Tuesday, November 8, 2016

BURIANI BABU: NIMJUAVYO SAMWEL JOHN SITTA






Alfajiri ya leo, Novemba 7, 2016 imekuwa siku ya huzuni na majonzi makubwa kwa Taifa. Tuliamka na kukutana na habari za kusikitisha juu ya kifo cha Mzee wetu Samwel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mzee Sitta alikuwa mgonjwa kwa kitambo kidogo, lakini bado tulikuwa na matumaini kuwa afya yake ingetengamaa na kuendelea kuwa nasi.

Habari hizi za kufariki dunia kwake zilizosambaa kwa kasi kubwa kupitia mitandao ya kijamii zimetushtusha mno. Hatimaye taarifa rasmi ikatoka kuthibitisha habari hizo. Kuwa Mzee watu amefariki dunia akiwa kwenye matibabu nchini Ujerumani.

Samwel John Sitta aliitumikia nchi yetu kwa muda mrefu na kwa uadilifu mkubwa sana. Si hivyo tu, sisi wengine pia kwa kiasi flani Hata kukua kwetu kisiasa kumetokana na utumishi wake uliotukuka kwa nchi yetu alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika tanzia hii ninamkumbuka Mzee Sitta Kwa namna nilivyofungamana naye binafsi na namna nilivyomshuhudia katika kazi zake mbalimbali za uongozi.

Samwel Sitta ananigusa mimi binafsi moja kwa moja. Alikuwa Babu yangu. Tukiwa Bungeni akiniandikia kitu alikuwa akitumia neno hilo 'babu' kwa mwandiko wake mzuri usiotoka kwenye kumbukumbu zangu kabisa. Labda siku za usoni 'vinote' (vimemo) hivi vinaweza kuchapishwa pindi watafiti watakapokuwa wakiandika historia ya nchi yetu na Bunge letu. Hivyo siku zote za maisha yetu nilimuita babu.

Disemba 29, 2005 mzee Sitta aliniapisha kiapo cha ubunge tarehe. Maneno ambayo aliniambia baada ya kunikabidhi Kanuni za Bunge na Katiba ya Nchi niliyaandika kwenye daftari langu la kumbukumbu siku hiyo hiyo jioni. Baada ya kula kiapo cha Utii na cha uaminifu kawaida Wabunge hupewa mkono na mwapishaji na kupewa nyaraka za kazi.

Kwangu haikuwa hivyo, Mzee Sitta alinikumbatia na kuniambia "Utakuwa Kiongozi muhimu sana kwa nchi yetu. You have a bright future (unayo kesho njema)". Maneno haya hayajawahi kunitoka katika kumbukumbu zangu, ni maneno ya faraja na msukumo wa kunitaka kwenda mbele kila ninapopata misukosuko ya kisiasa. Mara kadhaa yeye mwenyewe alikuwa akinipigia na kunikumbusha juu ya maneno yake haya na kunitia moyo.

Babu Sitta alikuwa Mlezi wa wanasiasa vijana, binafsi amenilea na kunisomesha. Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Tano (Form Five) katika Shule ya Sekondari ya Galanos ya jijini Tanga, nikisomea mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE). Hali ya hewa ya jiji la Tanga haikunipenda, hivyo nikawa naumwa mara kwa mara. Lakini pia sikupenda kusoma HGE, nilitaka kusoma Hisabati badala ya Historia. Wakati wa likizo ya mwezi Disemba mwaka 1996, nilitoka Tanga nikaenda Dar es Salaam, Wizara ya Elimu kuomba uhamisho kwenda shule yenye Somo la Hisabati kidato cha Tano na Sita. Nikakataliwa. Lakini nikaambiwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari wakati ule, ndugu Ndeki alisoma pamoja na Samwel Sitta.

Kipindi hicho Mzee Sitta akiwa Mkurugenzi wa Investments Promotion Centre (IPC) mara kabla haijabadilishwa jina kuwa Tanzania Investments Centre (TIC) mara baada ya kuwa mbunge wa Urambo kwa miaka 20 (1975 - 1995). Nikaenda Ofisi za IPC, zilizokuwa mahala ambapo leo ni Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe. Nilipofika Katibu Muhtasi wake akaniuliza kama nina miadi na bosi wake, nikasema hapana. Akaniambia hawezi kukuona. Nikasisitiza sana na kumlilia dada yule aniruhusu hata kwa akika chache tu. Akaniruhusu.

Nilipofika Mzee Sitta aliniuliza shida zangu kwa heshima kubwa. Nikamwambia kwamba ninataka kuhama shule. Akaniomba matokeo yangu ya Kidato cha Nne, nikampa maana nilikuwa natembea nayo. Alipoyasoma akaniambia, "wewe hupaswi kuhangaika kutafuta shule maana kwa matokeo yako unaweza kusoma shule yeyote nchini ya chaguo lako". Akainua simu akampigia ndugu Ndeki kumuomba anihamishe.

Kisha akaniandikia kikaratasi niende Wizarani muda ule ule. Nilipofika Wizarani nikapewa uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mazengo. Nilipotoka nje ya Wizara nikakutana na kijana mwengine, Godfrey Hiluka, anaomba uhamisho, yeye anatoka Mazengo anataka kwenda Tosamaganga Iringa. Akaniambia, achana na Mazengo hakuna Mwalimu wa Uchumi na hali ya vyoo ni mbaya sana.

