Monday, October 12, 2015
CCM YATOA MWENENDO WA KAMPENI ZAKE
Do you like this story?
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, January Makamba. |
Tunapenda kuwataarifu wanachama wetu na umma
wa Watanzania kuhusu masuala yafuatayo: Mwenendo
wa Kampeni za CCM Mgombea Urais wa CCM, Dkt. John Pombe
Magufuli, na Mgombea Mwenza, Ndugu Samia Hassan Suluhu, wameendelea kufanya
kampeni katika maeneo mbalimbali nchini.
Hadi jana, tarehe 10.10.2015, Dkt. Magufuli
alikuwa amekwishatembelea Mikoa 22 na Majimbo 203.
Amekwishafanya mikutano
mikubwa rasmi 240 na mikutano 865 ya kusimamishwa na wananchi njiani, hasa
wananchi wa vijijini. Dkt. Magufuli amekuwa akitumia usafiri wa barabarani,
ambapo hadi sasa ametembea kilomita 31,467 kwa barabara kuu, barabara
za mikoa, barabara za wilaya, barabara za mlisho (feeder roads),
na barabara za mijini na vijijini.
Watu wengi wamekuwa wanajitokeza kwenye
mikutano yetu. Lakini la muhimu zaidi ni hamasa na matumaini wanayopata baada
ya kumuona jukwaani na kumsikiliza Dkt. Magufuli.
Wananchi wanapoondoka kwenye
mikutano yetu ya kampeni wanakuwa wamepata fursa ya kumsikia mgombea wetu kwa
kitambo kinachotosheleza, wamemuelewa, wameelewa sera za CCM na wameshawishika
kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi. Tunaingia katika ngwe ya mwisho ya kampeni
zetu. Tangu kampeni zianze hadi sasa, ushindi wa CCM unajidhihirisha.
Hata hivyo, katika kujihakikishia ushindi na
kuongeza kiwango cha ushindi, katika ngwe hii ya mwisho, tumeanza kampeni
nzito. Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahman Kinana, ameanza ziara ya kampeni
katika majimbo 64.
Vilevile, viongozi wengine wa CCM, akiwemo Rais na
Mwenyekiti wa CCM Mstaafu Mzee Benjamin William Mkapa, nao wataanza safari za
kuzunguka nchi nzima kumuongezea kura Dkt. Magufuli na wagombea wetu wa
Ubunge na Udiwani.
Tutatumia helikopta nne kwa ajili ya shughuli
hii. Dkt. Magufuli na Ndugu Suluhu wataendelea kutumia usafiri wa gari
hadi mwisho wa kampeni, isipokuwa pale tu itakapokuwa hakuna budi. Maandalizi
ya Kuleta Mabadiliko ya Haraka na ya Kweli.
Pia, tunapenda kutoa taarifa kwamba, mgombea
wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, ameunda jopo la wanataaluma na wataalamu huru
magwiji wazalendo wa uchumi, biashara, utawala na sheria, kutoka kwenye taasisi
za elimu ya juu, asasi zisizo za kiraia, na sekta binafsi, kwa ajili ya
maandalizi ya kufanya mabadiliko makubwa Serikalini kuanzia siku ya kwanza
atakayokuwa madarakani.
Dkt. Magufuli amelipa jopo hili majukumu
yafuatayo:
1. Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo
Serikali itabana matumizi, ikiwemo manunuzi ya umma, posho za vikao na matumizi
ya magari, ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa;
2. Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo
Serikali itaongeza mapato mara moja bila hatua za kibajeti kuanzia siku ya
kwanza atakapoapishwa;
3. Kuchunguza na kupendekeza maboresho
makubwa katika mfumo wa utendaji na utumishi na ufanisi katika Serikali; 4.
Kupitia kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wa ngazi zote,
wakulima, wafugaji na wavuvi iwapo unaweza kurekebishwa bila kuathiri bajeti ya
Serikali inayotekelezwa sasa.
5. Kupitia sheria zote za nchi na kuorodhesha
Sheria ambazo zinapaswa kubadilishwa haraka ili kuharakisha mabadiliko ya kweli
na ya haraka ambayo ameyaahidi kwa Watanzania;
6. Kupitia na kuorodhesha masuala yote na
kero zote zinazosubiri maamuzi ya Serikali ili atoe maamuzi kuanzia siku
ya kwanza atakapoapishwa.
7. Kupendekeza miundo na idadi ya Wizara na
kutengeneza rasimu za mikataba ya kazi kwa Mawaziri, Makatibu Wakuu na
watendaji wengine wakuu atakaowateua mara baada ya kuapishwa.
8. Kupendekeza njia za haraka za kumaliza
kero za watumishi wa umma,hasa walimu, askari, madaktari na wauguzi, ili aanze
nao kazi wakiwa na ari na morali ya kusukuma mabadiliko ya kweli.
9. Kutengeneza rasimu ya mpango-kazi wa
utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi alizozitoa kwenye kampeni, hasa
upatikanaji wa ajira kwa haraka na umeme wa uhakika;
10. Kupendekeza muundo wa kitaasisi na
utaratibu muafaka wa kutekeleza ahadi ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila
kijiji na mtaa nchini. Dkt. Magufuli ameazimia kuanza kazi mara moja kwa bidii
kubwa na maarifa mapya.
Imetolewa na:- January Makamba Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
11 Oktoba 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “CCM YATOA MWENENDO WA KAMPENI ZAKE”
Post a Comment