Tuesday, March 3, 2015

HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI, 2015, YAMHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ILIYOTOLEWA TAREHE1 MACHI, 2015.





HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI, 2015, YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ILIYOTOLEWA TAREHE 1 MACHI, 2015

Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuzungumza kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa hotuba za kila mwisho wa mwezi.  Kwa mwisho wa mwezi wa Februari nina mambo matano ninayopenda kuyazungumzia. 
Zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura
Ndugu Wananchi;
          Jambo la kwanza ni uandikishaji wa Wapiga Kura.  Tarehe 24 Februari, 2015 Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda alizindua rasmi uandikishaji wa wapiga kura ikiwa ni sehemu ya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchini.  Zoezi hili lilizinduliwa Makambako, Mkoani Njombe na litaendelea nchini kote mpaka litakapokamilika kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa na Tume ya Uchaguzi.  Uandikishaji unatumia teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa alama za vidole (BVR) na macho ya mtu anayeandikishwa.  Teknolojia hii itatusaidia kuondoa kutoaminiana, manung’uniko na madai kuhusu udanganyifu katika chaguzi zetu kwamba wamepiga kura wasiostahili.  Kuanza kutumika kwa teknolojia hii ni kielelezo cha utashi wa Serikali kuwa nchi yetu iwe na chaguzi zilizo huru, wazi na haki.

Ndugu Wananchi;
          Mtakumbuka kuwa, kabla ya uzinduzi wa zoezi hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya zoezi la majaribio ya uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia mashine za teknolojia hii mpya katika kata 10 katika Halmashauri za Kinondoni, Kilombero na Mlele kati ya tarehe 15 hadi 23 Desemba, 2014.  

          Habari njema ni kuwa, kwa kutumia mashine za BVR, idadi ya waliojiandikisha ilivuka lengo la uandikishaji kwa kipindi kilichopangwa katika Kata hizo.  Katika Halmashauri ya Kilombero walioandikishwa walifikia asilimia 110.9 ya lengo, katika Halmashauri ya Mlele uandikishaji ulifikia asilimia 101 ya lengo na katika Jimbo la Kawe, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni walioandikishwa walikuwa asilimia 105.67 ya lengo.    Mafanikio haya ni ya kutia moyo pamoja na changamoto za kiufundi zilizojitokeza na zile zinazotokana na upya wa mfumo wenyewe kwa watumiaji.  Changamoto hizo zimefanyiwa kazi na watengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika awamu hii ya uandikishaji wa wapiga kura nchi nzima. 

Ndugu Wananchi;      
Nimefarijika na taarifa kuwa zoezi la uboreshaji wa Daftari na uandikishaji wa wapiga kura limeanza vizuri Makambako.  Wananchi wamejitokeza kwa wingi kuliko ilivyotarajiwa.  Kati ya tarehe 23 hadi 25 Februari, 2015 kwa mfano, Tume ilitegemea kuandikisha wapiga kura 9,541 lakini kutokana na mwamko wa wananchi kuwa mkubwa wameweza kuandikisha wapiga kura 13,042.  Kila kituo kilikuwa kinaandikisha kati ya wapiga kura 80 na 150 kwa siku.  Lengo la Tume ni kuandikisha wapiga kura 32,000 katika Halmashauri ya Makambako ambako kwa siku wanatarajia kuandikisha watu 4,320.  Naambiwa kuwa hesabu za juzi na jana wameandikisha hadi wapiga kura 6,000 kwa siku.  Kwa kasi hii na kama mambo yatakwenda kama inavyotarajiwa, lengo hilo litafikiwa na hata kuvukwa.

