Tuesday, November 8, 2016
TAARIFA KUTOKA IKULU: MAAGIZO YA RAIS MAGUFULI KWA SUMA JKT KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO YA CHAKULA
Do you like this story?
Shirika la
uzalishajimali lililo chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (Suma – JKT) litaanza
kutekeleza mpango wa kufuga samaki kwa kutumia vizimba (Cages) katika bahari ya
Hindi baada ya mpango huo kuonesha mafanikio makubwa katika mito na maziwa
mbalimbali hapa nchini.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa JKT Meja Jenerali Michael Isamuhyo muda mfupi baada ya
kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Meja
Jenerali Isamuhyo amesema ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba umepata
mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali nchini hususani katika ziwa Viktoria
na kwamba ili kupanua ufugaji huo Suma-JKT inajielekeza kufuga samaki katika
bahari ya Hindi.
Ameongeza
kuwa pamoja na ufugaji wa Samaki, Rais Magufuli ameliagiza Jeshi la Kujenga
Taifa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na shughuli zilizotajwa katika
misingi ya uanzishaji wa jeshi hilo ili Serikali isipate gharama za kununua
chakula kwa ajili ya vijana wanaokwenda kupata mafunzo ya JKT na pia kupata
chakula cha ziada ambacho kitatumika kutatua tatizo la uhaba wa chakula katika
maeneo yatakayokumbwa na uhaba.
Meja
Jenerali Isamuhyo ameongeza kuwa Rais Magufuli ameitaka JKT kujenga mabwawa kwa
ajili ya kuanzisha kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yanayofaa kwa kilimo
hicho.
Aidha, Mkuu
huyo wa JKT amebainisha kuwa JKT itahakikisha inasimamia utekelezaji wa
maelekezo ya Mhe. Rais na kuongeza kuwa kazi hii itakwenda sambamba na
utekelezaji wa majukumu mengine ya JKT yaliyoainishwa katika uanzishwaji wake
mwaka 1963 ikiwemo ujenzi kwa gharama nafuu.
Wakati huo
huo, Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Jenerali Mstaafu
George Marwa Waitara Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
08 Novemba,
2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TAARIFA KUTOKA IKULU: MAAGIZO YA RAIS MAGUFULI KWA SUMA JKT KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO YA CHAKULA”
Post a Comment