Thursday, March 10, 2016

RIPOTI YA MADAWA YA KULEVYA YAZINDULIWA NCHINI, BIASHARA YA BANGI, MIRUNGI, HEROIN YAONGOZA.


Uzinduzi wa Ripoti ya Bodi ya Kimataifa ya Kuzuia Madawa ya Kulevya (INCB) ukifanyika.

Mkuu wa Elimu, Habari na Takwimu kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Amani Msami akisoma ripoti ya Bodi ya Kimataifa ya Kuzuia Madawa ya Kulevya (INCB).

Afisa Habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Bi. Stella Vuzo akizungumza kuhusu ripoti ya INCB kuhusu madawa ya kulevya. Kulia ni Afisa wa Umoja wa Mipango wa Umoja wa Mataifa anayesimamia udhibiti wa dawa za kulevya na uhalifu unaosababishwa na madawa ya kulevya, Immaculate Maliyamkono.

Mkemia Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Yovin Ivo akizungumza jambo kuhusu madawa ya kulevya. Kushoto ni Mkuu wa Elimu, Habari na Takwimu kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Amani Msami.


Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) kimezindua ripoti ya Bodi ya Kimataifa ya Kuzuia Madawa ya Kulevya (INCB) na kuelezea hali ya matumizi ya madawa ya kulevya ilivyo nchini na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.

Akisoma ripoti hiyo, Mkuu wa Elimu, Habari na Takwimu kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Amani Msami alisema katika ripoti hiyo inaonyesha kuanzia mwaka 2014 biashara ya Bangi, Mirungi na madawa ya kulevya aina ya Heroin yaliongezeka na katika kipindi cha mwaka 2013 zaidi ya Kilo 321 za Heroin zilikamatwa nchini.

Alisema nchi za Afrika Mashariki zimekuwa zikitumika kama sehemu ya kupitishia madawa kwenda maeneo mengine ya dunia ambapo dawa hizo zimekuwa zikitokea nchi za Afghanstan, India, Iran na Pakistan na kupelekwa nchi kama China, Japan, Afrika Kusini, Marekani na nchi zingine za Ulaya.

Aliongeza kuwa madawa hayo yamekuwa yakipitishwa nchini kwa kutumia meli kubwa ambazo zimekuwa zikitumia majahazi, mashua, ngalawa na boti ziendazo kasi ili kufikisha madawa ya kulevya nchi kavu.

Aidha alieleza kupitia ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika kila watu 100 barani Afrika, watu 8 wanakuwa wanatumia bangi na hivyo kuifanya bangi kuongoza kwa matumizi makubwa Afrika na zaidi matumizi ya bangi ipo nchi za Afrika Magharibi na Afrika ya Kati.
Madawa mengine yanayoongoza kwa matumizi makubwa Afrika ni pamoja na madawa aina ya Heroin ambapo katika watu 1,000 watu 3 wanatumia madawa hiyo na Cocaine inashika nafasi ya tatu kwa matumizi makubwa.

Pia alisema kuwa ripoti imezitaja nchi za Tanzania, Kenya na Senegal kwa kuanza kutoa huduma ya kuwapa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya, dawa za Methadone ambazo zinasaidia kuwarudisha waathirika katika hali zao za awali.

“Ripoti hii inaonyesha jinsi hali ilivyo na Tanzania kama nchi wanachama inatakiwa ifanye baadhi ya marekebisho ili kuzuia biashara na matumizi na hawa wafanya biashara wa haya madawa wanatumia sana watu wenye kipato cha chini na wakifikisha mizigo yao wanawalipa,” alisema Msami.

Nae Afisa wa Umoja wa Mipango wa Umoja wa Mataifa anayesimamia udhibiti wa dawa za kulevya na uhalifu unaosababishwa na madawa ya kulevya, Immaculate Maliyamkono alisema ripoti imeyotolewa na INCB inaonyesha kuwa bado kuna biashara ya madawa za kulevya kwa nchi za Afrika Mashariki na hivyo ni wajibu wao kama wanachama wa bodi hiyo kuangalia upya sera zao ili kudhibiti biashara na matumizi ya madawa ya kulevya.

“Kama ripoti imevyoonyesha INCB inawataka wanachama wake wafanye sawa na mkataba wa mwaka 2009 ili kuzuia biashara ya haya madawa na hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na kubadili sera inayotumika sasa,” alisema Bi. Maliyamkono.


0 Responses to “RIPOTI YA MADAWA YA KULEVYA YAZINDULIWA NCHINI, BIASHARA YA BANGI, MIRUNGI, HEROIN YAONGOZA.”

Post a Comment

More to Read