Monday, October 12, 2015

BAADA YA MITAMBO YA MTERA KUZIMWA KIDATU NAYO YASHINDWA KUZALISHA UMEME




Baada ya shirika la umeme nchini kuzima mitambo ya kuzalisha umeme katika kituo chake cha Mtera, kituo kingine cha kuzalisha umeme cha Kidatu kinachotegemea maji kutoka Bwawa la Mtera kinatarajiwa kuzima mitambo yake hivi karibuni kutokana na kuishiwa maji kwa ajili ya kuendesha mitambo hiyo.

Meneja wa Tanesco kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu muhandisi Justus Mtolela amesema kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha megawati mia mbili kimepunguza uzalishaji wake hadi kufikia megawati 30 na kwamba hali hiyo inatokana na kukosekana kwa maji ya kuendeshea mitambo ambapo kina cha maji katika bwawa la Kidatu kimeshuka kutoka mita za ujazo 450 hadi kufikia mita 441 huku kiwango cha mwisho kinachoruhusiwa kuzalisha umeme kikiwa ni mita 433.

Kukauka kwa maji katika bwawa la Mtera na Kidatu ni athari inayotokana na kukauka kwa maji ya mto Ruaha mkuu ambao ndiyo tegemeo la bwawa hilo la Mtera linalohudumia pia bwawa la Kidatu kwa pamoja na mto Lukosi na Iyovi ambayo na yenyewe imekauka.

Hivi karibuni baadhi ya wataalamu na wadau wa rasilimali za maji wamekuwa na maoni na mapendekezo kwa serikali juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kunusuru rasilimali hiyo na kuifanya kuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kutazama upya mgawanyo wa maji kwa sekta mbalimbali na pia kusimamia ufanisi katika matumizi yake.

0 Responses to “BAADA YA MITAMBO YA MTERA KUZIMWA KIDATU NAYO YASHINDWA KUZALISHA UMEME”

Post a Comment

More to Read