Friday, September 9, 2016
MAHAKAMA YAIZUIA NHC KUPIGA MNADA MALI ZA FREEMAN MBOWE
Do you like this story?
Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi imeliamuru Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
kutouza au kupiga mnada mali za Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mpaka kesi ya msingi itakapomalizika.
Shirika
hilo lilizichukua mali mbalimbali za kampuni za Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa
Jimbo la Hai, wiki iliyopita kupitia mawakala wa kampuni ya Fosters Auctioneers
katika jengo lililopo makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Gandhi (Makunganya)
jijini Dar es Salaam.
Hatua
hiyo ya NHC ilitokana na mgogoro wa muda mrefu, wakimtuhumu Mbowe kushindwa
kulipa deni la zaidi ya Sh. 1.3 bilioni, ikiwa jumla ya fedha za kodi ya
kupangishwa kwenye jengo hilo.
Kutokana
na mvutano huo, Mbowe alifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi,
kupinga hatua ya NHC kumuondoa katika jengo hilo, pamoja na kuchukua mali zake
huku wakitangaza kuzipiga mnada baada ya siku 14 tangu kuzichukua.
Jana,
Jaji Siyovelwa Mwangasi alitoa zuio na kuiamuru NHC kutouza wala kupiga mnada mali
hizo za Mbowe mpaka mahakama hiyo itakapotolea uamuzi katika kesi ya msingi.
Katika
kesi hiyo namba 722 ya mwaka 2016, Mbowe anawakilishwa na Mawakili Peter
Kibatala na Omary Msemo.
Jaji
Mwangasi amesema kuwa, anakubaliana na maombi ya mlalamikaji na kutaka mali
hizo zisiuzwe hadi hapo mahakama itakapofanyia uamuzi kesi ya msingi.
Hatua
hiyo inakuja baada ya upande wa NHC kupitia mawakili wake Aloyce Sekule na
Miriam Mungula kushindwa kuwasilisha hoja za msingi kueleza, ni kwanini zuio
hilo lisitolewe hadi hapo kesi ya msingi itakapoanza kusikilizwa.
Awali,
mawakili wa NHC, walidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi
ya Mbowe kwa kuwa hakuna kesi ya msingi ambayo imefunguliwa, hivyo maombi hayo
yatupiliwe mbali.
Wakili
Kibatala alijibu hoja hiyo kwa kusema, hatua ya kuwasilisha maombi hayo
inalenga kubaini kama kweli Mbowe anadaiwa kodi ama la.
Kibatala
alidai kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo inaweza
ikatoa uamuzi wowote, na ndiyo maana wamewasilisha maombi hayo ili itolewe amri
ya muda ya kuzuia mchakato huo.
Miongoni
mwa hoja za Mbowe alizoziwalisha mahakamani hapo, ni pamoja na hoja kuwa, yeye
(Mbowe) na shirika hilo walikubaliana kwamba atalikarabati na kulipanua jengo
hilo kwa asilimia 100. Makubaliano ambayo yaliingiwa mwaka 1997.
Amedai
kuwa katika makubaliano hayo yeye na NHC walikubaliana watamiliki jengo hilo
kwa pamoja kwa muda wa miaka 99, huku Mbowe katika mgawanyo wa mapato akitakiwa
kupata asilimia 75 na NHC ikitakiwa kupata asilimia 25.
Pia
alieleza kuwa katika makubaliano hayo, licha ya mwenendo wa kibiashara kutokuwa
mzuri, muda wote alikuwa akilipa asilimia hiyo 25, kwa mujibu wa makubaliano
yao.
Hivyo
kutokana na hatua ya NHC kuvunja mkataba huo kwa kumtoa kwenye jengo na
kuchukua mali zake, anaiomba mahakama iliamuru shirika hilo limlipe fidia.
Mbowe
aliondolewa kwenye jengo husika mnamo Septemba mosi kwa madai ya kushindwa
kulipa deni la zaidi ya Sh. bilioni 1.3.
Mawakala
wa NHC walifika katika jengo hilo saa 12:30 asubuhi na wafanyakazi zaidi ya 50
na kwenda moja kwa moja katika kampuni ya Free media pamoja na ukumbi wa
Bilcanas na kuchukua vifaa mbalimbali ikiwemo, meza, viti na kompyuta.
Siku
chache baada ya kuondolewa kwa Mbowe katika jengo hilo, Rais John Magufuli
alilisifu shirika hilo kwa hatua hiyo na kulitaka lichukue hatua kama hizo kwa
wadaiwa wengine zikiwemo taasisi za umma
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “ MAHAKAMA YAIZUIA NHC KUPIGA MNADA MALI ZA FREEMAN MBOWE”
Post a Comment