Friday, February 13, 2015
AGIZO HILI LA SERIKALI LADAIWA KUUA UBORA WA TAALUMA NCHINI.
Do you like this story?
SIKU chache baada ya Serikali kusema
itazifutia usajili shule zitakazokaidi agizo la kuweka viwango maalumu na
tofauti vya ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine, wadau wa elimu
wamezungumza na kusema agizo hilo linalenga kuua ubora wa taaluma nchini.
Akizungumza na HabariLeo, Katibu Mkuu
wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali
(TAMONGSCO), Benjamin Mkoya alisema viwango vinavyowekwa na shule binafsi
vinakubaliwa na wazazi na kuwa kinyume chake shule hizo zitakufa kutokana na
uwezekano wa kufifia ubora wa kitaaluma.
“Viwango vinavyoweka huwa vinakubaliwa
na wazazi, na lengo la kufanya hivyo ni kutaka shule zifanye vizuri hivyo
kuweza kujiendesha, kwani mbali na kutoa huduma, tunafanya biashara,” alisema
Mkoya.
Alisema suala la baadhi ya shule
kupanga viwango vya ufaulu limekuwa likifanyika muda mrefu na kuridhiwa na
wizara husika ya elimu Julai 2013, baada ya agizo la kuifungia shule ya
sekondari ya Mwilavya, Kasulu mkoani Kigoma iliyopandisha viwango vya ufaulu
hadi kufikia asilimia 45 kutokana na matakwa ya wazazi.
Mkoya alisema suala hilo lilifika
wizarani na uongozi wa TAMONGSCO kukutana na Naibu Waziri (wakati huo akiwa ni
Philipo Mulugo) ambaye alisema kama wazazi wameridhia viwango hivyo, shule
zinatakiwa kuendelea kufuata viwango hivyo.
“Tulikutana na uongozi wa wizara, na
hapa hatumuangalii mtu aliyekuwepo ofisini bali taasisi,” na tulizungumza hilo,
na hapo walisema kama wazazi wanaridhia viwango hivyo basi hakuna sababu ya
kugombana na wapiga kura ambao wanataka viwango vya juu,” alisema na kuongeza
kuwa kwa mwaka huu pekee wameshafanya vikao na viongozi wa Wizara ya Elimu mara
mbili kwa lengo la kuboresha sera ya elimu na suala zima la Matokeo Makubwa
Sasa (BRB).
Aidha, Mkoya alisema Serikali imekuwa
ikitoa maagizo mbalimbali yanaonekana kulenga kudhoofisha shule zisizo za
serikali, na kutolea mfano wa agizo lililotangulia lililotolewa na TAMISEMI
likizitaka shule hizo kutosajili wanafunzi mpaka hapo shule za serikali
zitakapojaa.
“Serikali inatakiwa kutoona shule hizi
kama ni ebola na kuzipiga vita, badala yake wazione kama partner (mshirika)
katika kuboresha elimu hasa katika kufikia BRN. Mkoya alisema wakati umefika
sasa, sekta ya elimu kuwa na taasisi huru ambayo itasimamia elimu hapa nchini
hivyo kuondoa mgongano wa kimaslahi kutoka kwa serikali ambayo ni wamiliki wa
shule na pia ndio wanaosimamia elimu. “Tunataka mamlaka huru kama ilivyo
SUMATRA, Wizara ndio yenye shule na ndio inayosimamia elimu, hapa hapatakuwa na
usawa,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Huduma ya Elimu kwa
Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) ambayo ni Bodi ya muungano wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo (CCT), Petro Pamba
alisema shule zao hazitakwepa mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu kwani
unaandaa wanafunzi na uwajibikaji kwa walimu.
Alisema taasisi yake yenye shule za
sekondari 368 nchi zima imekuwa ikiendesha shule kwa mifumo miwili ambayo ni shule
za seminari ambayo zinalenga kuwaandaa watumishi wa kanisa na ile ya kutoa
huduma ya elimu kwa jamii.
Alisema mfumo wa kupanga viwango vya
ufaulu umekuwa ukitumika muda mrefu na kujulikana na wizara na kwa sasa
hawawezi kuukwepa kwani umekuwa ukiwaandaa vizuri wanafunzi na uwajibikaji kwa
walimu.
“Mfumo wa kuweka viwango vya ufaulu
unawafanya walimu pia wajitathmini, ukiwaacha walimu huru basi nao wanabweteka,
hivyo sisi tutaendelea na mfumo huo kwani umekuwa ukifanyika muda mrefu na
mamlaka za elimu zinaelewa,” alisema.
Alisema viwango vilivyopo sasa ni kati
ya asilimia 40 hadi 49 na kuwa zaidi ya asilimia 50 kwa shule za seminari
ambazo zinaandaa watumishi wa kanisa.
“Huko kwenye seminari mchujo wetu ni
mkali sana kwa sababu ndio tunaowaandaa watumishi ambao watakuwa wakihudumia
jamii hivyo kutakiwa wawe vizuri kichwani,” alisema.
Hata hivyo, Pamba alisema taasisi yao
inakamilisha mfumo mbadala wa kuwasaidia wanafunzi wanaoelewa taratibu kwa
kuwaandalia mafunzo maalumu ili waweze kufanya vizuri mitihani ya mwisho na
kuwa wale wenye alama za chini watalazimika kurudia darasa.
Alisema pamoja na Wizara kutaka shule
kufuata Sera ya Elimu inayotaka viwango vya ufaulu kuwa ni asilimia 30, alisema
sera hiyo inaelekeza kwa wanafunzi wanapotakiwa kuvuka kutoka kidato cha pili
kwenda cha tatu na si katika madarasa mengine.
Alisema pia kiwango hicho cha ufaulu ni
cha chini ukilinganisha na mfumo mpya wa upangaji wa alama za ufaulu unaofanywa
na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ambayo ufaulu ni kati ya alama 40 hadi
49 (C), huku alama 30 hadi 39 ni ufaulu hafifu ambao unatoa daraja D.
Alisema kutokana na alama hizo kupitwa
na wakati, CSSC, imepeleka pendekezo wizarani kutaka kubadilishwa kwa viwango
vya ufaulu hadi kufikia alama 40 kwa kidato cha pili kwenda cha tatu.
Alipoulizwa Katibu wa Elimu wa Baraza
la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mohammed Jongo alisema: ”Wizara ndio wasajili wa
shule hapa nchini hivyo tutatekeleza agizo lao.”
Kwa nyakati tofauti wakijibu maswali
bungeni, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu
wake Anne Kilango Malecela walisema serikali itazifutia usajili shule zote za
serikali au binafsi, zitakazobainika kukaidi agizo la kuacha kuweka viwango
maalumu na tofauti za ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine.
Waraka wa Elimu Namba 6 wa mwaka 2011,
umetoa maelekezo kuhusu wastani wa ufaulu katika mtihani wa kidato cha pili
ambapo kiwango cha alama ya ufaulu ni asilimia 30 tu na si vinginevyo kwa shule
za serikali na binafsi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “AGIZO HILI LA SERIKALI LADAIWA KUUA UBORA WA TAALUMA NCHINI.”
Post a Comment