Monday, September 21, 2015
MABASI YOTE YA PRINCES MURO YAFUNGIWA NA SERIKALI.
Do you like this story?
MAMLAKA
ya Kudhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imesitisha kwa muda
usiojulikana leseni ya usafirishaji abiria ya kampuni ya mabasi ya Muro (Muro
Investment Co. Limited), kwa kutokidhi viwango vya kiufundi na usalama.
Aidha,
Sumatra imeiagiza kampuni hiyo kuwasilisha kwa mamlaka hiyo mpango wa
utengenezaji magari yake, nakala ya cheti cha ofisa usafirishaji wa kampuni
pamoja na mkataba wake wa ajira, iweze kujiridhisha endapo matakwa ya kanuni za
ufundi, ubora na usalama yamezingatiwa na kutimizwa.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Gilliard Ngewe, kampuni hiyo
ilijulishwa kuhusu uamuzi huo ambao utekelezaji wake unaanza leo kwa mabasi
yote ya Muro yanayosafirisha abiria kutoka Dar es Salaam- Arusha na Dar es
Salaam- Mwanza.
Kufuatia
maelezo ya Ngewe, mabasi hayo yamekuwa yakilalamikiwa na abiria kwa kuharibika
mara kwa mara pindi yawapo safarini, hivyo kushindwa kutoa huduma ya usafiri
kwa viwango vinavyotakiwa.
Alisema,
“Inapotokea mabasi yanayosafirisha abiria yanapata hitilafu za mara kwa mara na
kushindwa kuwapa abiria mabasi mbadala wakamilishe safari zao, mamlaka
inawajibika kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na
kusitisha leseni ya usafiri kwa kampuni husika”.
Mkurugenzi
Mkuu huyo alisema, hatua iliyochukuliwa dhidi ya kampuni ya Muro ilizingatia
ushahidi uliotolewa na abiria waliofikisha malalamiko yao kwa mamlaka hiyo,
wakiwemo walioachwa wakihangaika njiani Septemba 17, mwaka huu, kwa zaidi ya
saa 15 bila kupatiwa suluhisho wala huduma za kibinadamu.
Inaelezwa
abiria hao walikuwa wakisafiri kwa basi la Muro lenye namba za usaji T51BQP,
kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, lililoharibika katika eneo la Chalinze
mkoani Pwani saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:30 usiku, bila wahusika kuwaeleza
abiria chochote.
Mamlaka
hiyo pia ilieleza kuwa, abiria wa mabasi hayo yaendayo Mwanza yakitokea Dar es
Salaam wamekuwa wakikutwa na kadhia ya aina hiyo wawapo safarini, ambapo mara
kwa mara wamejikuta wakihangaika njiani pindi yanapoharibika bila kupatiwa
ufumbuzi wa haraka.
Ngewe
alitaja mabasi mengine ambayo yanahusika na adhabu hiyo kuwa ni lenye namba za
usajili T780BPY lililoharibika Septemba 5, mwaka huu katika eneo la Ruvu
Darajani mkoani Pwani na T788BPY lililoharibika Septemba 11, mwaka huu katika
eneo la Mailimoja-Kibaha mkoani humo.
Mabasi
mengine yaliyofungiwa ni yenye namba za usajili; T 881 BUR, T 485 BQV, T 536
CYC, T 540 CYC, T 534 CYC, T 531 CYC. “Makosa yaliyofanywa na kampuni ya Muro
ni ukiukwaji wa kanuni namba 21 na 22 ya Kanuni za Leseni za usafirishaji kwa
magari ya abiria ya mwaka 2007 na Kanuni namba 11 ya (1)(b) ya viwango vya
ubora na usalama vya mwaka 2008,” alisema.
Sumatra
ilieleza kuwa kufunguliwa kwa leseni kwa kampuni hiyo kutategemea majibu
yatakayotolewa na mkaguzi wa magari kutoka jeshi la Polisi, baada ya
matengenezo yatakayofanywa katika magari hayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “MABASI YOTE YA PRINCES MURO YAFUNGIWA NA SERIKALI.”
Post a Comment