Wednesday, February 18, 2015
BUNDUKI ILIYOPORWA KWA POLISI TANGA NA MAJAMBAZI YAPATIKANA IKIWA NA RISASI ZAKE 20
Do you like this story?
POLISI mkoani Tanga imesema imefanikiwa
kupata bunduki aina ya SMG, ikiwa na risasi 20 ndani ya mapango ya Majimoto
katika eneo la Amboni, inayodaiwa ilikuwa ikitumiwa na wahalifu waliorushiana
risasi na askari mwishoni mwa wiki.
Aidha, imesema inashikilia watu kadhaa
akiwemo aliyesababisha kupatikana kwa bunduki hiyo. Baadhi ya watu wanaendelea
kuhojiwa, kupata taarifa kwa lengo la kukamata waliopora silaha kwa askari na
kurushiana risasi kwenye mapango hayo.
Kupatikana kwa silaha hiyo, kunafuatia
msako maalumu uliodumu kwa siku nne sasa, uliolenga kusaka silaha na wahalifu
wanaodaiwa kujificha ndani ya mapango ya mawe yaliyopo Amboni, nje kidogo ya
mji wa Tanga.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa
Jeshi la Polisi, Paul Chagonja alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari
mjini hapa.
Alisema mafanikio hayo, yametokana na
subira ya wakazi wa Tanga na ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuuonesha kwa
Polisi inayoshirikiana na vikosi vingine vya ulinzi na usalama, kufanya operesheni
ya pamoja kwenye eneo hilo.
“Kutokana na taarifa kutoka kwa
wananchi Februari 16 mwaka huu katika kitongoji cha la ‘Kona Z’ kilichopo
Amboni, tulifanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye kwa sasa sitamtaja jina kwa
sababu upelelezi unaendelea, tulimhoji kwa kina akatupa taarifa kuhusu silaha
hii,” alisema.
Alieleza, “Tulikwenda mpaka pangoni na
kufanikiwa kupata SMG hii ikiwa na magazini moja na risasi 20… silaha hii ni
miongoni mwa zilizoporwa kwa askari mwezi uliopita”.
Alisema licha ya kupatikana kwa silaha
hiyo, watu kadhaa wanashikiliwa wakihusishwa na tukio hilo. Alisema upelelezi
unaendelea kupata taarifa za kuwezesha kupatikana kwa silaha nyingine na vitu
mbalimbali vilivyowahi kuibwa.
“Naomba wakazi wa Tanga na Watanzania
kwa ujumla muendelee kuvuta subira na kutoa ushirikiano…endelezeni utulivu na
mshikamano kwa jeshi la polisi, ili kwa pamoja tuweze kumaliza tatizo hili,”
alisema.
Alisema upo umuhimu mkubwa kwa
wananchi, kuendeleza utulivu kwa kutokubali kuamini taarifa potofu zenye kujenga
hofu, zinazosambazwa na baadhi ya mitandao ya kijamii kwa kuwa zinalenga
kuwavuruga.
“Kimsingi jeshi la polisi pamoja na
vyombo vingine vya usalama, linaamini na kuthamini kazi ya vyombo vya habari
hasa vile makini, ambavyo vimeendelea kuwaarifu wananchi habari sahihi ambazo
hazina ghilba wala kuwachanganya”, alisema.
Alikanusha taarifa zilizoenea mjini
kwamba ipo miili ya wahalifu,iliyokutwa ndani ya mapango hayo, kutokana na
mapigano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
“Ndugu zangu mwanzoni tulikuwa
tukisikia harufu kali ya kama miili iliyooza, kweli tulijitahidi kutafuta na
tukafanikiwa kuona mizoga ya ngedere na siyo binadamu ...wanyama hao walikuwa
watatu na walikuwa na majeraha makubwa sana. Kwa hiyo hawakuwa watu, bali ni
ngedere ndio walikokuwa wamekufa na kuoza humo pangoni,” alisema.
Akizungumzia mkakati wa kupata silaha
iliyosalia na vifaa vingine vilivyoporwa, Chagonja alisema jeshi lake na kikosi
cha operesheni hakitalala usingizi mpaka vitu vyote vipatikane.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BUNDUKI ILIYOPORWA KWA POLISI TANGA NA MAJAMBAZI YAPATIKANA IKIWA NA RISASI ZAKE 20 ”
Post a Comment