Tuesday, January 26, 2016

BOMOABOMOA YANUKIA MBEYA


Meneja wa Tanroads mkoani Mbeya, Paul Lyakurwa




NA SAMWEL NDONI, MBEYA
WAKATI baadhi ya wakazi wa jiji la Dar-es-Salaam wanaoishi Mabondeni, wakionja shubiri ya kubomelewa nyumba zao wakala wa barabara nchini (Tanroads) mkoani Mbeya imewatahadharisha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya barabara kinyume cha sheria kuhama maeneo hayo kabla zoezi hilo kuanza.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Meneja wa Tanroads mkoani Mbeya, Paul Lyakurwa wakati akizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake ambapo alieleza kuwa zoezi hilo litawalenga wananchi waliowekewa alama nyekundu kwenye nyumba zao.

Lyakurwa alisema kuwa kabla ya kufanyika kwa zoezi hilo  Tanroads itaendelea kutoa taarifa kwa wananchi hao kupitia njia ya barua ili kuwakumbusha kuhama maeneo hayo kabla ya kuanza bomoabomoa.

Alisisitiza kuwa waliowekewea alama ya x nyekundu ni wale  ambao wamejenga nyumba zao kwenye mita 22.5 kila upande ya hifadhi ya barabara kabla yakuanza kutumika  sheria ya barabara ya mwaka 2007.

Aliongeza kuwa waliowekewa alama ya x yenye rangi ya kijani ni wale ambao barabara iliwafuata baada ya kuanza kutumika sheria ya mwaka 2007 ambayo inataka mtu asifanye shughuli za kuendeleza ndani ya mita 30, kila upande wa barabara na kwamba hao watalipwa fidia.

“Dhumuni la kuweka alama ya x kwenye nyumba za watu waliondani ya hifadhi ya barabara ni kuwafahamisha kuwa hawatakiwa kuendeleza shughuli zozote za kibinadamu ndani ya eneo hilo, waliowekewa alama za x nyekundu watabomoa nyumba kwa gharama zao bila fidia,”alisema
“Waliowekewa alama ya x ya kijani kwenye nyumba zao kwa matakwa ya sheria ya barabara ya mwaka 2007 na kanuni zake za mwaka 2009, hao wataondolewa serikali itakapohitaji maeneo hayo na watalipwa fidia,”alisema Lyakurwa.

Alisisitiza kuwa lengo la kuweka alama ya x yenye rangi ya kijani ni kuwataka wasiendeleze shughuli za ujenzi ili kuipunguzia serikali gharama za fidia pindi itakapoyahitaji maeneo hayo .

Aidha alisema serikali kupitia Tanroads itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuondoka kwa hiari katika maeneo hayo lengo likiwa kuwapunguzia hasara inayoweza kujitokeza wakati zoezi la bomoabomoa litakapoanza.
Hata hivyo hakuweka wazi ni lini zoezi hilo litaanza isipokuwa aliwatahadharisha wananchi kuwa muda wowote wataanza kupatiwa ‘notisi’ za kuwataka waondoke kupisha hifadhi ya barabara.
MWISHO

0 Responses to “BOMOABOMOA YANUKIA MBEYA”

Post a Comment

More to Read