Ndugu Wananchi;
          Hatuna budi kutoa pongeza kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa hatua hii ya kutia moyo tuliyofikia katika mchakato huu.  Inaondoa hofu iliyoanza kuingia miongoni mwa baadhi ya watu kuwa huenda zoezi hili lisingefanikiwa.  Tunachokitaka kwa Tume ni kuona zoezi hili linaendelea na kukamilika kama ilivyopangwa. Napenda kurudia ahadi niliyokwishaitoa kwa Tume kwamba Serikali itafanya kila linalowezekana kuiwezesha kirasilimali ili iweze kutimiza jukumu lake hilo.  Nimekwishawakumbusha Hazina kuhusu umuhimu wa zoezi hili kufanikiwa kama ilivyopangwa.  Hivyo basi, nimewataka wahakikishe kutoa kipaumbele cha kwanza katika mgao wa fedha.   Kama haifanyiki nawaomba Tume waniambie mimi mwenyewe.

          Wito wangu kwenu, wananchi wenzangu, ni kujitokeza bila ya kukosa kwenda kujiandikisha kwa mujibu wa ratiba ya uandikishaji katika maeneo yenu kama itakavyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.  Msifanye ajizi maana hakutakuwepo na fursa nyingine ya kujiandikisha kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu baada ya fursa hii kupita.  

Ndugu Wananchi;
Kama ilivyoelezwa na Tume na mimi kusisitiza mara kadhaa kuwa watakaojiandikisha wakati huu ndio watakaopiga kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa na ndio watakaopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.  Vitambulisho vya zamani vya mpiga kura havitatumika, hivyo watu wote ambao ni Watanzania na wana umri wa miaka 18 au zaidi lazima wajitokeze kuandikishwa upya. Watu pekee ambao hawatapaswa kujiandikisha tena ni wale tu walioandikishwa katika zoezi la majaribio lililofanyika katika zile kata 10 za Halmashauri za Kinondoni, Ifakara na Mlele mwezi Desemba, 2014.  Vitambulisho walivyopata ndivyo vyenyewe.

Ndugu Wananchi;
          Napenda kutumia nafasi hii pia kuwaomba viongozi wa vyama vya siasa, Serikali, dini na asasi za kiraia kuungana na Serikali na Tume ya Uchaguzi katika kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi wakajiandikishe.  Naomba tusiwachanganye wananchi kwa kutoa taarifa zisizokuwa za kweli na kuwafanya wakaacha kujiandikisha. Sisi katika Serikali tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa kila atakayejitokeza kujiandikisha anaandikishwa. Aidha, tutahakikisha kuwa kila panapojitokeza changamoto zinatafutiwa ufumbuzi kwa wakati mwafaka.  

Tunatambua kuwa mfumo huu ni mpya hivyo panaweza kujitokeza changamoto zinazosababishwa na upya wake.  Nawaomba wahusika kuendelea kuwaelimisha watendaji wanaohusika ili wapate uzoefu unaostahili.  Aidha, nawasihi wananchi kuwa wavumilivu na waelewa pale ambapo wakati mwingine watalazimika kukaa kwenye mistari kwa muda mrefu kusubiri kujiandikisha, au wakalazimika kuja siku ya pili. 

Ndugu Wananchi;
 Kupiga kura kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa au kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani ni haki na wajibu wa kila raia.  Lakini, kuipata haki hiyo na kuweza kutimiza wajibu huo kunategemea kuwa na kitambulisho cha mpiga kura.  Bila ya hivyo haiwezekani.  Haya shime jitokezeni, mjiandikishe, ili muweze kuitumia haki yenu na kutimiza wajibu wenu wa kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa na kuchagua viongozi mnaowaona wanafaa kuongoza nchi yetu, jimbo lako na kata yako.
Kura ya Maoni
Ndugu Wananchi;
          Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia ni kuhusu Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.  Kama mjuavyo, baada ya Bunge Maalumu la Katiba kutunga Katiba Inayopendekezwa na Rais kuchapisha Katiba hiyo katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni, kinachoendelea sasa ni matayarisho ya kufanyika kwa kura hiyo.  Yapo majukumu ya Serikali, yapo majukumu ya Tume ya Uchaguzi, na yapo majukumu ya Serikali na Tume kwa pamoja.  Utekelezaji umeishaanza na unaendelea.  Miongoni mwa mambo yanayotakiwa kufanyika ni uandikishaji wa wapiga kura ambao umekwishaanza na unaendelea. 

