Monday, December 15, 2014

WAHAMIAJI HARAMU WAKAMATWA TANGA.




Polisi wilayani Korogwe mkoani Tanga imewakamata wahamiaji haramu 12 wenye asili ya Ethiopia wakiwa wamefichwa katika gari lililokuwa likielekea Dar es Salaam.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Tanga, Freisser Kashai aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wahamiaji hao walikamatwa juzi saa 10:00 jioni katika kizuizi cha polisi kilichowekwa Kijiji cha Bwiko, Barabara ya Mombo-Segera.

Aliwataja watu hao kuwa ni, Kashoma Bayen (24), Berchano Gamada(32), Awal Jamal(23), Yanis Gatiso(28), Metson Sipril(21), Tashona Hayalis(30), Adino Samiru(20)Kengeny Siyun(22),Charnes Egesa(20), Abdi Badru(21), Siumanda Samadu (26) na Malako Abuu (23).
Alisema wakati wa mahojiano ilikuwa vigumu kuelewana kutokana na watu hao, waliokuwa katika hali mbaya kiafya, kutojua kuzungumza Kiswahili wala Kiingereza, hivyo kupata majina yao tu.

Alisema kwa sasa, polisi inaendelea kufanya upelelezi na mara baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuingia nchini bila kibali.

Akizungumzia kuhusu watu wanaofanya biashara ya kusafirisha watu, kamanda Kashai alisema polisi itaendelea kufanya upelelezi ili kuwabaini watu hao na kuwafikisha mahakamani.

0 Responses to “WAHAMIAJI HARAMU WAKAMATWA TANGA.”

Post a Comment

More to Read