Sunday, January 24, 2016

KUKU WA AJABU AKWAPUA PESA KIASI CHA SH 430,000 MBEYA




Na Esther Macha, Rungwe
WANACHAMA wa kikundi cha kuweka na kukopa cha Mwijangasyege kilichopo katika Kijiji cha Isange Kata ya Isange katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, wameingia katika hali ya taharuki baada ya kuku wa ajabu kukwapua fedha kiasi cha sh.430,000 na kutokomea nazo.

Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo wanakikundi hao walikuwa katika eneo lao la kukutania wakihesabu fedha hizo kwa lengo la kugawana ndipo kuku huyo alipojitokeza akudonoa pesa hizo na kukimbia kusikojulikana.

Kwa mujibu wa maelezo ya wanakikundi hao, fedha zilizochukuliwa na kuku huyo ambaye wao walidai kuwa ametumwa kishirikina zilikuwa shilingi 430,000 ambazo zilikuwa zimeshahesabiwa zikatengwa pembeni.

Hamu Kitaje, ni miongoni mwa  mwawanakikundi hicho ambapo alisema kuwa kuku huyo alikwapua pesa hizo kwa kasi kubwa mithiri ya mwewe anapokwapua vifaranga vya kuku na kwa kasi hiyohiyo aliyoingia nayo akapotea.

Alidai kuwa mpaka sasa wanashindwa kuelewa kilichokuwa nyuma ya kuku huyo kwa kuwa siotukio la kawaida, na moja kwa moja akalihusisha tukio hilo na mambo ya ushirikina akidai kuwa kwa vyovyote vile alikuwa ametumwa na mtu.


Kitaje alisema kuwa tukio hilo wanalichukulia kama la kishirikina kwa sababu, kabla ya kuku huyo kubeba pesa hizo, ilitokea hali ya tofauti eneo hilo ambapo kulitokea kama ukungu ghafla na ndipo wanakikundi wakawa kama wamepumbazwa ndipo kuku huyo akanyakua pesa hizo walizokuwa wameziweka kwenye ungo.

Alisema kuku huyo alikuwa mwenye rangi nyeupe, ambayo ni aina ya kuku wanasemekana kuwa wanatumika sana katika nguvu za giza na hivyo waliamini kuwa tukio hilo lilikuwa la kishirikina.

“Ilikuwa majira ya saa 11 jioni, tulikuwa tumekaa tunapiga mahesabu ya pesa zetu ili tugawane ndipo akatokea kuku mweupe aliyekuwa anarukaruka na kusogea eneo tulipo, lakini sisi kwa sababu tumezoea kuwa kuku ni ndege wa kawaida anayefugwa hatukuwa na wasiwasi”

“lakini ghafla ilitokea kama ukungu, tukawa tumepumbazwa ndipo ghafla kuku huyo akadonoa fedha zetu na kukimbia nazo,” alisema Kitaje.

Kwa upande wake katibu wa kikundi hicho, Basimenye Silimmani, alisema kuwa jumla ya fedha zote za kikundi hicho zilikuwa 2490,000 lakini na baada ya kurudia mahesabu ili wajuwe kuku huyo alikuwa amebeba kiasi gani ndipo walipobaini kuwa 430,000 hazipo.

Silimmani alisema kuwa  walishindwa cha kufanya baada ya tukio hilo lakini kwa sasa wanamtegemea mungu kwa madai kuwa yeye ndiye aliyekuwa amewapatia njiaza kupata fedha hizo na hivyo wanamtegemea yeye awalinde.


Hata hivyo aliwataka wenzake kutokata tamaa na kwamba kwa kuwa wanamtegemea mungu kikundi chao kitaendelea kuwa imara na kwamba kilichotokea ni jaribu kama majaribu mengine.

Tukio kama hili limekuwa la pili kutokea mkoani Mbeya mwezi huu ambapo mwanzoni mwa mwezi huu lilitokea katika Kijiji cha Ibale kata ya Ibale katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ambapo mbwa alitokomea na pesa za wanakikundi shilingi milioni 1 kati y
a milioni 6 mkoani hapa.

Mwisho.

0 Responses to “KUKU WA AJABU AKWAPUA PESA KIASI CHA SH 430,000 MBEYA”

Post a Comment

More to Read