Sunday, October 23, 2016
MFALME WA MOROCCO KUPOKEWA KWA MABANGO LEO HAPA NCHINI
Do you like this story?
Wakati
Mfalme wa Morocco, Mohamed VI akitarajiwa kuwasili leo nchini kwa ziara ya
kikazi, huenda akapokewa kwa mabango baada ya vijana wanaounda kamati ya
mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi (TASSC) kujipanga kufanya hivyo
kushinikiza nchi hiyo kuacha kuitawala kwa mabavu Sahara Magharibi.
Vijana
hao wamefikia uamuzi huo kutokana na kile walichodai kusikitishwa kwao na
kitendo cha Morocco kuendelea kuitawala kwa mabavu nchi ya Sahara Magharibi na
kupuuza wito wa Umoja wa Mataifa (UN) unaoitaka kuipa uhuru nchi hiyo.
Hata
hivyo, Serikali ya Tanzania kupitia msemaji wake, Hassan Abass imesema ujio huo
ni muhimu kwa uhusiano wa kidiplomasia na uchumi.
“Serikali
ilishaeleza msimamo wake, kuna uhusiano wa aina nyingi, ujio huu ni muhimu kwa
uhusiano wa kidemokrasia na uchumi kama hisia zitawatuma kufanya hivyo,
wanapaswa kufuata sheria,” alisema
Abass.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa TASSC, Alphonce
Lusako alisema jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili Morocco iiache huru
Sahara Magharibi lakini watawala wa nchi hiyo wamekuwa wagumu kuruhusu hilo.
Lusako
alieleza kuwa TASSC inafahamu fika kwamba Mfalme Mohamed VI amekuwa akifanya
ziara katika mataifa mbalimbali akijaribu kutafuta kuungwa mkono ili Morocco
iendelee kuitawala Sahara Magharibi.
Alisema
Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazoitambua Sahara Magharibi inapaswa
kumuonyesha wazi Mfalme Mohamed VI kuwa haiungi mkono utawala wa kimabavu.
“Tunamtaka
Mfalme wa Morocco kuacha mara moja vitendo vya kibeberu vya kuikalia Sahara
Magharibi sambamba na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na wanaharakati
wanaoshikiliwa magerezani katika maeneo yanayokaliwa kimabavu.
"Ni
aibu kwa nchi moja ya Kiafrika kuitawala nchi nyingine: Tunaunga mkono msimamo
wa Tanzania wa kuendelea kuitambua na kuiunga mkono Sahara Magharibi kwenye
vyombo vya kimataifa na tunasisitiza isiyumbishwe katika msimamo huo, ” alisema.
Katibu
wa TASSC, Jasper Hassan alisema tangu kamati hiyo ianzishwe mwaka jana imekuwa
ikifanya harakati mbalimbali ikiwamo mihadhara ya wazi inayolenga kuisukuma
Morocco kuacha kuitawala Sahara Magharibi.
“Jitihada
zilianza muda mrefu ila mwaka jana ndiyo vijana tukaona tuingilie kati tukiwa
kama Waafrika, tunapinga kila aina ya unyonyaji tunataka Sahara Magharibi iwe
huru,” alisema Hassan.
Juzi,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema ziara ya kiongozi huyo
itakuwa na manufaa kwa nchi, kwani akiwa na mwenyeji wake, Rais John Magufuli
watasaini makubaliano 11 ya ushirikiano katika sekta za kilimo, gesi, mafuta,
Reli ya Liganga na Mchuchuma na sekta ya utalii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MFALME WA MOROCCO KUPOKEWA KWA MABANGO LEO HAPA NCHINI”
Post a Comment