Saturday, February 20, 2016

CHATU AZUA KIZAAZAA SONGEA




SONGEA: WAKAZI wa Mtaa wa Matuli Kata ya Majengo na Mfaranyaki-Makaburini, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, wameingiwa na hofu ya usalama wa maisha yao baada ya kuonekana kwa chatu anayezunguka katika pori la mto unaotenganisha maeneo hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari mjini hapa, wananchi hao walisema kuwa chatu huyo ameonekana zaidi ya mara tatu kwa nyakati tofauti tangu wapate taarifa ya uwepo wa chatu huyo katika maeneo hayo hali inayosababisha shughuli za kilimo katika bonde la Mto Ruvuma kusimama.

Kama hiyo haitoshi, chatu huyo amesababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo kutokana na kuhofia usalama wao.

Fatuma Omary na Zainabu Msangu, wakazi wa Majengo, Mtaa wa Matuli walisema kuwa mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Mfaranyaki aliwatahadharisha wananchi kuwa ofisi yake imepokea taarifa ya kuwepo kwa chatu mkubwa katika bonde la Majengo na kuwataka wawe makini wanapotembea na kufanya shughuli za kilimo.

Aidha, Afisa Mifugo, Aletas Kapinga anayeishi katika bonde hilo, aliwaomba maafisa wanyamapori kutumia ujuzi walionao kumtafuta nyoka huyo anayetishia maisha ya wananchi na mifugo yao kwani shughuli za kilimo na bustani zimesimama.

Kufuatia tukio hilo inadaiwa kuwa mbwa watatu pamoja na kuku wawili wamekamatwa na kumezwa na chatu huyo jambo linalosababisha watoto kukatazwa kwenda kuchota maji kwenye bonde hilo na wengine kushindwa kwenda kumwagilia bustani zao.

Kwa upande wake, Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Songea, Oscar Bakumbezi amethibitisha kuwa ofisi yake imepokea taarifa toka kwa wananchi wa maeneo hayo kuhusu uwepo wa chatu huyo na kwamba amekwisha kamata mbwa watatu na kuku wawili na tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kufanya doria ya kumsaka nyoka huyo na amewataka wananchi kufanya usafi wa mazingira kwa kufyeka nyasi kwenye maeneo yote yanayozunguka nyumba zao.

0 Responses to “ CHATU AZUA KIZAAZAA SONGEA”

Post a Comment

More to Read