Thursday, December 17, 2015

MADIWANI WATAKIWA KUBUNI NJIA ZA KUJIINGIZIA MAPATO,ABBAS KANDORO



Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro


NA SAMWEL NDONI, ILEJE
MKUU wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amewashauri madiwani wanaounda Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kubuni miradi mbalimbali ya kuliingizia kipato ili waweze kuwa na bajeti isiyotegemea msaada kutoka Serikali kuu.

Kandoro alitoa ushauri huo katika mkutano wa kwanza wa baraza la madiwani hao, ambapo alisema kuwa endapo madiwani hao watakuwa na vyanzo vingi vya mapato wataweza kuharakisha shughuli za maendeleo ya wilaya hiyo.

Alisema kuwa mpaka sasa Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, ni kwakiasi kikubwa huku akidai kuwa asilimia 92 ya bajeti hiyo inategemea fedha kutoka katika tegemezi serikali kuu, hali ambayo alidai inafanya wilaya hiyo isipate maendeleo haraka kama ilivyo kwa wilaya zingine za mkoa wa Mbeya.

Aidha katika mkutano huo wa baraza la Madiwani hao ulifanyika uchaguzi wa Mwenekiti na makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo pamoja na uundwaji wa kamati  mbalimbali za maendeleo.

Katika uchaguzi huo Diwani wa Kata ya Bupigu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ubatizo Songa, alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Halmashauri hiyo kwa kupita bila kupingwa, ambapo alipigiwa kura za ndio 24 zilizompa nafasi yakuweza kuiongoza Halmashauri hiyo kama Mwenyekiti.

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, diwani wa kata ya Isongole pia kupitia CCM, Gwalusako Kapesa, alipita bila kupingwa kama ilivyokuwa kwa mwenyekiti na kupigiwa kura za ndio 24.

Wagombea wa CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje walipita bila kupingwa kutokana na vyama vya upinzani kuwa na Mgombea mmoja pekee kutoka Chadema, ambaye ni Diwani wa kata ya Chitete.

Baada ya kufanyika kwa Uchaguzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Rosemary Senyemule, aliwataka madiwani hao kuwajibika ipasavyo ili kuendana na kasi ya Rais Dk. John Magufuli ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 alipata kura nyingi katika Wilaya hiyo kuliko katika Wilaya nyingine zote za mkoa wa Mbeya.

Senyamule alisema ili kudhihirisha kuwa kura ambazo wananchi wa Ileje walimpigia Dk. Magufuli pamoja na madiwani hao zilikuwa ni za maendeleo ya wananchi wafanye kazi kwa bidii ili wananchi wafurahie matunda ya kura zao.

Wilaya ya Ileje ina jumla ya kata 18 ambapo katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu, Chama cha Mapinduzi kilipata Jumla ya kata 17 huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiambulia kata moja hali iliyokifanya CCM kuongoza Halmashauri hiyo bila kupingwa.
Mwisho.

0 Responses to “MADIWANI WATAKIWA KUBUNI NJIA ZA KUJIINGIZIA MAPATO,ABBAS KANDORO”

Post a Comment

More to Read