Friday, July 3, 2015

BIASHARA YA KADI ZA KLINIKI KWA WAJAWAZITO YASHAMIRI,ZAUZWA SH 3,000




WAKATI Sera ya Afya nchini ya mwaka 2007, chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inaeleza wazi kwamba kina mama wajawazito wanaohitaji huduma za afya katika taasisi za umma, kwa maana ya Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati, pamoja na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano watapatiwa huduma bure, hali halisi ilivyo ni tofauti kabisa katika taasisi hizo za umma nchini

Uchunguzi wa muda sasa, uliofanywa katika maeneo kadhaa yanayotoa huduma za afya kwa kina mama wajawazito nchini, umebaini kwamba mbali na kina mama hao kutakiwa kuchangia huduma mbalimbali wanazotakiwa kupata kwa mujibu wa sera hiyo ya afya, hata Kadi za Kliniki sasa wanatakiwa wazilipie kwa gharama ya kati ya Sh 2,000 hadi 3,000.
Hali hiyo ya kugeuza maeneo ya kutolea huduma za afya ya jamii kama vitega uchumi kwa baadhi ya watoa huduma wenye tamaa ya kipato na wasiozingatia maadili ya kazi zao pamoja na sera nzima ya afya ya jamii, imetafsiriwa na baadhi ya wadadisi wa mambo nchini kwamba Tanzania kwa sasa inakabiriwa na mazingira hatari ya kuishi kwa mama na mtoto.

Sera ya Afya ya Mama na Mtoto ya mwaka 1990, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007, inaeleza kwamba afya ya mama na mtoto ni mfumo wa utoaji huduma maalumu kwa wanawake walio katika umri wa uzazi na watoto wenye umri chini ya miaka mitano, hasa watoto wachanga tangu kuzaliwa hadi siku 28.

Huduma kwa mama na mtoto zinazotajwa na sera hiyo, zinajumuisha kutambua viashiria au vidokezo hatari kwa wanawake na watoto, chanjo, tiba, elimu ya uzazi, uzazi salama, mbinu shirikishi za udhibiti wa magonjwa ya watoto, afya katika jamii, lishe na afya mashuleni.

Sera hiyo ilitungwa mahsusi na Serikali, kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa lengo la kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga, hasa baada ya kubainika kuwepo kwa vifo vingi vya watoto wachaga ambao idadi yao ilifikia wastani wa vifo 578 mwaka 2005, kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa hai.

Kutokana na hali hiyo, sera hiyo inatamka kwamba Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi zinazotoa huduma bila faida pamoja na mashirika ya kimataifa, itaendelea kutoa huduma bila malipo yoyote kwa wanawake wajawazito, watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Hata hivyo, pamoja na uwepo wa sera hiyo pamoja na msisitizo huo wa Serikali, uchunguzi umebaini kwamba maeneo mengi yanayohusika na utoaji wa huduma hizo za mama wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano, yamegeuzwa kuwa sehemu ya biashara, kwa kina mama hao kutakiwa na baadhi ya wauguzi na wakunga kuchangia huduma hizo kwa malipo yanayoingia mifukoni mwa watoa huduma hao.

Hospitali ya Rufaa ya Mwananyama, katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, imetajwa kuwa miongoni mwa taasisi za umma, ambazo wakunga na wauguzi wake wamekithiri kwa biashara hiyo ya kadi za kliniki kwa kina mama wajawazito, ikielezwa kwamba kina mama wengi wanaofika kwa mara ya kwanza kuanza huduma hiyo wamekuwa watakiwa kutoa Sh 2,000 kama gharama ya kupata kadi hiyo kwa kisingizio cha kuadimika kwa kadi hizo kunakochangiwa na bajeti finyu ya Serikali Kuu.

Mwana mama Jorida Almasi (35), ambaye ni mmoja wa wajawazito waliokumbana na hali hiyo alipokwenda kwa mara ya kwanza kuanza kliniki katika hospitali hiyo, ameithibitisha kudaiwa kiasi cha Sh. 2,000 ili kupata kadi hiyo ya kliniki, ingawa anasema hata baada ya kutoa fedha hizo hakuna stakabadhi yoyote ya Serikali aliyopewa ili kuhalalisha uhalali wa malipo hayo.

