
kukosa utulivu na kufanya baadhi ya faulo ambazo kwa bahati nzuri mwamuzi
hakuziona.
Kipindi cha pili,
Yanga walianza mpira kwa kasi wakishambulia kutoka upande wa kulia ambako
Mrisho Ngassa alionekana kuwa hatari zaidi.
Dakika ya 45 Ngassa
alipiga krosi kutoka winga hiyo ya kulia na ukagonga katika mkono wa nahodha wa
Mtibwa, Nditi na mpira kumpata Jaja aliyetia nyavuni, lakini mwamuzi alikataa
goli hilo na badala yake kutoa penalti.
Jaja katika dakika 46
alipewa penalti yake ya kwanza akiichezea Yanga, lakini alikosa baada ya kipa
Said Mohamed kuokoa kwa mguu wake wa kushoto.
Dakika moja baadaye,
Yanga walishambulia kwa kasi na Saimon Msuva aliyeingia kuchukua nafasi ya
Hamis Kiiza alitia nyavuni mpira, lakini mwamuzi msaidizi alikataa bao hilo
akidai winga huyo aliotea.
Dakika ya 51
Niyonzima alipiga mpira wa adhabu ndogo na kuunganishwa kwa njia ya kichwa na
Cannavaro, lakini ‘Mchawi’ wa Yanga leo hii, Kipa Mohamed aliudaka mpira huo.
Dakika ya 61,
Niyonzima alipiga mpira mwingine wa adhabu ndogo uliotua kichwani kwa Jaja ,
lakini kipa aliokoa kwa mara nyingine.
Jaja aliyepata mipira
minne mizuri, alitia kambani mmoja lakini goli lilikataliwa na mitatu alipiga
vichwa vya hatari. Hii inaonesha mshambuliaji huyo kutoka Brazil ni mtu wa
kuchungwa.
Dakika ya 69, Msuva
alienda golini kwa Mtibwa na kutoa mfuko wa ‘Gloves’ za kipa Said Mohamed
ingawa haikujulikani ni kwanini.
Kwa tamaduni za soka
la Tanzania, inawezekana Msuva amehisi mfuko ule ndio unawazuia kufunga magoli.
Kifupi ni kama imani za kishirikina.
Dakika ya 82 Amel
Ally alipata mpira mrefu na kusumbuana na Cannavaro akiwa na mwenzake Yondani,
akatishia akapiga mpira wa juu ambapo kipa Dida alipaa juu na kujaribu
kuokoa, lakini ukazama nyavuni na kuiandikia Mtibwa bao la pili.
Goli hilo lilitokana
na uzembe wa mabeki wa Yanga ambapo kwa muda mrefu timu yao ilikuwa
ikishambulia na mpira ulipopigwa hawakuwa tayari kukuabiliana na shambulizi
hilo la kushitukiza
Kwa ujumla kipindi
cha pili Yanga walitawala mpira na kufika langoni kwa Mtibwa mara nyingi zaidi,
lakini mambo yalikuwa magumu.
Katika kipindi hicho,
Yanga walimiliki mpira kwa asilimia 54 kwa 46, lakini haikuwasaidia kukwepa
kipigo hicho kutoka kwa wakata miwa wa Manungu Turiani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “YANGA YA MAXIMO YACHARAZWA 2-0 NA MTIBWA SUGAR JAMHURI...JAJA AKOSA PENALTI..”
Post a Comment