 Ipo pia kazi ya kuchapisha na kusambaza Katiba Inayopendekezwa ili wananchi waweze kuisoma na kuielewa kabla ya kupiga kura ya maoni.  Tayari Katiba Inayopendekezwa imetangazwa katika tovuti za Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo na katika tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.  Pia imechapichwa magazetini.  

Hadi tarehe 27 Februari, 2015 vitabu 1,558,805 vilikuwa vimechapishwa na nakala 1,341,300 kusambazwa.  Nakala 1,141,300 zimesambazwa kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara na nakala 200,000 zimegawiwa kwa Zanzibar.  Kwa upande wa Tanzania Bara kila Kata imepewa vitabu 300.  Kwa vile Kata zina wastani wa vijiji vitano (5) hii ina maana kwamba kila kijiji kimepata vitabu 60 kwa kila kijiji ambayo si haba.  

Ndugu Wananchi;
Tume ya Uchaguzi itatoa maelekezo kuhusu utaratibu wa kutoa elimu kwa umma.  Nimeambiwa tayari asasi za kiraia 420 kwa upande wa Bara na 75 kwa upande wa Zanzibar zimejiandikisha kwa ajili ya zoezi hilo. Halikadhalika, Tume itatoa maelekezo husika kuhusu kampeni ya Kura ya Maoni wakati ukiwadia.  Naomba watu wawe na subira na kuzingatia masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni na Kanuni zake.  Tukifanya hivyo, zoezi hili muhimu na la kihistoria litatekelezwa kwa usalama na utulivu.  Watu watafanya uamuzi kwa uhuru, uelewa, amani na usalama.  
Hali ya Usalama Nchini
Ndugu wananchi;
          Jambo la tatu ninalotaka kulizungumzia ni hali ya usalama nchini.  Kwa jumla hali ya usalama ni nzuri, hata hivyo kuna matukio ya kiusalama ambayo ningependa kuyazungumzia.  La kwanza ni mashambulizi yenye sifa za ujambazi na mwelekeo wa kigaidi.  Na, la pili ni la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Katika kipindi cha miezi 12 hivi kumekuwa na matukio ya watu kuvamia vituo vya Polisi, wengine wanachoma moto au wengine wanapora silaha.  Pia kumekuwepo na matukio ya kuwashambulia Polisi walioko kwenye doria na wengine kuporwa silaha.  Vituo vya Polisi vilivyovamiwa na silaha kuporwa ni vya Newala Mkoani Mtwara silaha tatu ziliporwa, Ikwiriri katika Wilaya ya Rufiji silaha saba, Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga silaha tano, mbili za polisi na tatu za raia waliokwenda kuzihifadhi pale, na Ushirombo Wilaya ya Bukombe silaha 18.  Pugu Machinjioni na Tanga, askari waliokuwa katika shughuli za ulinzi na doria walishambuliwa na kuporwa silaha tatu.  Kule Songea kulikuwepo na matukio mawili ya Polisi kushambuliwa lakini silaha hazikuporwa.

Bahati mbaya, vijana wetu saba wa Jeshi la Polisi walipoteza maisha katika matukio hayo.  Newala alikufa Polisi mmoja, Kimanzichana mmoja, Ikwiriri wawili, na Ushirombo watatu. Wapo Polisi kadhaa waliopata majeraha ya namna mbalimbali katika mashambulizi haya.  