Hali kama hiyo ya Mwananyamala ya kugeuza biashara kadi hizo za kliniki kwa mama wajawazito, inadaiwa kukithiri pia katika Zahanati ya Lamba, iliyoko kijiji cha Lamba, Kata ya Mgori, Wilaya ya Singida Vijijini, Mkoa wa Singida.

Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika Zahanati hiyo, aliyejitambulisha kwa jina la Zuena Mrema, amekiri kuwepo kwa tozo mbalimbali kwa mama wajawazito na wenye watoto wa umri wa chini ya miaka mitano, akidai kuwa hali hiyo inatokana na hali halisi ya mazingira magumu yalivyo katika hospitali na vituo vya afya vya umma, hasa katika suala zima la upatikanaji wa fedha kutoka Serikali Kuu ili kuwawezesha kutoa huduma bure kwa mujibu wa sera hiyo.

“Hali halisi ya mazingira magumu ya utoaji huduma kutokana na ufinyu wa bajeti unaozikabili hospitali karibu zote za umma na vituo vya afya, hasa katika utoaji wa huduma ya mama na mtoto, wakati mwingine tunalazimika kuwashauri kina mama wajawazito kuja na vifaa vyao ili kuwaepushia usumbufu na ukosefu wa huduma kwa muda muafaka,” anasema Mratibu huyo wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika Zahanati hiyo.

Malalamiko kama hayo ya kina mama wajawazito wanaokwenda kuanza huduma ya Kliniki kutakiwa kulipia kadi zao, yamepokelewa kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, Mkoa wa Kigoma.

Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Fadhili Suleiman, amekiri kupokea malalamiko hayo kutoka kwa baadhi ya kina mama waliofanyiwa vitendo hivyo, huku akiahidi ofisi yake imepanga kufanya kikao cha wafanyakazi wote wa hospitali ya wilaya hiyo mwanzoni mwa mwezi ujao wa Julai, 2015, ili pamoja na mambo mengine, kujadili namna ya kukomesha tabia hiyo aliyoilezea kama kero kubwa kwa kina mama na watoto wanaostahili kupata huduma zao bure kwa mujibu wa maelekezo ya sera ya afya nchini.

Uchunguzi zaidi wa timu ya waadishi wetu walioko katika maeneo mbalimbali nchini umebaini kuwepo kwa biashara hiyo ya kadi za kliniki pamoja na uchangiaji wa huduma kwa mama wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano katika Hospitali Kuu za Wilaya ya Nachingwea, Lindi, pamoja na Bunda, Butiama na Musoma Mjini katika mkoa wa Mara.

Vyanzo kadhaa vya taarifa hizi kutoka katika maeneo hayo vimethibitisha pasipo na shaka yoyote kwamba katika baadhi ya hospitali hizo, kadi hizo za kliniki zimekuwa zikiuzwa hadi Sh 3,000 kwa mama mjamzito anayezihitaji kutokana na ulazima wake katika kutunza kumbukumbu za mwenendo wa ujauzito wake pamoja na afya yake kwa ujumla.

“Hivi ni lini hasa sisi kina wajawazito hapa nchini tutakuja kupata huduma bora za kliniki bila malipo kama Serikali yetu inavyoagiza kila siku? Ni nani hasa anastahili kuwajibika katika hili, ni hawa watoa huduma wetu katika vituo vya afya au ni uongozi wa Manispaa ya Kinondoni unaopaswa kusimamia utoaji wa huduma za afya kwa jamii katika wilaya hii?” alihoji mwana mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Asia, mkazi wa Mbezi Makabe, jijini Dar es Salaam katika malalamiko yake kuhusiana na suala hilo.

Kumbukumbu kuhusu dhana nzima ya Uzazi Salama au Usio Salama kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini, zinaonyesha kwamba dhana hiyo inahitaji usimamizi wa karibu wa mtoa huduma a afya ya ujauzito kwa mama mjamzito, kuanzia pale inapothibitishwa kuwepo kwa ujauzito hadi wakati wa kijifungua na hata baada ya kipindi cha wiki sita za baada ya kujifungua.

CHANZO:FikraPevu

0 Responses to “ BIASHARA YA KADI ZA KLINIKI KWA WAJAWAZITO YASHAMIRI,ZAUZWA SH 3,000”

Post a Comment

More to Read