Tuesday, June 16, 2015

MBATIA AIBOMOA BAJETI 2015/2016,ASEMA NI BAJETI LIPUA LIPUA


Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, James Mbatia
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, James Mbatia


KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia kwa Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, James Mbatia, imesoma bajeti mbadala wa ile iliyowasilishwa na Serikali, huku ikiainisha masuala kadhaa ya kukuza uchumi na kupunguza utegemezi...Anaandika Mwandishi Wetu ... (endelea).

Kwa mujibu wa Mbatia aliye Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, katika kipindi cha miezi minne ijayo kuanzia sasa, Serikali ya CCM ianze kujiandaa kisaikolojia kuondoka madarakani na kupiisha kwa amani serikali adilifu itakayoongozwa na UKAWA kuingia madarakani ili waweze kuwatumikia Watanzania.

Akiwasilisha maoni ya upinzani leo kwa Bajeti ya 2015/16, Mbatia amesema “tunapendekeza kukusanya Sh. bilioni 19,695.2 ambapo mapato ya kodi na yasiyo ya kodi Sh. bilioni 18,847.1 (sawa na asilimia 20) ya Pato la Taifa.”(P.T)
Aidha, mapato ya halmashauri ni asilimia 0.9 ya pato la Taifa sawa na Sh. bilioni 848.1.

Amesema hiyo ni bajeti isiyo na mikopo ya kibiashara, hivyo inalenga kulipunguzia taifa mzigo wa madeni, tofauti na ile ya serikali yenye mikopo ya masharti ya kibiashara ya 10% na hivyo kuwaongezea wananchi mzigo wa madeni.

“Bajeti inayoendelea kusisitiza umuhimu wa kuwalipa pensheni wazee wote nchini wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wakati ile ya serikali iko kimya kabisa kuhusu malipo ya pensheni kwa wazee wote nchini, kwani bado inaendelea kufanya upembuzi yakinifu usioisha,”amesema.

Mbatia ameongeza kuwa bajeti yao inaendelea kusisitiza kushusha kiwango cha tozo ya kodi ya mapato ya ajira kwa wafanyakazi (PAYE) hadi kufikia asilimia 9 badala ya 11 ya serikali inayokandamiza wafanyakazi.

Kuhusu vyanzo vipya vya mapato ya ndani, upinzani umeainisha na hivyo kuonesha kuwa ni nchi inayojitegemea kwa asilimia 89.5 wakati ya serikali ni tegemezi kwa asilimia 10.32 kutokana na kukopa kwa kiwango kikubwa na hivyo kuongeza deni la taifa.

Mapato ya ndani ya kodi na yasiyo ya kodi, Mbatia anasema yatakuwa asilimia 20 ya pato la Taifa kinyume na serikali yenye mapato ya ndani ya kodi na yasiyo ya kodi asilimia 14.3 ya pato la Taifa.

“Bajeti yetu inalenga kupunguza misamaha ya Kodi hadi kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa ili kuongeza mapato ya ndani wakati serikali imetaja tu azma ya kupunguza misamaha ya kodi bila kufafanua kwa undani.

“Tunalenga kutekeleza kikamilifu miradi ya maendeleo kwa kutenga asilimia 27.34 ya bajeti yote kugharamia miradi ya maendeleo. Bila kukopa katika mabenki ya ndani wakati asilimia 26.31 ya bajeti ya serikali ni matumizi ya maendeleo. Hii ni pamoja na kukopa kibiashara katika mabenki ya ndani,” amesema.

Mbatia ameongeza kuwa, bajeti yao inalenga kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo ambavyo havimuumizi mwananchi wa kawaida tofauti na serikali inayolenga kukusanya mapato kutoka katika bidhaa zinazotumiwa kila siku na wananchi hivyo kuongeza ugumu wa maisha.

Anasema “matumizi ya kawaida yatakuwa ni asilimia 72.66 ya bajeti yote baada ya kutenga fedha za wazee na kuongeza mishahara kwa 10% huku ile ya serikali matumizi ya kawaida ni 73.69.”

Kwa mujibu wa Mbatia, bajti yao ni ya kumsaidia mwananchi wa kawaida kutoka katika wimbi la umaskini, tofauti na ile ya serikali ya CCM aliyosema haimtambui mwananchi maskini na kuongeza matumizi makubwa kwa watawala.

Kuhusu ongezeko la bei ya mafuta, Mbatia amesema, “ni suala mtambuka litakasababisha mfumuko mkubwa wa bei na hatimaye kuongeza uchungu na ugumu wa maisha ya Mtanzania kwa sababu bei za usafiri na bidhaa za mazao zinazosafirishwa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine pia zitapanda
Habari hii imeandaliwa kwa hisani ya Mwanahalisi oline

0 Responses to “MBATIA AIBOMOA BAJETI 2015/2016,ASEMA NI BAJETI LIPUA LIPUA”

Post a Comment

More to Read