Wednesday, May 20, 2015
RIPOTI YA CAG YAANIKA MADUDU.
Do you like this story?
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad |
RIPOTI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, imetolewa na kuwasilishwa bungeni jana
huku ikiendelea kuibua madudu katika matumizi ya fedha.
Moja ya madudu hayo yamebainika katika
usimamizi wa rasilimali watu katika balozi za Tanzania, ambapo watumishi
waliokoma kutumikia Taifa, wameendelea kugharimiwa katika maisha yao katika
nchi hizo.
Moja ya gharama iliyotajwa na Profesa Assad
wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge ni Sh milioni
543 zilizotumika kulipa posho ya pango kwa watumishi hao baada ya kustaafu.
Katika Ripoti ya Ukaguzi ya Serikali Kuu,
Profesa Assad alikwenda ndani zaidi na kutaja orodha ya balozi hizo ambazo
watumishi wake wameendelea kulipwa ingawa wamestaafu, kwa madai kuwa hakukuwa
na fedha za kugharimia urudishwaji wao nyumbani.
"Maofisa hawa wastaafu, walibakia
wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kwa kuwa Serikali ilikuwa na uhaba wa
fedha, kwa ajili ya kulipia gharama ya kuwarudisha nyumbani baada ya kufikia
umri wa kustaafu," ameeleza Profesa Assad katika ripoti yake.
*Balozi zenyewe
Ubalozi wa kwanza kuwa na maofisa wa aina
hiyo ni wa Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo
mtumishi alistaafu tangu Machi 28, 2014 na akalipwa posho ya Sh milioni 130.8,
kutokana na kufanya kazi kwa miezi 10 zaidi.
Katika ubalozi huo huo, Profesa Assad alisema
mtumishi huyo huyo alipewa Sh milioni 41.2 ya kodi ya pango kwa miezi kumi
aliyofanya kazi akiwa amestaafu na hana mkataba na Serikali.
Ubalozi mwingine ni wa Maputo nchini
Msumbiji, ambapo mtu alilipwa posho ya kufanya kazi akiwa amestaafu ya Sh
milioni 204 kwa miezi 19 zaidi baada ya kustaafu.
"Kiwango hiki cha posho ni sawa na mara
tatu ya gharama ya kumsafirisha yeye, mizigo na familia yake," ameeleza
Profesa Assad katika taarifa hiyo.
Katika Ubalozi wa Ottawa nchini Canada,
Profesa Assad alibainisha wazi kuwa ndiko angalau kulikokuwa na mstaafu ambaye
alipewa mkataba wa miaka miwili, ingawa hakukuwa na maelezo ya sababu ya
kuongezewa mkataba.
Mstaafu huyo wa Canada yeye alilipwa Sh
milioni 137.5, huku katika Ubalozi wa Washington Marekani, mtumishi aliyefanya
kazi ya miezi mitatu tu zaidi baada ya kustaafu, akiibuka na kitita cha Sh
milioni 30.
Vyama vya siasa Wakati wanasiasa wakiwa
vinara wa kushutumu watumishi wa Serikali na hata viongozi wengine kwa matumizi
mabaya ya fedha za Serikali, Profesa Assad amebainisha kuwa vyama vinavyoongoza
kwa kupokea ruzuku kubwa kutoka serikalini, baada ya ukaguzi vimepata hati
yenye mashaka.
Vyama hivyo ni CCM, Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi huku chama kimojawapo kilichojiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) cha NLD, kikiwa miongoni mwa vyama sita vilivyopata hati mbaya.
Akielezea sababu ya kutoa hati hizo kwa vyama
hivyo, Profesa Assad alisema alibaini kuwa taarifa ya hesabu za vyama hivyo,
zinatofautiana na misingi ya uhasibu na mfumo wa uandaaji wa taarifa za fedha.
Vyama vingine maarufu ambavyo hata
havikupeleka taarifa zao za fedha kwa ajili ya kukaguliwa na CAG, ni pamoja na
UDP na DP, huku chama cha ADC kinachotarajia kusimamisha mgombea urais
Zanzibar, kikipata hati mbaya.
"Nashauri Msajili ya Vyama vya Siasa kwa
kushirikiana na Mhasibu Mkuu wa Serikali, kuandaa mwongozo mzuri wa namna ya
kuandaa taarifa za hesabu. Hii itawezesha kutoa taarifa za fedha kwa ubora unaotarajiwa,"
alieleza Profesa Assad.
Watumishi hewa Profesa Assad ameendelea
kubainisha kuwa ndani ya Serikali kumeendelea kutolewa mishahara hewa,
inayolipwa kwa watumishi waliostaafu, walioacha kazi na waliofukuzwa kazi.
"Nimebaini kuwepo kwa malipo ya shilingi
milioni 141 katika taasisi saba...ambao hawakugundulika na kuondolewa katika
orodha ya mishahara kwa wakati baada ya muda wao wa utumishi kufikia ukomo
kinyume cha Sheria ya Umma kwa Wastaafu," amesema.
Malipo hayo yalikutwa katika Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii Sh milioni 74, Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga Sh milioni
24, Ofisi ya Waziri Mkuu Sh milioni 13 na Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro Sh
milioni 10.
Mishahara mingine hewa imekutwa katika
Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga Sh milioni 10, Idara ya Huduma za Uhamiaji Sh
milioni 6 na Wizara ya Mambo ya Ndani Sh milioni 1.9.CHANZO:HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RIPOTI YA CAG YAANIKA MADUDU.”
Post a Comment