Tuesday, November 3, 2015
CCM YAFUTA USHINDI WA MTOTO WA DK ABDALLAH KIGODA
Do you like this story?
Kamati Kuu ya CCM imefuta matokeo ya kura za maoni katika
Jimbo la Handeni, mkoani Tanga ambako Omar Abdallah Kigoda ambaye ni mtoto wa
mbunge wa zamani, marehemu Abdallah Kigoda alikuwa ameshinda.
Akizungumza jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alisema jana kuwa kutokana na kufutwa kwa matokeo hayo, uchaguzi wa kura
maoni katika jimbo hilo unarudiwa leo.
Alifafanua kuwa wagombea 11 waliwania nafasi hiyo lakini
wawili kati yao, Kigoda na Hamis Amad Mnondwa walipata kura zaidi kuwashinda
wenzao.
Mkutano mkuu wa jimbo la Handeni, ulimchangua Omari Kigoda
kwa kura 296 akiwashinda wenzake wawili Hamisi Mnondwa na Athumani Lukoya
waliokuwa wamechujwa kutoka miongoni mwa wanachama 11 walioomba nafasi hiyo.
“Lakini matokeo yanaonyesha hakuna mshindi aliyepata kura za
kuridhisha kuingia katika ushindani na vyama vingine, ndiyo maana Kamati Kuu
imeamua urudiwe,” alisema bila kutaja idadi ya
kura walizopata wagombea hao.
Mchakato huo wa kupata mgombea unafanyika kutokana na kifo
cha aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk Abdallah Kigoda kilichotokea
Oktoba 12, mwaka huu nchini India.
Nape alisema marudio hayo ya kura za maoni yatasimamiwa na
makada watatu wa CCM, Dk Maua Daftari, Dk Emmanuel Nchimbi na Abdallah Bulembo.
Nape alisema Kamati Kuu inaendelea na kikao chake cha siku
moja ambacho kina ajenda ambazo hakutaka kuzitaja. Kamati Kuu imefanya uamuzi
huo huku kukiwa na sintofahamu juu ya chama hicho kuanza ‘utaratibu mpya’ wa
kuwateua watoto wa vigogo wa chama hicho wanaofariki dunia wakiwa wabunge au
wagombea, kuwania nafasi iliyoachwa na wazazi wao.
Mbali na Omary, Goodluck Mtinga, mtoto wa aliyekuwa Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi) Celina Kombani naye amepitishwa na chama hicho
kugombea ubunge katika jimbo la Ulanga.
Utaratibu kama huo ulitumika katika Jimbo la Kalenga mwaka
2014, CCM ilipomsimamisha Godfrey Mgimwa, mtoto wa marehemu Dk William Mgimwa,
kugombea ubunge katika jimbo hilo lililokuwa likishikiliwa na baba yake.
Mwaka 2012, CCM pia ilimteua Sioyi Sumari kugombea ubunge
katika Jimbo la Arumeru Mashariki kuziba nafasi iliyoachwa na baba yake,
marehemu Jeremiah Sumari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ CCM YAFUTA USHINDI WA MTOTO WA DK ABDALLAH KIGODA ”
Post a Comment