Ndugu Wananchi;
Silaha zote 18 zilizoporwa Ushirombo zimepatikana na watu 10 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo wamekamatwa.  Katika tukio la Tanga silaha moja kati ya mbili zilizoporwa imepatikana.  Watuhumiwa saba wametiwa mbaroni, wanne  kati yao ni wale waliokuwa wamejifisha katika mapango ya Kiomoni katika Kitongoji cha Karasha-mikocheni, kilichoko kijiji cha Mzizima wilayani Tanga. Tayari watu wanne wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la Ikwiriri wamekamatwa.  Polisi wanaendelea na upelelezi kuwapata watu wengine na kuzipata silaha saba zilizoporwa kituoni hapo.  Kwa tukio la Newala silaha zote tatu zimepatikana pamoja na bastola moja ya mtuhumiwa aliyehusikaa  na watu wawili wametiwa nguvuni.  Hali kadhalika, upelelezi unaendelea wa kuzipata silaha zilizoporwa ambazo hazijapatikana mpaka sasa: yaani Kimanzichana moja, Pugu Machinjioni moja na Tanga iliyosalia moja. 

Ndugu Wananchi;
          Matukio haya yana sura mbili.  Yana sura ya ujambazi, lakini pia baadhi yake yana dalili za ugaidi.  Vyombo vyetu vya usalama vinaendelea kufanya kazi yake ya uchambuzi wa kila tukio na kulipa nafasi yake stahiki.  Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa Jeshi la Polisi wakishirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na vyombo vingine vya usalama kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo kupambana na uhalifu nchini.  Mafanikio tunayaona, kama nilivyoeleza na kama tulivyosikia kule Tanga hivi karibuni ni matunda ya ushirikiano huo.  Hata hivyo, nimewataka waendelee kuwasaka watu hawa waovu po pote walipo ili wafikishwe mahakamani na kuzirejesha mikononi mwa Polisi silaha zote zilizoporwa. 

Nawaomba wananchi wenzangu wote kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama hususan Jeshi la Polisi ili tuweze kupata mafanikio zaidi dhidi ya uhalifu huu na uhalifu mwingineo. Nawaomba mfanye mambo mawili:  Kwanza, toeni taarifa Polisi mnapozipata habari za vitendo viovu au nyendo za watu waovu wanavyokusudia kufanya wahalifu au taarifa za wale waliokwishafanya uhalifu.  

Pili, naomba watu waache kuwashabikia watu hawa waovu wala kueneza taarifa zao potofu kwenye mitandao ya kijamii.  Badala yake tutumie mitandao ya kijamii kuponda fikra zao potofu, fikra zao hasi na vitendo vyao viovu pamoja na kuwafichua wao na mambo yao mabaya wayafanyo.  Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wote walioweza kutoa taarifa zilizowezesha kuzuia uhalifu usifanyike au zilizowezesha kutiwa mbaroni kwa wahutumiwa wa vitendo vya ujambazi na ugaidi.    Hatuwezi kushinda uhalifu bila ushirikiano baina ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi
Ndugu wananchi;
          Nimesikitishwa sana na taarifa kuwa mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) yameibuka upya baada ya hali kuwa tulivu mwaka 2011.  Mwaka jana (2014) yalitokea matukio matatu katika mikoa ya Mwanza, Tabora na Simiyu na mwaka huu limetokea tukio moja mkoani Geita. 

Lazima tulaani vikali mauaji ya ndugu zetu albino.  Ni vitendo vya kinyama ambavyo havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yeyote ya watu waliostaarabika, ya watu wanaomuabudu Mungu.  Watu wenye ulemavu wa ngozi ni wanadamu wenzetu, wenye haki sawa ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao kama walivyo wanadamu wengine.  Hawastahili kufanyiwa wanayofanyiwa.  Hawapaswi kuishi kwa hofu katika kijiji chao, mtaa wao au katika nchi yao.  Jamii nzima na sisi sote mmoja mmoja na katika umoja wetu, tunao wajibu wa kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao kama ilivyo  kwa watu wengine wote.  

Kwa kweli, mauaji ya albino ni jambo linalofedhehesha na kulidhalilisha taifa letu.  Ni vitendo visivyovumilika.   Hatuna budi sote kushikamana na kuhakikisha kuwa tunapambana nao kisawasawa na kuwashinda.  Tusikubali kamwe wakaturudisha kule kubaya tulikokuwa zamani.    Naungana na Chama cha Albino Tanzania kulaani ukatili huu na kutaka watu wote wanaojihusisha na ukatili huu wasakwe, wakamatwe, wafikishwe Mahakamani na kupewa adhabu kali inayowastahili wanapopatikana na hatia.  

Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa wakati wote Serikali imelipa uzito mkubwa suala la kudhibiti na kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi au kukatwa baadhi ya viungo vyao wenyewe wakiwa hai.  Tumefanya hivyo bila ya kuchoka tangu tukio la kwanza baada ya mimi kuingia madarakani Aprili 17, 2006 na miezi mitatu tu  kule Nyahunge, Geita alipouawa Alfa Amon ambapo watuhumiwa wawili waliuawa na raia.  Mwaka 2007 kulikuwa na matukio saba.  Mwaka 2008 ndio ulikuwa mwaka mbaya sana walipouawa watu 18.  

Kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wananchi mauaji yalipungua na kuwa tisa mwaka 2009.  Mwaka 2010 kukawa na tukio moja na mwaka 2011 hapakuwepo na tukio lolote.  Mwaka 2012 kukawa na tukio moja, mwaka 2013 aliuawa mtu mmoja na wawili kujeruhiwa.  Mwaka 2014 waliuawa watu watatu na wawili kujeruhiwa, na Januari, 2015 kumetokea tukio moja kule Geita.  

Ndugu Wananchi;
          Tangu mwaka 2006 mpaka 2015, watuhumiwa 139 wametiwa nguvuni, miongoni mwao wako watuhumiwa 16 wa matukio ya Desemba na Januari mwaka huu. Mashauri 35 yamefunguliwa mahakamani na kati ya hayo 10 bado yanaendelea na yapo katika hatua mbalimbali.  Watuhumiwa 73 wameachiliwa na 15 wamepatikana na hatia.  Kati ya hao waliopatikana na hatia 13 wamehukumiwa kifo na wawili wamepata kifungo cha miezi 6.  Watuhumiwa kwa matukio sita bado wanasakwa.

          Matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yametokea katika mikoa kumi kati ya mikoa 30 hapa nchini.  Mikoa hiyo ni hii ifuatayo:  Mwanza matukio 13, Kagera sita, Tabora matano, Geita manne, Mara manne, Kigoma manne, Simiyu matatu, Shinyanga mawili, Arusha moja na Mbeya moja.  Utaona matukio 41 kati ya 43 yametokea katika ukanda wa ziwa ambapo pia wanaongoza kwa mauaji ya vikongwe na wanawake kwa sababu za ushirikina.  

Ndugu Wananchi;
          Inawezekana kuwa matukio ya hivi karibuni yanaashiria kuwa uhalifu huu unataka kuibuka upya. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na Watanzania kwa jumla, kuwa hatutaacha hali iwe mbaya kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.  Tutatumia mbinu na maarifa tuliyoyatumia kukabili wimbi kubwa la mauaji lililokuwepo mwaka 2007 na 2008 na kwa sababu hiyo tukaweza kupunguza hadi kufikia kutokuwa na tukio lolote la mauaji mwaka 2011.  

Tunachokiomba kutoka kwa wananchi ni ushirikiano na msaada wa kuwafichua watu wanaofanya vitendo vya mauaji na kukata viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.  Pia wasaidie kutoa taarifa kuhusu wanunuzi wa viungo hivyo na waganga wanaochochea mahitaji ya viungo vya albino.  Ushirikiano wa wananchi wa wakati ule uliwezesha kupatikana kwa mafanikio niliyaeleza.  Naamini safari hii tukifanya hivyo tutafanikiwa pia.

Ndugu Wananchi;      
Kutokomeza kabisa matukio ya mauaji na ukataji wa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi ni jambo linalowezekana.  Hata hivyo, litategemea watu kuacha imani za ushirikina.  Imani potofu, ati kuwa mtu akiwa na kiungo cha mtu mwenye ulemavu wa ngozi atafanikiwa katika shughuli zake za biashara, uvuvi na uchimbaji wa madini ndicho kichocheo cha uovu wote huu unaoendelea.  Ni ujinga ulioje kwa mtu kuamini kuwa mafanikio yake hayatategemea juhudi zake na maarifa yake bali kuwa na kiungo cha mwanadamu mwenzake mwenye ulemavu wa ngozi.  
 
