Thursday, January 21, 2016

KAMPUNI ILIYOTAJWA MAHAKAMANI KUTOROSHA TANZANITE YABANWA.




Wizara ya Nishati na Madini imeanza kutumia hukumu iliyotolewa na mahakama kuhusiana na kukamatwa kwa gramu 2015.59 za Tanzanite zenye thamani ya dola za Marekani 310,137.255 (sawa na Sh. milioni 670), zikitoroshwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Desemba 15, mwaka jana.

Katika tukio hilo, raia wa India, Anarag Jain (44),  alikamatwa akitorosha madini hayo kupitia uwanja huo.

Akizungumza mjini hapa jana, Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane, aliitaka kampuni ya Crown Lapidey iliyotajwa kuhusika katika njama za kushirikiana na raia huyo wa India, Jain kutorosha madini hayo kujieleza.

Alisema baada ya kupata hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro iliyoitaja kampuni hiyo kuhusiana na tukio hilo, taratibu za uchunguzi zimeanza.

Alisema serikali inaendelea na uchunguzi kwa kushirikisha wanasheria  na wataiandikia barua kampuni ya Crown Lapidey kujieleza ili kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa kwani madini yaliyokamatwa yameshataifishwa.

Magayane alisema utoroshwaji wa Tanzanite unaifanya Tanzania licha ya kuwa ndiyo eneo pekee ambalo madini hayo yanapatikana duniani kuwa ya tatu katika kuuza madini hayo duniani.

“Takwimu za serikali za mwaka 2014 zimeitaja India kuongoza kwa kupata kiasi cha Sh. bilioni  509, Kenya  Sh. bilioni 173 na Tanzania ikiambulia Sh. bilioni 45.5,” alisema.

Katika hukumu ya kesi ya kutorosha madini hayo iliyokuwa inamkabili mfanyabiashara Jain  ambaye alikamatwa Disemba 15, mwaka jana katika uwanja wa KIA akitorosha madini hayo, ilidaiwa kuwa baadhi ya maofisa wa kampuni hiyo ndio walihusika na njama hizo.

Kampuni hiyo ambayo inamilikiwa na mfanyabiashara wa kiasia raia wa Kenya, Rajan Verma, imetajwa kwenye hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkoa Kilimanjaro, Joachim Tiganga, ambayo ilimtia hatiani mtuhumiwa.

Baada ya hukumu hiyo, Wizara ya Nishati na Madini, imeanza kufanya uchunguzi juu ya vitendo vya kutorosha madini hayo kwenda nje ya nchi.

Ilidaiwa katika kesi hiyo kuwa, mfanyabiashara huyo alinunua madini katika kampuni hiyo huku akiwa hana leseni na ofisa wa kampuni hiyo aliyetajwa kwa jina la Lucas Mdemu ndiye alimsindikiza hadi uwanja wa KIA.

 Mdemu alikanusha kampuni hiyo kuhusika na wizi huo.

0 Responses to “ KAMPUNI ILIYOTAJWA MAHAKAMANI KUTOROSHA TANZANITE YABANWA.”

Post a Comment

More to Read