Thursday, December 17, 2015
BILLION 131 ZATENGWA ELIMU BURE
Do you like this story?
RAIS John Magufuli amewahakikishia Watanzania
kuwa fedha kwa ajili ya kutimiza ahadi ya kutoa elimu bure kwa shule za msingi
na sekondari, zimetengwa Sh bilioni 131 mwezi huu na kupelekwa moja kwa moja
katika shule husika.
Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa
Wilaya na Wakuu wa Mikoa, watapatiwa nakala za taarifa za ugawaji wa fedha hizo
na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayethubutu kuzitumia
vibaya.
Rais Magufuli alisema hayo Ikulu Dar es
Salaam jana muda mfupi baada ya kupokea ujumbe maalumu kutoka kwa Waziri Mkuu
wa Japan, Shinzo Abe aliyemtumia salamu za pongezi kwa kuchaguliwa kuiongoza
Tanzania.
Dk Magufuli aliongeza kuwa fedha hizo ambazo
ni pamoja na fedha za maendeleo, fedha za mitihani na fedha vifaa vya ku
fundishia zitaanza kutumwa kila mwezi kuanzia mwezi huu.
Katika kipindi cha kampeni, Rais Magufuli
aliahidi kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari kidato cha nne
na hivi karibuni kupitia Wizara ya Elimu ilitoa waraka maalumu wa kusisitiza
agizo hilo la elimu bure.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli
amempongeza Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Philip
Mpango kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato inayofanywa na mamlaka hiyo.
“Kwa mara ya kwanza mwezi huu ukusanyaji wa
mapato hayo unatarajiwa kuwa zaidi ya shilingi trilioni moja na bilioni mia
tatu,” alisema Rais Magufuli katika taarifa hiyo iliyotolewa jana na Ikulu.
Rais Magufuli pamoja na mambo mengine, jana
alipokea ujumbe maalumu wa maandishi kutoka kwa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo
Abe uliowasilishwa na Waziri wa Nchi anayeshughu likia Mambo ya Nje ya Japan,
Seiji Kihara.
Ujumbe huo umemueleza Rais Magufuli kuwa
Japan imeridhishwa na hatua ambazo Serikali ya Tanzania inazichukua katika
kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuahidi kuongeza msukumo kwa
upande wa Japan katika kuharakisha utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na
Japan nchini.
Mjumbe huyo juzi alishuhudia utiaji saini wa
makubaliano ya ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilometa 441.5 kutoka
Singida – Manyara – Namanga na kuunganisha hadi Kenya, ambapo Japan imetoa
mkopo wa Dola za Marekani milioni 96 ili kufanikisha mradi huo.
Akizungumza baada ya kuagana na Mjumbe huyo
Maalumu, Rais Magufuli alisema kwa kuwa Tanzania inaelekea kuwa na umeme wa
ziada, mradi huo ukikamilika utaiwezesha kuuza umeme nje nchi.
Kuhusu ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa
gesi wa Kinyerezi II, ambao Japan imetoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 292
kwa ajili ya kuutekeleza, Rais Magufuli alisema baada ya kubana matumizi katika
bajeti ya serikali, wiki hii Tanzania itakamilisha utoaji wa kiasi cha Dola za
Marekani milioni 51.8 ambazo ni sawa na asilimia 15 ya fedha zote
zitakazogharimia ujenzi huo.
Aidha, Rais Magufuli alisema taratibu za
kuanza ujenzi wa barabara ya juu yaani “Flyover” katika makutano ya barabara
eneo la Tazara zimeanza na kwamba jiwe la msingi linatarajiwa kuwekwa mwezi
ujao, na kwamba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Flyover hiyo ya kwanza nchini zipo
na mkandarasi ameshalipwa fedha za awali.
Dk Magufuli pia alizungumzia ujenzi wa
barabara nyingine mbili ambazo ni ya Gerezani – Bendera Tatu itakayokuwa na
flyover katika eneo la Kamata na Barabara ya Mwenge – Morocco na kwamba Japan
imeahidi kutangaza zabuni hizo hivi karibuni
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


.gif)


0 Responses to “ BILLION 131 ZATENGWA ELIMU BURE”
Post a Comment