Thursday, February 12, 2015
SERIKALI YAANZA KUSAMBAZA KWA WANANCHI KATIBA INAYOPENDEKEZWA
Do you like this story?
Serikali imeanza kusambaza nakala milioni mbili za
Katiba Inayopendekezwa nchini kote ili kuwawezesha wananchi kuisoma na
kushiriki katika Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika tarehe 30 Aprili mwaka
huu.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro
amesema JANA (Jumatano, Februari 11, 2015) jijini Dar es Salaam kuwa kati ya
nakala hizo zilizochapwa jijini Dar es Salaam, nakala 1,800,000 zinasambazwa
Tanzania bara na nakala 200,000 zinasambazwa Tanzania Zanzibar.
Kwa mujibu wa Waziri Migiro, hadi kufikia jana
(Jumanne, Februari 10, 2015), jumla ya nakala 707,140 zilikuwa zimesambazwa
katika mikoa 12 ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ambayo imepata nakala
200,000 na kuwa kazi hiyo inaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika katika
muda mfupi ujao.
Mikoa hiyo na nakala ziliozosambazwa katika mabano
ni Katavi (15,640), Rukwa (27,040), Ruvuma (47,740), Mbeya (78,640), Simiyu
(34,840), Mara (52,540), Tabora (58,540) na Kigoma (41,440). Mikoa mingine ni
Kagera (54,340), Geita (36,940), Mwanza (57,040) na Pwani ambapo usambazaji
umeanza kwa wilaya ya Mafia ambayo imepata nakala 2,400.
“Idadi ya nakala ya Katiba Inayopendekezwa kwa kila
mkoa inategemea na wingi wa kata katika mkoa, ndiyo maana baadhi ya mikoa unaona
imepata nakala nyingi,” amesema Dkt. Migiro ofisini kwake wakati akiongea na
baadhi ya waandishi wa Habari waliotaka ufafanuzi kuhusu hatua iliyofikiwa
katika kazi ya uchapishaji na uasambazaji wa nakala za Katiba Inayopendekezwa.
Kwa mujibu wa Waziri Migiro, kuna zaidi kata 3,800
nchini kote na lengo la Serikali ni kusambaza nakala 300 katika kila kata
ambazo zitasambazwa kwenye vijiji, vitongoji na mitaa kupitia Ofisi za Wakuu wa
Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji.
Kuhusu taasisi za elimu na dini, Waziri Migiro
amesema Serikali imepanga kusambaza nakala 658,400 kwa taasisi za elimu, dini,
vyama vya siasa na asasi za kiraia na kuwa usambazaji huo utaanza hivi
karibuni.
Pamoja na usambazaji huo, Waziri Migiro amewakumbusha
wananchi ambao bado hawajapata nakala za Katiba Inayopendekezwa, kuisoma
kupitia tovuti ya Wizara ya Katiba na Sheria (www.sheria.go.tz) na
tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (www.agctz.go.tz).
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SERIKALI YAANZA KUSAMBAZA KWA WANANCHI KATIBA INAYOPENDEKEZWA ”
Post a Comment