Friday, February 6, 2015

JESHI LA POLISI MBEYA LATOA UFAFANUZI JUU YA KUIBUKA KWA VURUGU ZA MBALIZI MBEYA.




Na Mwandishi wetu,Mbeya

POLISI Mkoani Mbeya, imetoa ufafanuzi kufuatia vurugu zilizofanywa na wananchi wa Mji mdogo wa Mbalizi na baadhi ya askari wa jeshi la wananchi kikosi cha 44KJ cha Mbalizi, ambapo vurugu hizo zilisababisha kifo cha askari mmoja.

Aidha imeelezwa kuwa , vurugu hizo hazikusababishwa  na  ugomvi wa kimapenzi kama ulivyoelezwa na kuenezwa na baadhi ya watu bali ni ugomvi ambao uliwahusisha baadhi ya vijana raia na wanajeshi wa kikosi cha Mbalizi 44KJ baada ya mwanajeshi mmoja aliyepanga ulaiyani kuibiwa mali zake.

Akimtaja askari huyo aliyeuawa katika vurugu hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, amesema ni marehemu  mwenye namba FT 1096619 Mwaka Ahadi kutoka kikosi namba 825 cha JKT Mtabila kilichopo Mkoani Kigoma.

Aidha, amesema kuwa askari huyo alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Jeshi ya Mbalizi  kikosi cha 44KJ.

Akielezea sababu za vurugu hizo, Msangi amesema, viashiria vya kutokea kwa vurugu hizo, vilianza kutokea siku ya Jumanne ya tarehe 3 mwezi February, 2015 baada ya kukamatwa kwa vijana nane na kufikishwa katika kituo cha Polisi cha Wilaya ya kipolisi ya Mbalizi kwa tuhuma za wizi wa radio na televisheni.


Amesema, kwa mujibu wa taarifa hizo, inasemekana kwamba katika msako huo vijana nane walikamatwa kati ya tisa na kufikishwa katika kituo cha polisi.

Amesema, hivyo wananchi walipowaona wanajeshi kwenye eneo lao walianzisha vurugu zilizoambatana na uvunjifu wa amani .

Amesema, wakati pande hizo mbili zikitoa maelezo yao ndipo kulipozuka mzozo  mkubwa  hivyo kuibukatena kwa vurugu zilizovuta hisia za watu ambao walifika na kuzua taflani.

Amesema, katika vurugu hizo askari mmoja wa jeshi la wananchi, Ahadi Mwaka aliumizwa kwenye sehemu ya kichwa na katika kidevu hivyo kukimbizwa hospitali ya jeshi ya Mbalizi na kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu hayo.

Amesema, vurugu hizo zilisababisha hali ya amani kutoweka  kwenye eneo hilo, hivyo polisi kulazimika kuongeza nguvu zilizosaidia kuwatuliza wananchi ikiwa na kuwaondoa hofu iliyokuwa ikiwatawala kwamba huenda wanajeshi  wakawavamia na kuwapiga.

Hata hivyo, katika vurugu hizo hakuna raia aliyeumia lakini baadhi ya watu wamelalamika kuharibiwa mali zao  na kwamba uchunguzi unaendelea.
Mwisho.

0 Responses to “JESHI LA POLISI MBEYA LATOA UFAFANUZI JUU YA KUIBUKA KWA VURUGU ZA MBALIZI MBEYA.”

Post a Comment

More to Read