Nilisema katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi Machi, 2008 kwamba, kama kuwa na kiungo cha albino ndiko kutakakomfanya mtu kufanikiwa katika shughuli zake za kibiashara na kiuchumi basi ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi wangekuwa ndiyo matajiri wakubwa nchini na duniani.  Maana wao sio tu wana viungo bali wana mwili mzima.    Kwa sababu ya kuwepo imani hizi za hovyo, juhudi za kuelimisha jamii kuachana na imani hizi potofu ziongezwe.  Naomba hili ndilo liwe jambo la msingi katika mapambano haya.  Tukifanikiwa katika hili, matatizo yote haya yatakoma.  Serikali na jamii haitalazimika kushughulikia mambo haya ambayo siyo tu ni fedheha hata kumsimulia mtu bali yanatisha na kusikitisha.

Ndugu Wananchi;
          Wiki ijayo nitakutana na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi.  Nimekubali maombi yao ya kukutana nao ili niweze kusikiliza maoni yao na tubadilishane mawazo juu ya namna bora ya kumaliza tatizo hili.  Mimi naamini kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na jamii utatuwezesha kutokomeza mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na kuliondolea taifa letu aibu hii.
Ziara ya Zambia
Ndugu Wananchi;
          Tarehe 25 na 26 Februari, 2015 nilifanya ziara ya siku mbili ya kiserikali nchini Zambia kwa mwaliko wa Rais mpya wa nchi hiyo, Mheshimiwa Edgar Lungu.  Ziara ilikuwa na mafanikio makubwa.  Mimi na ujumbe wangu tulifarijika sana kuona kuwa mawazo ya nchi zetu mbili yanashabihiana sana kuhusu namna ya kuimarisha na kuboresha uhusiano wetu na ushirikiano na uhusiano wa nchi zetu mbili.  Kimsingi tumekubaliana katika masuala yote muhimu tuliyoyazungumza.   

Kuhusu TAZARA tumekubaliana kuchukua hatua thabiti kutatua matatizo ya kiungozi, kifedha na kiufundi yanayolikabili shirika letu hilo hivi sasa.  Tumeelewana kuwa hatuna budi kufanya marekebisho ya kimfumo na kiutendaji ili kutatua matatizo ya kimuundo na kimenejimenti yanayochangia kuzorota kwa ufanisi wa Shirika.    Tumekubaliana pia kuwa, Serikali zetu mbili zitekeleze ipasavyo wajibu wake kwa TAZARA ikiwa ni pamoja na kutoa mchango wake wa fedha kwa ajili ya kulifufua Shirika hili muhimu kwa uchumi wa nchi zetu mbili. 

Ndugu Wananchi;
Tumekubaliana pia, kwamba, tuangalie uwezekano wa kuruhusu makampuni au mashirika mengine ya reli kutumia reli ya TAZARA kusafirishia mizigo yao kwa kulipa ushuru kwa TAZARA kwa huduma hiyo.  Tumeagiza Baraza la Mawaziri kulifanyia kazi wazo hili jema ili litekelezwe mapema iwezekanavyo. 

Kwa upande wa sekta ya nishati, tumekubaliana  kuwa, nchi zetu mbili ziendelee kushirikiana kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA. Ndugu zetu wa Zambia walitueleza dhamira yao ya kutaka kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam hadi Zambia.  Wameomba tukubali kuwauzia gesi asilia.  Niliwaeleza ni jambo linaowezekana, tumekubaliana nchi zetu zilifanyie kazi ombi hilo.

