Thursday, February 11, 2016

ABIRIA 60 WANUSURIKA AJALI MKOANI SINGIDA




Abiria wanakadiriwa kuwa zaidi ya 60 waliokuwa wakisafiri na basi T.974 CDB aina ya scani mali ya kampuni ya Wibonela,wamenusurika kufa baada ya basi hilo kuacha njia na kupinduka.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida,ACP Thobias Sedoyeka,alisema ajali hiyo iliyojeruhi abiria 10,imetokea februari tisa mwaka huu saa 11.40 asubuhi huko katika eneo la kijiji cha Tumuli wilaya ya Mkalama mkoani hapa.

Alisema basi hilo lililokuwa likitokea Kahama likienda jijini Dar-es-salaam likiendeshwa na Mzamidu Ahmed (38) mkazi wa Geita ambaye pia amejeruhiwa vibaya kichwani,lilipinduka kutokana na kuwa kwenye mwendo kasi pamoja na utelezi uliosababishwa na kunyesha kwa mvua.

Alitaja maheruhi wengine kuwa ni Augustino Sylvester (22),Mariamu Abbubakari (20),Juma Simoni (27),Francis Abdul (22),Samson Luziga (24),Clement Aloyce (45),Rahimu Rashid (3),Lemi Mganda (25) na Bruno Ndeliel (40) wote wakazi wa Geita.

“Majeruhi walikimbizwa katika hospitali ya mkoa iliyopo mjini hapa,baadhi bado wanaendelea na matibabu na wengine waliruhusiwa,” alisema Sedoyeka.

Abiria ambao hawakuweza kujeruhiwa,walifaulishwa kwenye basi jingine ambalo hata hivyo,namba zake za usajili hazikuweza kupatikana mara moja.

Kamanda Sedoyeka alisema kuwa uchuguzi wa awali unaonyesha ajali hiyo imesababishwa na mwendo kasi na utelezi ulisababishwa na kunyesha kwa mvua kubwa.

“Nitumie nafasi hii,kuwataka madereva wa vyombo vya usafiri pamoja na watumiaji wengine wa barabara,kuzingatia sheria,kanuni na taratibu za usalma barabarani,ili kuepuka ajali zinazochangia watu kupoteza maisha na mali zao,” alisema.
Imeandaliwa na Nathaniel Limu, Singida

0 Responses to “ ABIRIA 60 WANUSURIKA AJALI MKOANI SINGIDA”

Post a Comment

More to Read