Wednesday, October 28, 2015
WALIOSAMBAZA MATOKEO YA URAIS KINYUME CHA SHERIA WAPANDISHWA KIZIMBANI, DAR
Do you like this story?
Vijana waliokamatwa wakiwa katika mahakama hiyo. |
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam leo. |
Askari wa FFU wakiimarisha ulinzi mahakamani hapo. |
Na Dotto Mwaibale
WATU wanane
akiwemo Raia mmoja wa Korea na raia mmoja wa Kenya wamepandishwa kizimbani kwa
kusambaza taarifa za matokeo ya urais katika Mtandao wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi yakiwa na kichwa 'M4C election result management system' bila
kuthibitishwa kwa lengo la kupotosha umma.
Sanjari na
hilo, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), amewasilisha mahakamani hati ya
kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa kile alichadai kuwa ni kwa sababu ya usalama
na kwa maslahi ya Taifa.
Washtakiwa hao
ni Mashinda Mtei (49) mkazi wa Tengeru Arusha, Julius Mwita (40) mwanasiasa na
ni mkazi wa Magomeni, Frederick Fussi (25) IT, mkazi wa Mbezi, Julius Matei
(45) raia wa Kenya, Meshack Mlawa (25) mchungaji na ni mkazi wa Keko, Anisa
Rulanyan (41) Mhandisi, mkazi wa Kawe, Jose Nimi (51) mkazi wa Uingereza na Kim
Hyunwook (42) raia wa Korea.
Wakili wa
Serikali Mkuu Edwin Kakolaki alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Respicius
Mwaijage wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa washtakiwa
wanashtakiwa kwa mashtaka matatu.
Ilidaiwa kuwa
katika shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote, ambapo inadawa kati ya
Oktoba 25 na 26 mwaka huu, wakiwa katika vituo tofauti tofauti ndani ya Jiji la
Dar es Salaam walitoa taarifa za uongo kwenye mitandao wakati wakijua
hazijadhibitishwa.
Kakolaki alidai
washtakiwa hao walisambaza taarifa hizo kwenye mtandao huo na katika mitandao
mingine ya kijamii ambayo ni Facebook na Twitter kutangaza matokeo ya
urais ya mwaka huku kwa lengo la kupotosha umma huku wakijua hayajadhibitishwa
na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika shtaka
la pili linamkabili Matei, Nimi na Hyunwook, ambapo wanashtakiwa kuwa Oktoba 26
mwaka huu wakiwa katika hoteli ya King iliyopo Kinondoni , Dar es Salaam wakiwa
na hati za kusafiria zenye namba A1532119, 930879 na M 27687807 walijiingiza
katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya urais ya uchaguzi wa mwaka
huu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) bila kibali.
Pia, alidai
katika shtaka la tatu lina mkabili Matei peke yake ambaye akiwa raia wa Kenya
mwenye hati ya kusafirilia namba A1532119 akiwa ndani ya Jiji la Dar es
Salaam alijihusisha na biashara katika Saccos ya Wanama bila kibali.
Baada ya
washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo, walikana kuhusika na tuhuma hizo, ambapo
Kakolaki alidai upelelezi bado haujakamilika na pia alidai DPP amewasilisha
hati ya kuzuia dhamana kwa sababu ya usalama na maslahi ya serikali.
Wakili wa
washtakiwa hao Peter Kibatala, alidai kuwa mashtaka yanayowakabili wateja wake
yanadhaminika, kwa hiyo aliiomba mahakama iwapatie dhamana.
Pia, alidai
hati hiyo ya DPP haiko mahakamani hapo kihalali na kuiomba Mahakama itupilie
mbali hati hiyo kwa sababu haina mashiko kisheria.
Kibatala alidai
kuwa hati ya mashtaka iko tofauti na hati ya DPP kutokana na kifungu
kilichokuwepo kuwa si sahihi, kwa hiyo kama ni hivyo hati hizo zote hazifai,
kutokana na mapungufu hayo.
Baada ya
Kibatala kudai hivyo, wakili Kakolaki alidai kuwa hati ya DPP ipo kihalali
mahakamani na anayetakiwa kuthibitisha hilo ni mahakama kwa hiyo waiyachie
mahakama.
Alidai kuhusu
kifungu kilichotumika ni sahihi, akaiomba mahakama itupilie mbali hoja za
Kibatala na washtakiwa wanyimwe dhamana kwa mujibu wa sheria, baada ya DPP
kuwasilisha hati hiyo.
Hakimu Mwijage
alisema uamuzi wa hoja hizo atazitoa Oktoba 30 mwaka huu na washtakiwa aliamuru
warudishwe rumande.
Nje ya mahakama
Washtakiwa hao
waliondoka katika eneo hilo la mahakama wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi
la Polisi ambapo wakiwa ndani ya magari ya polisi walikuwa wakionesha alama za
vidole viwili.
Mwenyekiti wa
Chadema Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sauti, Profesa Mwesiga Baregu na viongozi wengine wa
Chadema walijitokeza mahakamani hapo kufuatilia shauri hilo. (Imeandaliwa
na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WALIOSAMBAZA MATOKEO YA URAIS KINYUME CHA SHERIA WAPANDISHWA KIZIMBANI, DAR”
Post a Comment