Thursday, May 21, 2015
MMOJA AFARIKI DUNIA WAKATI AKIWA KWENYE FOLENI YA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGAKURA
Do you like this story?
Mtu mmoja amefariki
dunia baada ya kuanguka ghafla akiwa kwenye foleni ya kwenda kujiandikisha
kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa teknolojia mpya yaBiometric
Voters Registration (BVR).
Tukio hilo la
kusikitisha lilitokea juzi saa 6:30 mchana kwenye kituo cha Lusyoto, kata ya
Mpuguso katika eneo la Ushirika, wilayani Rungwe, ikiwa ni siku ya kwanza ya
kuanza uandikishaji wa wapigakura wilayani humo.
Baadhi ya wananchi
walioshuhudia tukio hilo wamemtaja aliyepoteza maisha kwenye tukio hilo kuwa
ni Mary Kabejela anayekadiriwa
kuwa na umri wa miaka 60, mkazi wa Ushirika wilayani Rungwe.
Wakizungumzia tukio
hilo, baadhi ya mashuhuda walisema Mary akiwa kwenye mstari wa foleni ya
kuelekea kwenye chumba cha uandikishaji, ghafla alionyesha kudhoofika na
kuishiwa nguvu na kisha kudondoka chini.
Amani Mwaipaya, mmoja
wa mashuhuda wa tukio hilo alisema baada ya mama huyo kuanguka, wananchi
walimwinua na kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya Makandana, ambako
alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu.
“Tulimwona
akianza kulegea na ghafla akaanguka chini, ndipo tulipomwinua na kumpakia
kwenye gari tukampeleka hospitali, lakini wakati daktari akianza kumhudumia
alifariki dunia,” Mwaipaya.
Baadhi ya wananchi na
viongozi wa kisiasa waliozungumzia tukio hilo, walisema kifo cha mama huyo
huwenda pia kimechangiwa na kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu kutokana na
kasi ndogo ya uandikishaji.
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mbeya, Ahamed Msangi, hakupatikana
kuthibitisha tukio hilo licha ya simu yake ya mkononi kuita kwa muda mrefu.
Mwandishi wa habari
hizi alifika kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na kuelezwa kuwa
Kamanda Msangi amesafiri kikazi na kwamba kaimu wake, Nyigesa Wankyo pia
alikuwa nje ya ofisi kikazi.
Mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mbeya Mjini,David
Mwambigija,
maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, ambaye yupo wilayani Rungwe kama wakala wa
chama chake kwenye kazi hiyo, alisema uandikishaji unafanyika kwa kasi ndogo,
hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu na hata
kusababisha presha kuwapanda.
“Inawezekana huyu
mama akawa amekufa kutokana na presha kupanda, kwani alisimama kwenye foleni
tangu asubuhi huku akipigwa na jua kali, kutokana na umri wake kuwa mkubwa
huenda presha ilimpanda na kumpelekea kupoteza maisha,” alisema Mwambigija.
Alisema kasi ya
uandikishaji siyo nzuri kutokana na watumishi wa serikali waliopewa kazi hiyo
kuonekana kama wanajifunza hivyo kutumia muda mrefu kukamilisha kumwandikisha
mtu mmoja, hali inayosababisha watu kusimama kwenye foleni kwa muda mrefu.
Mbali na tukio hilo
la kifo, zoezi la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la
Wapigakura lilianza juzi kwa kusuasua wilayani Rungwe kutokana na madai kwamba
mtandao ulikuwa na matatizo.
Kufuatia mtandao kuwa
siyo mzuri, idadi kubwa ya vituo vya kuandikishia wapigakura vilichelewa kuanza
uandikishaji hadi saa 4:00 asubuhi hali ilipoanza kutengemaa.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Veronica Kessy, alikiri kuwapo kwa changamoto
katika siku ya kwanza ya uandikishaji, ikiwamo tatizo la mtandao kusumbua.
Alisema hata hivyo
tatizo hilo lilikuwa la muda mfupi na baadaye hali ilikuwa nzuri na kasi ya
uandikishaji ikaendelea vizuri kama lilivyopangwa katika maeneo mengi.
Kessy alisema ni
vituo vichache tu ambavyo zoezi la uandikishwaji wapigakura liliingia dosari
kwa kukumbwa na changamoto ndogondogo kama vile kuchelewa kufunguliwa,
kujitokeza kwa idadi kubwa ya wananchi kuliko uwezo wa waandikishaji na tatizo
la mtandao kusuasua.
Katika Halmashauri ya
Jiji la Mbeya zoezi la uandikishwaji lilianza juzi katika kata 10 zilizopo
ndani ya Bonde la Uyole, ambako liliendelea vizuri licha ya wananchi
kulalamikia kasi ndogo ya waandikishaji.
Katika kituo cha Isyesye
kulitaka kutokea tafrani baada ya wananchi kumshtukia mtu mmoja anayedaiwa kuwa
kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukaa pembeni mwa kituo cha kuandikishia
wapiga kura akiwa na daftari na kalamu akiorodhesha watu wanaojiandikisha.
Wananchi hao walimjia
juu mtu huyo wakitaka kumpiga kabla ya askari wa Jeshi la Polisi kuingilia kati
na kumwondoa kwenye eneo hilo kabla hajaanza kushushiwa kipigo.
Awamu ya tatu ya
uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ilianza jana mkoani Dodoma
na Tabora utaanza leo, huku Katavi ukiwa umeanza tangu Jumatatu iliyopita.
Awamu ya kwanza
ilihusisha mkoa wa Njombe ambayo ulikamilika katikati ya Aprili, wakati awamu
ya pili inaendelea katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Lindi na Mtwara.
Uandikishaji huo
umekuwa ukilalamikiwa kusuasua kutokana na kasoro kadhaa hususani uchache wa
vifaa (BVR kit), uchache wa waandikishaji na vifaa hivyo mara nyingi
kukwama kufanya kazi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MMOJA AFARIKI DUNIA WAKATI AKIWA KWENYE FOLENI YA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGAKURA ”
Post a Comment