Tuesday, September 22, 2015
TUSIRUHUSU AMANI IVURUGWE NCHINI
Do you like this story?
TUPO kwenye kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu
Oktoba 25, mwaka huu, tumuombe Mungu siku hiyo ikifika tupige kura kwa amani na
kupata viongozi wetu kwa njia ya haki.
Nianze kwa kusema kila mtu mzalendo wa nchi
hii anaombea uchaguzi huo uwe wa haki na amani itawale kwa sababu baada ya
kupiga kura, kuna maisha yatakayoendelea kwa kila Mtanzania na hata kwa raia wa
nje aliyeko nchini.
Kabla ya kampeni kulikuwa na makongamano
ambapo hata Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kiliwahi kuandaa kongamano la
siku mbili lililokuwa na lengo la kutafakari amani ya taifa ambalo
liliwashirikisha viongozi mbalimbali waandamizi wa vyama vya siasa na serikali
wakiwemo mawaziri.Kongamano hilo lilikuwa zuri na nimelikumbuka kwa sababu hivi
sasa kuna viashiria vingi vya uvunjivu wa amani nchini.
Kumekuwepo kiwango kidogo cha uvumilivu wa
kisiasa na dini miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa na dini na kumekuwa na
waandishi wa habari wanaopuuza maadili na kuandika na kutangaza habari za
uongo, uchochezi na uchonganishi ambao unafanywa pia na mitandao ya kijamii.
Unayefanya hivyo unajua kwamba unataka kuingiza nchi katika janga zito?
Tanzania imepata fursa ya kuwa kisiwa cha
amani kiasi cha kutolewa mifano duniani hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuienzi
na kuilinda kwani historia inaonesha nchi nyingi zilizopoteza amani hadi sasa
zinaishi kwenye machafuko.
Amani ni tunu ambayo nchi nyingi zinaililia,
sisi
tumebahatika kuwa nayo tusiichezee wala kuwaruhusu watu wengine waichezee,
ikishatoweka huwa hairudi.Nawahimiza Watanzania kuendelea kupendana, kwani nchi
ambazo amani imetoweka zimekuwa na vilio kila kukicha na uchumi wao kudidimia
kwa kuwa wanakosa muda wa kushiriki shughuli za kuzalisha mali.
Amani tuiimarishe kwani nchi inapokosa amani
wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto, ambao wanakosa huduma muhimu kama
maji, dawa na wanawake ni wadau wakubwa wa amani na wanatakiwa wakishawagundua
viongozi wenye viashiria vya uvunjivu wa amani wawaadhibu kwa kuwanyima kura.
Vyama vya siasa vinatakiwa kuwa na mfumo wa
kuwashirikisha wanawake kulinda na kudumisha amani ya taifa, mchango wa
wanawake katika malezi ya familia, uongozi na uzalishaji mali ni mkubwa sana
una umuhimu wa kipekee katika kudumisha amani na kuleta maendeleo ya kisiasa,
kiuchumi na kijamii.
Ni jukumu la wanasiasa kujenga amani na siyo
kuchonganisha kwenye maeneo yote ya nchi na kwamba badala ya kukaa mijini tu
waende hata vijijini, katika kata wawakutanishe viongozi wao na kuwapa elimu
juu ya amani wakati huu wa kampeni za uchaguzi kabla mambo hayajaharibika.
Nashauri hivyo kwa sababu kuna viashiria vya
dhahiri vya uvunjifu wa amani kwa kuwa kuna watu wamekuwa wakiwapiga wenzao,
kuwaumiza na kuwaua kwenye mikutano ya kampeni hivyo nahimiza zifanyike
jitihada za haraka kukomesha tabia hiyo.
Hakika hali kwa sasa siyo shwari kwa upande
wa amani ya nchi na ni jukumu la kila mmoja kuhimiza amani kwa kuwa ikitoweka
hata serikali itashindwa kufanya kazi za kuwaletea maendeleo wananchi ambao nao
watashindwa kufanya shughuli zao mbalimbali.
Wanasiasa waache kutumia lugha za matusi na
kudhalilisha mamlaka zilizopo madarakani au kukashifiana wao kwa wao kwani
kufanya hivyo kunawafanya wafuasi wao kuchukiana. Nchi hii ina historia tukufu
tangu enzi ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia
mbinu za ulaghai, vitisho, uzushi, uongo, rushwa, kebehi na matusi kama mtaji
wao kisiasa kwenye kampeni zao, jamani nawaomba waache kufanya hivyo, kampeni
ziwe za kistaarabu. Tusiruhusu amani ya nchi ivurugike.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “TUSIRUHUSU AMANI IVURUGWE NCHINI”
Post a Comment