Thursday, May 21, 2015

UNESCO YAAHIDI KUSAIDIA TANZANIA KUKABILI DHULUMA DHIDI YA WANAOISHI NA ALBINISM.


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo akiendelea na maongezi na ugeni huo ofisini kwake jijini Mwanza.



Kiongozi wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues (kulia), akielezea nia ya Shirika lake kusaidia mapambano dhidi ya unyanyasaji na dhuluma zinazofanywa jamii dhidi ya watu wenye albinism nchini alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo ofisini kwake jijini Mwanza.

SHIRIKA la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limeahidi kusaidia mapambano dhidi ya unyanyasaji na dhuluma zinazofanywa jamii dhidi ya watu wenye albinism.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kiongozi wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues wakati akizungumza na mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo.

Mwakilishi huyo wa Unesco amesema hayo alipomtembelea Mkuu wa mkoa kumsalimia na kumweleza hatua zinazochukuliwana Unesco katika kukabiliana na ukatili dhidi ya watu wenye albinism.

Akifafanua zaidi alisema kwamba UNESCO haijatenga fedha zitakazotumika kuendesha kampeni mahsusi bali itatumia uwezo wa kiufundi uliopo kwa wataalamu walionao na kwamba wanakusudia kuona kwamba miaka 15 ijayo watoto wanaozaliwa nchini Tanzania wanakuwa huru pasipo na viashiria vya kuhatarisha maisha vinavyosababishwa na mauaji ya watu wenye albinism.

Akimkaribisha Bi Zulmira ofisini kwake, Mkuu wa mkoa Magesa Mulongo alisema kwamba ingawa kuna utulivu katika kipindi hiki mkoani Mwanza, bado mkoa wake unaendelea kukabiliana na viashiria vinavyosababisha ukatili kwa watu wenye albinism na wazee.

Bwana Magesa alisema imani potofu zilizopo zinazosadikika kufanikisha biashara za uvuvi wa samaki, uchimbaji wa madini na wanasiasa kuendelea na madaraka ni miongoni mwa sababu kubwa za mauaji hayo yaliyoitia doa jeusi jamii ya kitanzania nje ya mipaka.

Alisema kwamba jitihada zinafanywa kukabiliana na imani hizo potofu kwa kuihamasisha jamii kutoziamini na kwamba madaraka na utajiri unatokana na juhudi, kufanya kazi kwa bidii na si vinginevyo.

Aidha amesema mkoa wake umekuwa ukihakikisha kwamba makundi yanayotumika kuua watu wengine kwa kushirikisha jamii yanavunjwa na pia kuwachukulia hatua kali wote wanaobainika kushiriki kwa njia moja au nyingine.

Hata hivyo mwakilishi wa umoja wa mataifa alisema kwamba hali ya amani itatawala pale tu watu watakapobaini kwamba kuua ni ukiukwaji wa haki za binadamu na ni kosa la jinai.

Alisema pindi binadamu watakapokiri kwamba binadamu wote ni sawa na kuishi na albinism sio 'mzimu' watabadili mwelekeo mzima wa fikra potofu kimaisha na kuishi kwa amani na kuthaminiana.

Bi Zulmira alimwambia mkuu wa mkoa kwamba UNESCO kwa kushirikiana na wadau wengine wataendesha makongamano yenye lengo la kushirikisha jamii katika kuandaa na kutekeleza mikakati itakayo changia kuzuia na kutokomeza unyanyasaji na dhuluma zinazofanya dhidi ya watu wenye albinism


0 Responses to “UNESCO YAAHIDI KUSAIDIA TANZANIA KUKABILI DHULUMA DHIDI YA WANAOISHI NA ALBINISM.”

Post a Comment

More to Read