Tuesday, February 24, 2015
WALIMU ZAIDI YA 200 WALUNDIKANA MANISPAA YA IRINGA...PINDA ATOA AMRI KWA MKURUGENZI.
Do you like this story?
WAZIRI MKUU
Mizengo Pinda amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Bw. Ahmed Sawa akae
pamoja na Afisa Elimu wake na kuwapunguza walimu 230 waliozidi mahitaji ya
walimu kwenye manispaa hiyo na badala yake wawapangie kwenda vijijini.
Ametoa agizo
hilo jana jioni (Jumapili, Februari 22, 2015) wakati akizungumza na mamia ya
wakazi wa kata ya Ipogolo waliofika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye viwanja vya shule ya msingi Ipogolo, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa.
“Manispaa
inahitaji walimu 534 lakini waliopo ni 764. Hapa kuna ziada ya walimu 230 tena
kw shuke za msingi... Mkurugenzi kaa na Afisa elimu wako muwaondoe walimu
waliozidi na kuwapangia waende vijijini ambako kuna mahitaji zaidi,” alisema.
“Kwa upande
wa shule binafsi nako pia tatizo ni lile lile. Walimu wamezidi. Mahitaji ni
walimu 75 waliopo ni walimu 142 ... wanaozidi ni walimu 67,” alisema Waziri
Mkuu.
“Sina tatizo
na walimu wa shule binafsi kwa sababu wao wana mfumo wao wa ajira lakini hawa
wa shule za Serikali ni lazima muwaondoe tena haraka sana. Waondoeni waende
vijijini kwenye mahitaji makubwa sababu ualimu ni ualimu tu, siyo lazima mtu
awe mjini ndiyo afundishe vizuri,” alisema.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu aliupongeza uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kuwa na ufaulu
wa juu kwenye shule za msingi lakini akawataka wajiulize ni kwa nini ufaulu huo
umeanza kushuka tangu mwaka 2013.
“Mwaka 2010
kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 77; mwaka 2011 kilikuwa asilimia 87; mwaka
2012 kilipanda na kufikia asilimia 97. Lakini mwaka 2013 kilishuka hadi
asilimia 82 na mwaka jana ni kama kipo palepale kwani kilikuwa asilimia 82.5.
Kaeni mjiulize kumetokea nini na mtafanya nini ili kurudi tena kwenye asilimia
97 au zaidi.”
Akizungumzia
suala la afya, aliwaeleza wananchi hao kwamba ameuagiza uongozi wa mkoa kupitia
watoa tiba wake waweke utaratibu wa kutoa elimu walau kila baada ya miezi
miwili au mitatu ili wananchi wapate ufahamu wa magonjwa makuu yanayosumbua
hivi sasa.
Akifafanua
magonjwa ya akinamama, Waziri Mkuu aliyataja magonjwa hayo kuwa ni saratani ya
matiti, saratani ya shingo ya uzazi na tatizo la fistula wakati kwa upande wa
akinababa alisema wao wanahitaji kupatiwa elimu zaidi kuhusu ugonjwa wa tezi
dume.
“Matatizo
haya yanatibika lakini ni lazima watu waeleweshwe kwamba wakiwahi kwenda
hospitali matatizo haya yanatibika lakini wakichelewa inakuwa tatizo zaidi,”
alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WALIMU ZAIDI YA 200 WALUNDIKANA MANISPAA YA IRINGA...PINDA ATOA AMRI KWA MKURUGENZI.”
Post a Comment