Serikali ya Zambia, imeahidi kuimarisha njia ya umeme kutoka Kasama hadi Mbala Zambia inakoanzia njia inayoleta umeme Sumbawanga.  Kufanya hivyo kutaondoa matatizo ya sasa ambapo umeme unaofika Sumbawanga kutoka Mbala huwa mdogo kiasi kwamba hauna nguvu ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani, maofisini na viwandani.  Kwa sababu hiyo, hata mpango wa kuupeleka umeme huo Namanyere, Nkasi na Mpanda haukuweza kutekelezwa kama ilivyokuwa imekusudiwa awali.

Ndugu Wananchi; 
Kuhusu kuboresha huduma kwa abiria na mizigo katika mpaka wa Tanzania na Zambia pale Tunduma, tumekubaliana kuwa, Serikali ya Tanzania ikamilishe ujenzi wa jengo  litakalowezesha huduma zote muhimu za mpakani kutolewa katika jengo hilo (One Stop Border Post).  Wakati tunasubiri kukamilisha ujenzi huo, tumekubaliana tuwe na jengo la muda la kurahisisha taratibu za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo katika mpaka wetu na Zambia. 

Vilevile, tulizungumzia njia za kuimarisha na kuboresha taratibu za forodha kwa mizigo itokayo bandari ya Dar es Salaam kwenda Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Zambia.  Tumekubaliana kuwa, Mamlaka ya Kodi ya Mapato ya Zambia iangalie uwezekano wa kuwaweka maafisa wake katika Bandari ya Dar es Salaam kama inavyofanyika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Hii itarahisisha taratibu za forodha kwa bidhaa za Zambia katika bandari yetu.  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshaanza mchakato wa kupata fursa hiyo.  Kwa jumla, ziara ilikuwa ni yenye mafanikio makubwa.
Rambirambi
Ndugu Wananchi;
          Wakati tulipokuwa tunajiandaa kurekodi hotuba hii tukapata habari ya huzuni na majonzi makubwa ya kifo cha Mbunge wa Mbinga Magharibi, Mheshimiwa Capt. John Damian Komba.  Kifo chake kimeliondolea taifa letu mmoja wa viongozi wake wazuri, msanii mahiri, raia mwema na mzalendo wa kweli.  Marehemu alitumia muda mwingi wa maisha yake kuelimisha jamii kuhusu mambo mema, amefanya hivyo akiwa mwalimu na baadaye Kiongozi wa Kikundi cha Sanaa cha JWTZ na hapa mwishoni kiongozi wa kikundi cha Tanzania One Theatre cha Chama Cha Mapinduzi.  Kwa kutumia kipaji alichojaaliwa na Mola wake ametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa Chama Tawala.  Daima tutamkumbuka kwa mambo mengi mema aliyoifanyia jamii ya nchi yetu na taifa kwa jumla.
 
Ndugu Wananchi;
          Katika salamu zangu za rambirambi kwa Spika wa Bunge na Katibu Mkuu wa CCM niliwaomba kupitia kwao salamu ziwafikie Wabunge wote na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi.  Hali kadhalika, niliomba kupitia kwao salamu ziwafikie familia ya marehemu Capt. John Komba.  Kwa familia ya ndugu yetu mpendwa, napenda  kuwahakikishia kuwa tuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo.  Tunawaombea kwa Mola awape moyo wa subira na uvumilivu.  Wananchi wa Wilaya ya Nyasa tunawapa pole nyingi kwa msiba mkubwa uliowakuta na pengo kubwa mlilolipata.  Nawaomba watambue kuwa namna bora zaidi ya kumlilia Mbunge wao aliyewapenda ni kudumisha mema yote aliyofanya na kukamilisha zile kazi ambazo alikusudia kuzifanya lakini hakuweza kufanya hivyo kwa sababu ya kukutwa na umauti.

          Mwisho nawaomba, Watanzania wote tuungane na familia yake kumwombea marehemu Capt. John Damian Komba mapumziko mema.  Amin.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibari ki Tanzania!

Asanteni kwa kunisikiliza.

0 Responses to “HOTUBA YA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI, 2015, YAMHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, ILIYOTOLEWA TAREHE1 MACHI, 2015.”

Post a Comment

More to Read