Wednesday, May 27, 2015
FOLENI YA IKULU:MWANDOSYA, MUHONGO KUTANGAZA NIA WIKI IJAYO.
Do you like this story?
Ni dhahiri sasa kuwa hatua ya vikao vya juu
vya CCM kuwafungulia makada wake waliokuwa wamefungiwa kwa kuanza kampeni
mapema na kutangaza tarehe za kuanza kuchukua fomu, vimechochea harakati za
kusaka urais na kuongeza urefu wa foleni ya wanaotaka kuelekea Ikulu kumrithi
Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yamejitokeza ndani ya siku nne baada ya
uamuzi huo wa CCM kutangazwa mjini Dodoma na kuwafanya makada wake, kuanza
kujitokeza hadharani wakiweka bayana tarehe za kutangaza nia hiyo.
WanaCCM waliojitokeza ni mtoto wa Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospeter
Muhongo ambao kwa nyakati tofauti wamethibitisha kuwa wanatangaza nia hiyo wiki
ijayo.(P.T)
Wakati Makongoro akisema sasa anajisikia
kuomba kazi ya urais na anatarajia kutangaza nia hiyo kabla ya Juni 3, Profesa
Muhongo ameahidi kufanya hivyo kati ya Mei 31 na Juni 3, huku Profesa Mwandosya
akisema ataweka wazi kila kitu Jumatatu ijayo. Tarehe ya kuanza kuchukua fomu
kwa chama hicho ni Juni 3 na kurejesha ni Julai 2.
Kuingia ulingoni kwa mada hao ambao kwa muda
mrefu hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, kunaongeza orodha ya makada
waliokwishajipanga kwenye foleni hiyo akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa anayetarajia kutangaza kile anachoita 'safari ya matumaini' Jumamosi
mjini Arusha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
aliyetangaza nia hiyo juzi, akifafanua kuwa atafanya hivyo hivi karibuni huko
Mtama, Lindi alikozaliwa.
Pia wamo, Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Stephen Wasira aliyekwishaeleza nia hiyo, Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba aliyejiuzulu unaibu Katibu Mkuu wa CCM Jumapili ili aweze
kuwania urais bila mgongano wa masilahi katika vikao vya chama hicho, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla,
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Balozi
wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), Amina Salum
Ali.
Katika mlolongo huo wapo makada waliokuwa
wanatajwa muda mrefu ambao wanasubiriwa kuweka bayana ni hiyo ambao ni Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kauli ya Makongoro
Akiwa mjini Mbeya juzi, mbunge huyo wa Afrika
Mashariki alisema: "Najisikia kuomba kazi ya kuwaongoza Watanzania katika
ngazi ya juu ya uongozi, kwani uwezo ninao, afya na muda wa kufanya hivyo
vinaniruhusu."
Makongoro alisema hayo wakati akitoa shukrani
kwa viongozi wa dini baada ya kumkabidhi Tuzo ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
kwa niaba ya familia, ikiwa ni ishara ya kuenzi na kukumbuka kazi alizofanya
Baba wa Taifa enzi za uhai wake.
Awali, viongozi wa dini na machifu
walioshiriki hafla hiyo, walimtaka Makongoro 'kuvunja tetesi' zinazosambazwa
kupitia vyombo vya habari juu yake kuhusu kuwania urais na kumtaka atamke wazi
juzi hilo kwa kuwa wako tayari kumsaidia katika harakati zake.
Kiongozi wa machifu wa Busokelo, Prince
Mwaihojo alisema wananchi wa Mbeya wana imani kubwa na familia ya Mwalimu
Nyerere kwa kuwa mwasisi huyo wa Taifa alikuwa akitangaza mambo mazito akiwa
mkoani hapo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “FOLENI YA IKULU:MWANDOSYA, MUHONGO KUTANGAZA NIA WIKI IJAYO.”
Post a Comment