Saturday, January 23, 2016
RAIS MAGUFULI AFUNGA ZOEZI LA ONESHA UWEZO MEDAN, MONDULI
Do you like this story?
Rais Magufuli akijadiliana jambo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini Jenerali Davis Mwamunyange wakati akielekea kupewa maelezo ya zoezi zima la Onesha Uwezo Medani. |
Rais Magufuli akisalimiana na baadhi ya Maafisa wa jeshi katika tukio hilo la Ufungaji. |
Rais Magufuli akielekea kwenye uwanja wa maonesho akiwa pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini Jenerali Davis Mwamunyange. |
Rais Magufuli akipewa maelezo ya zana mojawapo ya Kivita katika Zoezi la Onesha Uwezo Medani Mkoani Arusha. Picha na IKULU |
Rais Magufuli (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa ngazi za juu wa Jeshi mara baada ya kufunga zoezi la Onesha Uwezo Medani Monduli Mkoani Arusha. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli amefunga “Zoezi la Onesha Uwezo Medani” lililoandaliwa na
kutekelezwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ambalo ni sehemu ya Jeshi la
wananchi Tanzania katika eneo la Lang’arurusu nje kidogo ya Chuo Cha Mafunzo ya
Kijeshi Monduli Mkoani Arusha.
Akizungumza na Askari na Maafisa wa Jeshi la
wananchi Tanzania kabla ya kufunga zoezi hilo, Rais Magufuli amesema katika
awamu yake ya tano ya uongozi amedhamiria kulitumia Jeshi la wananchi Tanzania
katika kujenga uchumi, ikiwemo kuanzisha viwanda na kampuni za ujenzi ili
kuharakisha maendeleo.
Ametoa mfano wa kiwanda cha Nyumbu ambacho
kipo chini ya jeshi la wananchi Tanzania na kueleza kuwa wakati umefika wa
kukiimarisha na kukiendeleza kiwanda hicho, ili kiweze kufanya uzalishaji
mkubwa kwa manufaa ya nchi ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa.
“Zipo nchi nyingi ambazo majeshi yao
yanatumika katika uchumi na yanafanya kazi nzuri ya kupigiwa mfano, wakati
umefika na sisi kufanya hivyo. Hata hizi sare za jeshi na viatu, hatuna sababu
ya kuvinunua kutoka nje ya nchi, tunaweza kutengeneza sisi wenyewe” Alisisitiza
Rais Magufuli.
Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la wananchi
wa Tanzania (JWTZ) kwa kuandaa “Zoezi Onesha Uwezo Medani” ambalo
limethibitisha uwezo, weledi na utayari lilionao katika jukumu lake la
kiulinzi.
Ameahidi kuwa ataendeleza juhudi zilizofanywa
na viongozi wenzake waliotangulia za kuliimarisha kwa vitendea kazi na maslai
ya wanajeshi ili liweze kutekeleza wajibu wake bila vikwazo.
Pamoja na kuwapongeza Askari na maafisa wa
Jeshi la wananchi Tanzania walioshiriki katika zoezi hilo, Rais Magufuli ameagiza
Askari Mgambo na Askari wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT) walioshiriki zoezi hilo
kuajiriwa na jeshi la wananchi Tanzania.
Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya
Rais Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, amesema Wizara yake itaongeza na kusimamia juhudi za kuliboresha jeshi
hilo kwa zana, vifaa na maslai kwa wanajeshi ili kuwajengea uwezo na morali ya
kutekeleza majukumu yao ya kuilinda nchi, pamoja na kutoa msaada stahiki kwa
nchi zenye kuhitaji ulinzi wa amani popote duniani.
Kwa upande wake Mkuu wa majeshi ya Ulinzi
nchini, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange amemhakikishia Rais Magufuli kuwa
Jeshi la wananchi Tanzania lipo imara na litaendelea kutekeleza majukumu yake
kwa weledi, nidhamu ya hali ya juu na uzalendo mkubwa.
Kabla ya kuwahutubia maafisa wa jeshi la
wananchi, Askari na wananchi waliohudhuria ufungaji wa “Zoezi Onesha Uwezo
Medani”, Rais Magufuli ameoneshwa zana mbalimbali za kivita ikiwa ni pamoja na
kushuhudia upigaji wa mizinga ya masafa mafupi, masafa ya kati na masafa
marefu.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
22 Januari, 2016
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
22 Januari, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ RAIS MAGUFULI AFUNGA ZOEZI LA ONESHA UWEZO MEDAN, MONDULI”
Post a Comment