Wednesday, January 27, 2016

HOFU YA KUENEA KWA KIPINDUPINDU YATANDA KIGOMA




Na Emmanuel Senny, Kigoma
Wananchi  wa Kata ya Machinjioni katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma-Ujiji mkoani Kigoma, wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu kufuatia kaya 15 kupoteza  vyoo vilivyosombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.

Akizungumza Mwenyekiti wa Mtaa wa Ukumbi, Kata ya Machinjioni, Jumanne Baheza, amesema mvua hiyo ilinyesha jana majira ya saa 5:00 asubuhi  na kusababisha kaya mbili kubomoka huku vyoo 15 vikisombwa na mafuriko.

Amesema, kusombwa kwa vyoo hivyo kulisababisha kaya 15 kukosa vyoo huku kukiwa na hofu ya kutanda kwa magonjwa ya mlipuko kwa wakazi wa maeneo hayo kutokana na uchafu wa vyoo kupelekwa kwenye vyanzo vya maji ambayo wakazi wa eneo hilo huyatumia. 

“Sasa kuna uwezekano mkubwa wa wananchi kupata magonjwa mana kila siku hutumia maji yanayotoka kwenye vyanzo vya maji (bondeni) ambako ndiko uchafu wa vyoo ulielekea huko,” amesema Baheza.

Awali katika kikao cha mkoa kilichoketi Novemba 2015 kilichoadhimia  kudhibiti hali ya uchafu katika mkoa huu, Mganga Mkuu wa Kigoma, Leonard Subi ambaye alisema kuwa Kigoma inakabiliwa na ukosefu wa vyoo bora kwa asilimia 25  na vyoo  vingi  vimejaa.

 Aidha takwimu hiyo ya Mganga mkuu inaonyesha kuwa tatizo la ukosefu wa vyoo linaongezeka kutokana na athali za mvua zinazoendelea kunyesha mkoani hapa na kupelekea hofu ya magonjwa ya mlipuko.

Hata hivyo Baheza amewataka wakazi wa kata ya Machinjioni kufuata sheria na taratibu za afya ikiwa ni kunawa mikono kwa sababuni kabla na baada ya kula sambamba na kunywa maji yaliyochemshwa  pamoja na kuacha tabia ya kuoga kwenye vyazo vya maji kama alivyoagiza Mganga wa Mkoa.

0 Responses to “HOFU YA KUENEA KWA KIPINDUPINDU YATANDA KIGOMA”

Post a Comment

More to Read