Thursday, January 21, 2016

WAMILIKI WA SHULE, VYUO BINAFSI WAMPONGEZA NDALICHAKO.


Mwenyekiti Taifa wa Shirikisho la Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali, Mrinde Mnzava (kulia) akitoa ufafanuzi kwa wanahabari



WAMILIKI wa shule na vyuo binafsi kupitia Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali wamempongeza Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako kwa kuliagiza Baraza la Taifa la Mitihani kufanya mapitio ya mfumo unaotumika wa sasa wa wastani wa alama (GPA) na kurudisha katika mfumo wake wa zamani wa ‘division’.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti Taifa wa Shirikisho hilo (TAMONGSCO), Mrinde Mnzava, amesema kuwa kupitia shirikisho lao wanampongeza waziri huyo kwa kutoa ufafanuzi juu ya alama za mtihani zilizokuwa zikitumika kwa wanafunzi katika matokeo yao ya mitihani ya sekondari ambapo alama hizo zilikuwa zikileta sintofahamu kwa wazazi walio wengi hapa nchini.

Amesema agizo lake la kuliagiza Baraza la Taifa la Mitihani kupitia mfumo wake upya uliokuwa ukitumika wa GPA ni kwamba sasa wazazi waliokuwa wakienda shuleni kufafanuliwa matokeo ya watoto wao juu ya ufaulu wataweza kufurahia mfumo wa zamani uliokuwa ukitumika wa ‘division’.

Alifafanua kuwa mfumo huo wa GPA ulikuwa unashusha kiwango cha elimu ambapo mwanafunzi alionekana kupata wastani mzuri hata kama alikuwa amefeli kwa kuonesha amefaulu katika alama za chini tofauti na mfumo wa zamani.

Mrinde alieleza kuwa kupitia shirikisho lao watahakikisha wanafunzi wanaendelea kupata elimu bora kwani sababu kubwa zinazopelekea wanafunzi kufeli ni kutokana na kuyumbishwa kwa kubadilisha mitaala ya elimu.

Akizungumzia viwango vya ada wanazotoza katika shule zao alisema wanasubiri kupewa waraka elekezi wa viwango husika na hawana sababu ya kupingana na serikali kwani hata serikali haiwezi kushusha viwango vya ada kuwa chini kabisa bila kuangalia huduma zinazotolewa na shule hizo.
(NA DENIS MTIMA/GPL)

0 Responses to “ WAMILIKI WA SHULE, VYUO BINAFSI WAMPONGEZA NDALICHAKO.”

Post a Comment

More to Read