Thursday, February 11, 2016
MAJANGILI 9 WANAOTUHUMIWA KUTUNGUA HELKOPTA WAFIKISHWA MAHAKAMANI
Do you like this story?
Watuhumiwa wakiwa ndani ya gari la polisi, baada ya kufikishwa kituo cha polisi Bariadi wakitokea wilayani Meatu kwa ajili ya kufikishwa mahakamani. |
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Elaston Mbwilo akionyeshwa watuhumiwa wa ujangili ambao walihusika kutungua Helkopta. |
Watuhumiwa wakiwa Mahakamani. |
Watu tisa
wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kutungua helikopta iliyokuwa ikifanya
doria kwenye Pori la Akiba la Maswa wilayani Meatu, Simiyu na na kumuua rubani
wake.
Mbali na kutungua chopa na kumuua rubani wake, Rogers Gower, raia wa Uingereza, watu hao pia wameshtakiwa kwa kukutwa na nyara za Serikali, kuuza na kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Washtakiwa hao
walifikishwa mbele ya Mahakama ya Mkoa wa Simiyu jana wakiwa chini ya ulinzi
mkali wa polisi, huku umati wa wananchi wakifurika na kusababisha hekaheka
mahakamani hapo.
Yamiko Mlekano,
ambaye ni wakili mwandamizi wa Serikali, alidai kuwa washtakiwa wote kwa pamoja
wanakabiliwa na kesi tatu; uhujumu uchumi, mauaji na umiliki wa silaha bila ya
kibali.
Katika kesi
namba mbili ya mauaji, Wakili Yamiko alidai kuwa Shija Mjika (38), Njile Gunga
(28), Dotto Pangali (42) na Moses Mandagu walitungua helikopta hiyo Januari 29
kwenye Hifadhi ya Mwiba iliyoko Kijiji cha Makao wilayani Meatu na kumuua
rubani Gower.
Mlekano alidai
kuwa katika kesi ya uhujumu, mshtakiwa namba moja Iddy Mashaka (49) anadaiwa
kujihusisha na kuratibu tukio la uhujumu uchumi kinyume na sheria.
Mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, John Nkwabi, wakili huyo alida kuwa mshtakiwa
alitenda kosa hilo Januari 6 na Februari Mosi wilayani Meatu kwa kumshauri
mshtakiwa namba mbili, Shija Mjika (38) kuua wanyama wasioruhusiwa.
Katika shtaka
la pili, watu saba; Njile Gunga (28), Dotto Pangali (42), Moses Mandagu (48),
Dotto Huya (45), Mwigulu Kanga (40), Mapolu Njige (50) na Mange Barumu (47) pia
wanashtakiwa kwa kuhujumu uchumi.
Aliieleza
mahakama kuwa kati ya Januari 21 na 29 katika wilayani Meatu, washtakiwa
walipanga na kuratibu tukio la kuwinda wanyama aina ya tembo bila ya kibali cha
Serikali.
Wakili Mlekano
alidai kuwa shtaka la tatu la uwindaji wanyama wasioruhusiwa linawakabili
mshtakiwa wa pili hadi tisa na wanadaiwa kutenda Januari 26 na 29 kwenye
Hifadhi ya Mwiba Kijiji cha Makao wilayani Meatu wa kumuua tembo mwenye thamani
ya Sh32,891,100 bila ya kibali.
Katika shtaka
la nne, mshtakiwa namba mbili na tisa wanatuhumiwa kumiliki nyara za Serikali
kinyume na sheria.
Washtakiwa wanadaiwa
kutenda kosa hilo Januari 29 na Februari Mosi wilayani Meatu ambako walikamatwa
na meno ya tembo yenye uzito wa kilo 31 na thamani ya Sh32,891,100.
Katika shtaka
namba tano, Mashaka na Mjika wanashtakiwa kwa kuuzaji nyara za Serikali kinyume
na sheria na kwamba walitenda kosa hilo kati ya Januari 6 na Februari Mosi
wilayani Meatu.
Hakimu Nkwabi
alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo
kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na aliahirisha hadi Februari 24 zitakapotajwa
tena.
Katika kesi ya
tatu ambayo ni kukutwa na silaha kinyume cha sheria iliyosomwa mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Wilaya, Mary Mrio, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matano.
Washtakiwa hao
ni Buluma, Mjika, Pangani, Ngunga, Mandagu, Huya na Kanga ambao baadhi yao
walikiri kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria akiwamo Njile anayedaiwa
kutungua helikopta hiyo.
Washtakiwa hao
walikiri mashtaka mawili ambayo ni kukutwa na bunduki aina ya Riffle 303,
wakati Ngunga na Mandagu walikiri shtaka la tatu, nne na tano la kukutwa na
silaha na risasi bila ya kibali.
Hata hivyo,
Hakimu Mrio alishindwa kutoa hukumu kwa washtakiwa waliokiri kosa kutokana na
kutokuwapo kwa vielelezo mahakamani hapo, hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi
leo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MAJANGILI 9 WANAOTUHUMIWA KUTUNGUA HELKOPTA WAFIKISHWA MAHAKAMANI”
Post a Comment