Monday, December 15, 2014

KIZAAZAA CHA UCHAGUZI, OFISI YACHOMWA MOTO SUMBAWANGA.




Wananchi ambao walishindwa kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mjini Sumbawanga, Rukwa jana walivamia na kuchoma moto Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kizwite iliyokuwa imesheheni vifaa vya kupigia kura.


Tukio la Sumbawanga ni sehemu ya vurugu zilizozuka katika maeneo mbalimbali nchini, ambako watu walirushiana makonde huku Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakitumia mabomu ya machozi kutuliza vurugu katika baadhi ya maeneo.

Vurugu zilizowahusisha wafuasi wa CCM na Chadema na katika maeneo mengine, zilikuwa baina vyama vya upinzani kwa jumla yake dhidi ya chama hicho tawala.

Mjini Sumbawanga, FFU waliingilia kati na kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wananchi walioonekana kuwa na jazba baada ya kushindwa kupiga kura kutokana na vituo kutokufunguliwa.

Awali, wananchi hao wengi wakiwa vijana, walifunga barabara inayoingia kwenye ofisi hiyo huku wakitoa onyo kwa magari ya Serikali kutokatisha eneo hilo. Kuona hivyo, mtendaji wa kata alikimbia kutoka ofisini hapo na kutokomea kusikojulikana.

Vurugu hizo pamoja na dosari nyingine kadhaa zilizojitokeza katika uchaguzi huo, zilisababisha Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbawanga, William Shimwela kutangaza kuahirisha uchaguzi kwenye kata tisa kati ya 19 zilizopo.

Alisema kwa mujibu wa sheria, iwapo uchaguzi ukigubikwa na dosari nyingi ana mamlaka ya kuahirisha. Alisema wamekubaliana na vyama vyote vya siasa kwamba uahirishwe hadi keshokutwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwarwanda alisema watu wawili wanashikiliwa kutokana na vurugu hizo.

0 Responses to “KIZAAZAA CHA UCHAGUZI, OFISI YACHOMWA MOTO SUMBAWANGA.”

Post a Comment

More to Read