Wednesday, May 27, 2015
RCC YATOA MAPENDEKEZO YA UGAWAJI MAJIMBO MBEYA
Do you like this story?
Meya wa jiji la mbeya Atanasi
Kapunga akitoa mapendekezo yake katika kikao
|
KIKAO cha kamati ya ushauri cha Mkoa wa Mbeya,(RCC)kimetupilia
mbali mgawanyo wa majimbo manne ya uchaguzi ambayo yalipendekezwa kugawanywa
kwa ajili ya uchaguzi mkuu kwa mwaka 2015 baada ya kukosa sifa na vigezo
vilivyopendekezwa na Tume ya uchaguzi.
Kikao hicho pia, kimependekeza majimbo matatu yaliyomo katika
Wilaya ya Momba, Mbeya na Mbozi kugawanywa kutokana na kukidhi vigezo hususani
idadi ya watu.
Zoezi hilo limefanyika leo jijini Mbeya kupitia kikao cha
dharula cha kamati hiyo, kilichoketi Mkoani hapa na kuhudhuriwa na wajumbe
mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa na wabunge.
Awali, akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi
Kandoro, aliwataka wajumbe kuzingatia vigezo vya ugawaji wa majimbo
wakati wa mapendekezo hayo, huku akisisitiza kigezo kikuu ni wastani wa watu,
upatikanaji wa mawasiliano na ukubwa wa eneo la jimbo.
Wajumbe, hao walikubaliana na mgawanyo wa jimbo la Mbeya vijijini
ambalo linaongozwa na Mchungaji Lacksoni Mwanjale kupitia tiketi ya CCM, jimbo
hilo linagawanywa na kuwa majimbo mawili ya uchaguzi kwa mwaka 2015 ambayo ni
Jimbo la Mbeya na jimbo la Isangati.
Jimbo la Mbeya, litaundwa na Kata 11 za Tembela, Inyala,Itewe,
Njombe,Maendeleo, Igoma, Ilungu, Ihango, Lwanjilo, Ulenje na Swaya na kwamba
ukubwa wa eneo hilo ni kilomita 1,225,425 idadi ya watu ikiwa ni 107,349.
Jimbo la Isangati litakuwa na Kata 15 za Masoko,Ilembo,
Izyira,Iwiji, Isuto,Bonde la Songwe, Iwindi,Igale, Santiliya, Iyunga Mapinduzi,
Itawa, Utengule Usongwe na Nsalala ukubwa wa eneo ni kilomita 1,206.575
na idadi ya watu ni 221,480.
Jimbo la Mbozi Mashariki,linagawanywa na kuwa majimbo mawili ya
uchaguzi ya Vwawa na Mbozi na kwamba kigezo kikuu kilichotumika ni idadi ya
watu, hali ya kijiografia haijakaa vizuri pamoja na ugumu wa mawasiliano
uliopo.
Lingine ni jimbo la Momba,ambalo awali lilikuwa likitambulika
jimbo la Mbozi Magharibi, linagawanywa na kuwa majimbo mawili ya Momba na
Tunduma na kwamba kigezo kikubwa kilichotumika ni baada ya serikali kuupandisha
hadhi mji wa Tunduma na kuwa halmashauri ya mji mdogo.
Majimbo mengine yaliyotupiliwa mbali kugawanywa ni jimbo la
Mbarali, Rungwe, Kyela na Mbeya mjini ambayo yameonekana kukosa sifa
zilizoainishwa na tume ya uchaguzi hivyo kuendelea kubakia kama yalivyo.
Aidha, kikao hicho kimebadilisha majina ya majimbo ya uchaguzi
ambapo jimbo la Rungwe Mashariki limekuwa Jimbo la Busokelo huku jimbo la Mbozi
Magharibi kuwa jimbo la Momba.
Hata hivyo, alisema kuwa mgawanyo huo utawasaidia wabunge watakao
chaguliwa katika kutoa huduma kwa wananchi wa majimbo husika.
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ RCC YATOA MAPENDEKEZO YA UGAWAJI MAJIMBO MBEYA”
Post a Comment