Thursday, March 5, 2015
RAIS JAKAYA KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBILAMBI KWA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA KUFUATIA NA VIFO VYA WATU 38 WALIPOTEZA MAISHA KWA MVUA KUBWA. Mvua Kubwa
Do you like this story?
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Ali Nasoro Rufunga kuomboleza vifo vya
watu 38 huku wengine 82 wakijeruhiwa usiku wa kuamkia tarehe 4 Machi, 2015.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea
katika Kata ya Mwakata iliyoko katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga
kufuatia mvua kubwa ya mawe iliyonyesha ikiambatana na upepo mkali, hivyo
kuathiri watu 3,500. katika Kata Mwakata iliyoathiriwa zaidi, kaya 350
zimeathiriwa katika Kijiji cha Makata wakati katika Kijiji cha Ngumbi, kaya 100
zimeathirika. Katika Kijiji cha Magung’hwa, kaya 50 zimeathiriwa..
“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko
makubwa taarifa za vifo vya watu 38 waliopoteza maisha na wengine 82
waliojeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu
baada ya nyumba zao kusombwa kabisa na maji kutokana na mvua kubwa ya mawe
iliyoambatana na upepo mkali kunyesha”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba
huo.
Rais Kikwete amesema msiba huo siyo wa
Wana-Shinyanga pekee bali ni wa Taifa zima ambalo limepoteza nguvukazi muhimu
kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii ya Watanzania kwa ujumla.
“Naomba upokee Salamu zangu za Rambirambi
kutoka dhati
ya moyo wangu kwa kupotelewa ghafla na wananchi 38 kwa mara moja katika Mkoa
wako. Kupitia kwako naomba Rambirambi zangu na Pole nyingi ziwafikie
wafiwa wote kwa kuondokewa na wapendwa, ndugu na jamaa zao.
"Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi
wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu wote Mahala Pema Peponi,
Amina”, amezidi
kuomboleza Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais Kikwete amewaomba wafiwa wote wawe
na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao wanapoomboleza
vifo vya ndugu na jamaa zao, lakini amewataka wasisahau ukweli kwamba kazi ya
Mungu haina makosa. Aidha amewahakikishia wafiwa wote kuwa binafsi yuko
pamoja nao katika kipindi chote cha kuomboleza msiba huu mkubwa kwao na kwa
Taifa.
“Namwomba Mola awawezeshe majeruhi wote
wa tukio hilo wapone haraka ili waweze kuungana tena na familia, ndugu na jamaa
zao na kuendelea na maisha yao kama kawaida”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika
Salamu zake za Rambirambi.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Machi, 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS JAKAYA KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBILAMBI KWA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA KUFUATIA NA VIFO VYA WATU 38 WALIPOTEZA MAISHA KWA MVUA KUBWA. Mvua Kubwa ”
Post a Comment