Monday, October 24, 2016
WAZIRI MAKAMBA ATOA SIKU TANO KUSITISHWA KWA SHUGHULI ZA KILIMO NA UFUGAJI KATIKA KINGO ZA MTO RUKWA.
Do you like this story?
Waziri wa
Mazingira na Muungano, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe January Makamba amesema serikali itatangaza eneo la Ziwa
Rukwa kuwa eneo nyeti la Mazingira na kuagiza kusitishwa kwa shughuli zote za
Kilimo na Ufugaji zinazofanyika katika kingo za Ziwa Rukwa na kutoa siku 5 hadi
tarehe 28 mwezi huu kuhakikisha agizo hilo limetekelezwa.
Waziri
Makamba ametoa tamko hilo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nankanga,
Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa eneo
la Forodhani lililopo katika fukwe za Ziwa Rukwa ambapo ametanabaisha kuwa kina
cha Ziwa hilo limepungua kwa takribani mita 3 katika kipindi cha miaka 16
ambapo mwaka 2000 kina hicho kilikuwa mita 6 na hivi sasa ni takribani mita 3
pekee.
Waziri
Makamba ameainisha kuwa Serikali itachukua hatua za muda mrefu kuokoa Ziwa hilo
lakini katika hatua za awali za kuokoa Ziwa Rukwa ameagiza kuwa kuanzia tarehe 28 ya mwezi huu
haitoruhusiwa kufanya Kilimo ndani ya Mita 60 za ukingo wa Ziwa kama
inavyotakiwa na Sheria ya Mazingira, Sheria ya Maji na Sheria ndogo za Serikali
za Mitaa lakini vilevile kuanzia tarehe 28 mwezi huu haitoruhusiwa kuchunga na
kufuga mifugo ndani ya mita 200 za ukingo wa Ziwa.
Katika hatua
nyingine Waziri Makamba amesema Serikali itatoa agizo kwa Halmashauri zote za
Wilaya ambazo Ziwa Rukwa linapita kukutana na kukusanya pesa kutoka katika
vyanzo vyake ili ziweke alama (Beacon) na vibao katika mita 60 na Mita 200
kutoka kwenye Ziwa kujulisha umma kuwa hairuhusiwi kufanya shughuli katika
maeneo husika.
Amesisitiza
upandaji miti katika mkoa wa Rukwa akisema Mkoa huu bado upo nyuma sana katika
upandaji wa miti huku ukataji wa miti ya asili ukiwa ni mkubwa sana hivyo
kuagiza zoezi la upandaji miti kuanza mara moja.
Katika
kushughulikia tatizo la uvuvi kwa kutumia sumu na baruti amesema serikali
itaongeza adhabu ya wote watakaopatikana na kosa hilo ili kukomesha tabia hiyo
mara moja
Vilevile
ameutaka uongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri kuanza mara moja mchakato wa
kujua na kutambua idadi ya mifugo na wamiliki wake ili kuwezesha kutambua eneo
sahihi la kutengwa kwaajili ya wafugaji na kupunguza ufugaji holela ambapo hilo
ni kwa mujibu wa Sheria ya Mifugo namba 12.
Waziri
Makamba anaendelea na ziara yake mahsusi ya mazingira katika Mikoa 10 ambapo
amepokea taarifa ya Halmashauri ya Mazingira na Misitu ya Wilaya ya Sumbawanga
ambayo mbali na mengine imeonesha kuwa imeshatoa notisi kwa wavuvi
wanaotumia zana haramu kwa uvuvi
kuzisalimisha zana hizo kwa hiari hadi Novemba 17 na baada ya hapo mamlaka
husika na vyombo vya dola vitachukua hatua stahiki
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MAKAMBA ATOA SIKU TANO KUSITISHWA KWA SHUGHULI ZA KILIMO NA UFUGAJI KATIKA KINGO ZA MTO RUKWA.”
Post a Comment