Friday, May 22, 2015

TUHUMA ZA WANAUME ROMBO ZAMFEDHESHA MBUNGE WAO.




MADAI ya wanawake wa wilaya ya Rombo, Kilimanjaro, kukodi wanaume kutoka nchini Kenya, baada ya kukosa huduma za ndoa kutoka kwa waume zao kwa muda mrefu, kutokana na ulevi wa gongo uliopindukia, zimemfadhaisha Mbunge wao, Joseph Selasini (Chadema).

Mbunge huyo amefikia hatua ya kusema kuwa familia yake na wananchi wa huko, wamefadhaika na kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda wenzi wao katika ndoa zao ikiwemo ya mbunge, si waaminifu.

Selasini alisema hayo jana, alipokuwa akiuliza swali kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambapo alisema ingawa hali hiyo imewafadhaisha, lakini alitetea utengenezaji wa pombe za kienyeji, ikiwemo pombe haramu ya gongo.
Katika utetezi huo, Selasini alitaka Serikali iangalie namna ya kusaidia uboreshwaji wa pombe za kienyeji, kwa kuwa kipato chake kimekuwa kikisaidia ada za watoto, kujikimu na kuongeza kipato cha familia.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema kwa namna Selasini anavyozungumza, huenda anatetea suala la kuhalalisha pombe haramu aina ya gongo, na kama ndio hiyo Serikali itaendelea kupiga vita utengenezaji na matumizi ya pombe hiyo kwa sababu viwango vyake havipimiki.

“Mheshimiwa Selasini, kwa maelezo yako utakuwa unazungumzia gongo, sasa hii ni pombe haramu na Serikali inaendelea kuipiga vita kwa kuwa viwango vyake havipimiki.
“Lakini huenda kwa siku zijazo, jambo hili linaweza kuangaliwa na kiwanda cha Konyagi kuhusu namna ya kuiboresha kwa sababu hata Konyagi ni jamii ya gongo, lakini inapimika na haina madhara makubwa kwa watumiaji,” alisema Pinda.

Hata hivyo, katika swali la nyongeza la mbunge huyo, alimtaka Waziri Mkuu kukanusha tuhuma za Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lembrice Kipuyo alizotoa wiki iliyopita akidai kuwa wanawake wa wilaya hiyo, wanakodisha wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kuwahudumia mahitaji ya kimwili, kwa kuwa waume zao wameshindwa kutokana na ulevi uliopindukia.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunaomba kauli ya serikali kuhusu jambo hili, na mkanushe taarifa hizo kwani zimeleta mfadhaiko kwenye familia na hata familia yangu, wanandoa wana wasiwasi kwamba wenza wao wanatoka nje ya ndoa, lakini pia kauli hiyo ni ya kudhalilisha wananchi wa Rombo”, alisema Selasini.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema hajasikia tuhuma hizo ;na kwamba kama zimetolewa na Mkuu huyo wa Wilaya ni vyema aliyetoa, azikanushe mwenyewe kwa kuwa ndiye anayejua alizitoa katika mazingira gani na wapi.

Aidha, alisema ni vyema apewe muda wa kulifahamu jambo hilo ;na kusema ataiagiza Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuangalia jambo hilo kama Mkuu huyo wa Wilaya alichokisema, sio sahihi ili hatua nyingine zifuate.

0 Responses to “TUHUMA ZA WANAUME ROMBO ZAMFEDHESHA MBUNGE WAO.”

Post a Comment

More to Read