Tuesday, February 24, 2015

ZIARA YA WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA MKOANI MBEYA,IMEZUA UTATA KWA WAANDISHI WA HABARI.


Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mbeya Wakisikiliza kwa makiini Kuhusu ujio wa Waziri Mkuu Mh Mizengo Pinda



Na Pendo Fundisha, Mbeya.
ZIARA ya Waziri  Mkuu mizengo Pinda Mkoani Mbeya, imezua utata kwa waandishi wa habari, kutokana na kile kinachoonekana kuwepo kwa ubaguzi  kwa vyombo vya habari kutohusishwa  katika ziara hiyo.

Utata huo umeibuka jana, katika kikao  maalum kilichoitishwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na waandishi wa habari, lengo likiwa ni kutoa taarifa ya ujio wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, inayotarajia kuanza kesho(leo) Mkoani Mbeya na kutembelea halmashauri saba.

Katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro, aliwafahamisha waandishi wa habari, kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda atawasili Mkoani Mbeya kesho  na kwamba yupo katika ziara ya kikazi.

“Ndugu zangu waandishi wa habari nimewaiteni hapa, kuwafahamisha kwamba Waziri Mkuu atawasili Mbeya na kuanza ziara ya kikazi na kwamba atatembelea halmashauri saba za mkoa wa Mbeya,”alisema Kandoro.

Hata hivyo,  baada ya Mkuu huyo, kumaliza kutoa taarifa hiyo, baadhi ya waandishi wa habari akiwemo Mhariri Kanda za Nyanda za Juu Kusini Kampuni ya Free Media na mwandishi mkongwe wa gazeti la Tanzania Daima, Christopher Nyenyembe, aliomba kupatiwa utaratibu kuhusu waandishi wa habari watakavyofanya kazi kwenye ziara hiyo.
Akitoa utaratibu huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro, alieleza kwamba  utaratibu wa vyombo vitakavyoshiriki ziara hiyo, umefanyika tayari kwa kutumia viongozi wa chama cha waandishi wa habari wa Mkoa wa Mbeya.

“Ofisi iliwasilisha taarifa kwa uongozi wa klabu na kuomba kupatiwa vyombo kumi vya habari vitakavyoshiriki kwenye ziara hii na klabu yenu ilituwasilishia vyombo hivyo ambavyo ni Itv, Nipashe, Tbc, Chanel Ten, Star TV, Mwananchi, Habari Leo, Uhuru Mzalendo, Radio Bomba Fm na Mbeya FM,”alisema.

Kiongozi huyo, alipomaliza kutoa ufafanuzi huo ndipo Mwandishi Christopher Nyenyembe ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa Mbeya Press Club, alihoji juu ya vyombo vingine vya habari ambavyo vimekuwa na mchango mkubwa kwa serikali hiyo ya Mkoa lakini havimo kwenye orodha.

“Ujio wa Pinda ni wa kitaifa, hivyo vyombe vyote vya habari vinahaki ya kupata taarifa na kuwapasha wananchi kipi kinachoendelea lakini kwa hili lililojitokeza hatuwezi kuitupia lawama  ofisi ya Mkuu wa Mkoa haya ni mapungufu na udhaifu mkubwa unaofanywa na viongozi wa Press Klabu,”amesema.

Amesema,tatizo  lililopo ni  kwamba klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya,aina mshikamano, imekuwa ya kwanza kuwagawa wanachama hivyo kuiendesha klabu kwa urafiki zaidi hali ambayo ni hatari kwa tasnia hii ya habari nchini huku ikipoteza lengo halisi la uanzishwaji wa Press hizo mikoani ulioanzishwa na Baraza la habari nchini(UTPC).

Amesema, waandishi wa habari wamekuwa wakiitegemea klabu kama muhimili wa kuwajenga na kuwaimarisha kitaaluma lakini hivi sasa muhimili huo umegeuka shubiri kwa baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wake.
 
“Waandishi wanaitegemea  klabu kama  muhimili wa  kuwajenga lakini Press hii imegeuka sehemu ya kuwabomoa kitaaluma na kwamba endapo jambo hilo litafumbiwa macho klabu hiyo, itabaki na watu wachache ambao hawatakuwa na nafasi ya kuwasaidia waandishi badala yake kuangalia maslahi yao,”amesema.

Hata hivyo, alimaliza kwa kuwataka waandishi wa habari kutoitupia lawama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mbeya, kwamba imekuwa inawabagua kwani tatizo lipo kwa viongozi wa klabu ambao wamepewa jukumu hilo na kushindwa kuvitendea haki baadhi ya vyombo vya habari.
Mwisho.

0 Responses to “ZIARA YA WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA MKOANI MBEYA,IMEZUA UTATA KWA WAANDISHI WA HABARI.”

Post a Comment

More to Read