Monday, February 1, 2016

UZINDUZI WA SHEREHE ZA MIAKA 39 YA KUZALIWA KWA CCM KISIWANDUI MJINI UNGUJA


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Wananchi na Wanachama cha Mapinduzi  katika mkutano wa hadhara wa Mikoa minne  ya Unguja shamra shamra za Uzinduzi wa sherehe za miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM katika uwanja wa Ofisi kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanziba

Baadhi ya Wananchi na Wanachama cha Mapinduzi (CCM) wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akitoa hutuba yake katika shamra shamra za Uzinduzi wa sherehe za miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM katika uwanja wa Ofisi kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.


Na Ally Ndota, Zanzibar
Makamo  Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amesema kuwa miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM ni kilele tosha cha kupatikana kwa maendeleo katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Akizungumza katika uziunduzi wa miaka 39 ya kuzaliwa kwa chama hicho katika viwanja vya Afisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, amesema kuwa maendeleo yaliyopatikana katika serikali zote mbili ya Tanzania bara na Zanzibar yamesimamiwa na miongozo, ilani na mikakati mbali mbali iliyotokana na CCM.

Dkt. Shein alisema kuwa CCM iliyozaliwa mwaka 1977 baada ya kuungana kwa vyama viwili vya ukombozi vikiwemo TANU na Afro shraz party (ASP), chama hicho kimeweza kupigania haki za wanyonge kwa kusimasmisha serikali zenye misingi imara ya kuwatumikia wananchi kwa moyo wote bila ya ubaguzi.

“ Serikali nyingi zilizoundwa na vyama vya ukombozi duniani zimeangushwa na wakoloni kwa njia za kiutapeli lakini sisi serikali zetu bado ni imara na zitaendelea kutawala wananchi kwa njia bora na za kidemokrasia.

Pia ni lazima tuendelee kujitathimini kwa kila jambo nje na ndani ya chama chetu kwani bado kuna changamoto mbali mbali zinazotakiwa kufanyiwa kazi ipasavyo”, alisema Dkt. Shein.

Aidha Dkt. Shein aliwasihi wafuasi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20 mwaka huu, ili wapatikane viongozi wa kuongoza dola kwa miaka mitano ijayo.

Dkt.Shein alifafanua kwamba msingi wa uchaguzi wa marudio upo kikatiba kwani uchaguzi mkuu uliopita ulifutwa kisheria na mamlaka iliyokuwa inahusika na usimamizi na uratibu wa uchaguzi huo baada ya kubaini kasoro.

Akizungumzia mgogoro wa kisiasa uliopo visiwani Zanzibar, Dkt. Shein alisema kuwa ulikuwa utatuliwe kwa njia za mazungumzo lakini kiongozi wa CUF ambaye ni Maalim Seif Sharif Hamad aliyeomba mazungumzo ya maridhiano kabla hayajamaliza yeye alienda kutoa siri za vikao kwa waandishi wa habari Dar es saalam na baadae kuandika barua ya kujitoa katika mazungumzo hayo.

Aidha aliwataka wananchi kuendelea kulinda Amani na utulivu wa nchi na kuepuka kutumiwa na baadhi ya vyama vya kisiasa kufanya vurugu sizisokuwa na msingi kwa maslahi ya nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kuwa Zanzibar CCM itaendelea kuwa chama cha wananchi wote kinachoongozwa na uzalendo.

Alisema kuwa mpaka sasa CCM Zanzibar imejiandaa kwa kila hatua katika kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20 mwaka huu.

0 Responses to “ UZINDUZI WA SHEREHE ZA MIAKA 39 YA KUZALIWA KWA CCM KISIWANDUI MJINI UNGUJA”

Post a Comment

More to Read