Tuesday, January 27, 2015
:YULE JAMAA ALIYEJIFANYA TRAFIKI AFUNGWA JELA MIAKA SITA.
Do you like this story?
Aliyejifanya Askari Polisi wa Usalama Barabarani, James Hassan (54)
amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa
na sare za Polisi na kujifanya mtumishi wa jeshi hilo.
Aidha, adhabu hiyo ilitokana na makosa mawili ambapo mshitakiwa huyo
atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu mitatu kwa kila kosa.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Juma wa
Mahakama ya Wilaya ya Ilala, alisema kwamba ametoa adhabu hiyo ambayo haitaenda
kwa pamoja, kutokana na mshitakiwa huyo kuwa ni mkosefu mzoefu.
Pia alisema kwamba mahakama hiyo imemtia hatiani kupitia kwa mashahidi
watatu wa upande wa mashitaka walioithibitishia mahakama bila ya kuacha shaka.
Kabla ya hukumu, mshitakiwa huyo alidai kwamba kwa kuwa mahakama imemwona
kuwa ana hatia, yeye hakufanya kosa hilo na hata ikiwezekana mahakama imuachie
huru.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi hayo na badala yake
alihukumiwa kifungo hicho.
Wakili wa serikali, Florida Wenuslaus alidai kuwa mshitakiwa apewe adhabu
iwe fundisho kwa wengine.
Katika kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshitakiwa, ilibainika kwamba
mshitakiwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi
wa kutumia silaha, katika mahakama ya Wilaya ya Isanga, Dodoma na kufungwa
katika gereza la Isanga mkoani humo.
Pia mshitakiwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela kwa kosa la
kukutwa na sare za Jeshi la Polisi.
Katika barua iliyoandikwa na Mkuu wa Gereza la Keko kwenda kwa Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, iliithibitishia mahakama kwamba mshitakiwa huyo
alikuwa na kesi namba 32 ya mwaka 2004 na kwamba mshitakiwa alijiandikisha kwa
jina la Ally Kinanda.
Pia barua hiyo ilieleza kuwa Hassan alitoroka akiwa chini ya uangalizi wa
jeshi hilo na kwamba asipatiwe dhamana baada ya kukamatwa na kufikishwa katika
mahakamana hiyo, kwa kuwa mshitakiwa alikana kuhusika na tuhuma hizo na kueleza
kuwa watafuata taratibu zote kuchukua alama za vidole ili kuthibitisha kabla ya
kupatiwa dhamana.
Ilidaiwa kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 14, 2014 maeneo ya
Kinyerezi mnara wa Voda akijifanya kwamba ni askari polisi wa Usalama
barabarani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “:YULE JAMAA ALIYEJIFANYA TRAFIKI AFUNGWA JELA MIAKA SITA.”
Post a Comment