Wednesday, March 4, 2015
WAZIRI MAGUFULI AZUIA BOMOABOMOA MKOANI KILIMANJARO.
Do you like this story?
Waziri wa
Ujenzi Dkt. John Magufuli ametangaza kutobomoa nyumba zilizopo kando kando ya
barabara ya Mwanga-Kikweni/Vuchama-hadi Lomwe km 40.6 na kusema kuwa
barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami kwa kutumia upana wake uliopo sasa
hivi.
Dkt. Magufuli
alitoa kauli hiyo ya faraja kwa wakazi wa Kikweni Wilayani Mwanga Mkoani
Kilimanjaro kabla ya kuweka jiwe la msingi katika barabara ya
Mwanga-Kikweni/Vuchama-Usangi hadi Lomwe(km 40) itakayojengwa kwa kiwango cha
lami hivi karibuni.
Waziri wa
Ujenzi amechukua uamuzi huo kutokana na maeneo mengi ya milimani ambapo
barabara hiyo inapita kuwa na mashamba ya watu tofauti na sehemu nyingine.
“Nikiwa kama Waziri wa ujenzi katika maeneo haya ya milima sitatumia sheria ya
mita 30 kila upande katika ujenzi wa barabara hii ili nyumba na mashamba ya
wakazi wa huku yasiathirike”.
Dkt. Magufuli
aliongeza kuwa ujenzi wa Barabara una sheria zake ndio maana ameamua kutumia
sheria ya barabara namba 13 ya mwaka 2007 kifungu cha 13 na 20 kinachompa
mamlaka kupunguza upana wa barabara.
Aidha, Waziri
Magufuli aliwatoa hofu wakazi wote waliowekewa alama ya X katika nyumba zao na
kuwataka kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwasababu nyumba hizo
hazitabomolewa.
Katika hatua
nyingine Dkt. Magufuli aliwataka watu wote waliojenga vibanda karibu na
barabara ya zamani waanze kuondoka mapema kabla ya ujenzi wa barabara hiyo
kuanza hivi karibuni.
“Nawaomba
wote mlioweka vibanda karibu na barabara mtoe kwa hiari yenu ili tutengeneze
barabara hii bila vikwazo na kwa haraka tofauti na awali ambapo tulikuwa
tunatangaza zabuni kwa kilomita chache” alisisitiza Waziri Magufuli.
Kwa upande wa
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama amemshukuru Waziri Magufuli kwa hatua
yake hiyo na kusema kuwa kufunguka kwa barabara hiyo ni mkombozi mkubwa kwa
wilaya ya Mwanga na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
“Wilaya yetu
hii inapakana na nchi jirani hivyo hata kiusalama ni vizuri barabara hii
ikajengwa kwa lami ili irahisishe mawasiliano kwa haraka zaidi katika Wilaya
yetu hii” alisema Mkuu wa Mkoa.
Naye Mbunge
wa Mwanga ambaye pia ni Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe ameishukuru
Serikali na kusema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutawaondolea kero kubwa
ya usafiri wananchi wa Usangi na mwanga na kuwasaidia kufanya biashara kwa
urahisi zaidi tofauti na awali.
“Kukamilika
kwa barabara hii kutasaidia kuinua uchumi mkubwa uliopo huku Usangi tofauti na
hali iliyopo sasa” Alisema Profesa Maghembe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MAGUFULI AZUIA BOMOABOMOA MKOANI KILIMANJARO.”
Post a Comment