Nikarudi kwa Mkurugenzi. Mtumishi aliyenijazia fomu za Uhamisho (Mzee wa Makamo) aliponiona narudi na kumwambia sitaki kwenda Mazengo, akachukua fomu zangu za uhamisho na akachukua 'kifuta - wino' (whiteout) akafuta Mazengo na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira "nyie watoto wa wakubwa bwana!"Sikujali nikaenda zangu Tosamaganga kusoma Uchumi, Jiografia na Hisabati (EGM).

Samwel John Sitta akaendelea kufuatilia maendeleo yangu shuleni, mpaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Taasisi ya InWent nchini Ujerumani. Nilipotoka Ujerumani kusoma masomo ya Juu ya Biashara ya Kimataifa mwaka 2004 nilipaswa niwe na mradi wa kitaaluma. Nikachagua kuunganisha makampuni ya Kijerumani na makampuni ya Tanzania kwa kuandika mradi wa kuchukua wafanyabishiara 20 kutoka Tanzania na kuwaunganisha na wengine 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya.

Ilibidi kupata Taasisi ya Tanzania kwa ajili mradi huo na Mzee Sitta akawa mstari mbele kuhakikisha Mradi unafanikiwa na tukautekeleza kwa umakini kwa msaada wa afisa wa TIC aitwaye Phina Lyimo. Mafungamano yetu hayakuishia hapo, mwaka mmoja baadaye tukakutana na Mzee Sitta Bungeni, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki na mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ulezi wake kwangu ukaendelea mpaka mauti yalipomkuta leo mapema asubuhi. Taifa limepoteza Kiongozi mzalendo, lakini mimi nimepoteza pia 'babu Mlezi'.

Samwel John Sitta alikuwa Mwanamageuzi (Reformer), na kupitia uanamageuzi wake alifanya mabadiliko makubwa sana katika uendeshaji wa shughuli za Bunge akiwa Spika wa Bunge kwa miaka mitano. Sisi tuliohudumu kwenye Bunge la tisa chini yake, tukimwita Spika wa Viwango na Kasi, tuliona wenyewe juhudi zake za kuliweka Bunge katika nafasi yake ya Kikatiba.

Licha ya kuhakikisha kuwa maslahi ya Wabunge yanakuwa yanayolingana na hadhi ya Bunge, alihakikisha pia kuwa Bunge linaisimamia Serikali sawa sawa. Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa na mvutano mkubwa sana kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu Edward Lowasa katika kuleta mabadiliko hayo.

Tulikuwa tunaambiwa kuwa mvutano ule ulitokana na tetesi kwamba Sitta ndiye alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo badala yake. Sio Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha tetesi zile. Sitta ametangulia mbele ya haki, labda Edward Lowasa ataweza kusemea hili siku za usoni.

Samwel Sitta alitumia fursa ya msuguano huo kufanya mabadiliko makubwa ya kanuni za Bunge na kutoa uhuru mpana wa mawazo ndani ya Bunge na kuhakikisha kuwa Taarifa za Kamati za Bunge, hususan Kamati za Usimamizi wa Serikali, zinakuwa zinasomwa na kujadiliwa ndani ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni.

Wakati wa Bunge la 8 chini ya mzee Pius Msekwa, Taarifa za CAG hazikuwahi kusomwa hata mara moja bungeni. Ni kutokana na mabadiliko haya ya kanuni ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC ) ilianzishwa mwezi Machi, mwaka 2008. Nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ile na kuingia kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo kipindi hicho tuliiona kama Kamati ya Wabunge wazee.

Namna nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa POAC nayo ni hadithi nyengine ya namna ya malezi ya kiuongozi yalifanywa na Spika Sitta. Sikuwa nimejaza fomu kuomba hata ujumbe wa Kamati ya POAC. Wakati huo ulikuwa ni wakati wa vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa Madini uliosainiwa na Waziri wa Nishati Hotelini nchini Uingereza kwa siri).

Nilikuwa mjini Bagamoyo kwenye kazi za Kamati ya Bomani (Kamati iliyoundwa na Rais kuchunguza mikataba na sheria za madini) nikiwa na Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige. Spika wa Bunge akanipigia simu, akaniambia "Babu, kesho kuna uchaguzi wa Kamati za Bunge. Nimekuteua Kamati ya POAC ambayo ni Kamati mpya itakayokuwa chini ya Kambi ya Upinzani. Najua hukuomba kuwa mjumbe wa Kamati hii, lakini nahitaji damu changa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge. Naomba unikubalie na kesho uwepo Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi na ugombee. Utashinda maana nimeshafanya kazi yangu".

Sikuwa na namna ya kukataa japo nilitaka sana kuendelea kuwa mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya marehemu Abdallah Kigoda, ama Kamati ya Nishati na Madini chini ya Mzee William Shelukindo. Lakini ombi la Mzee ni amri. Nikawa Mwenyekiti wa POAC na kuwa mmoja wa washauri wakuu wa Spika wa Bunge. Kamati ya PAC ikawa chini ya Mzee John Momose Cheyo na Kamati ya LAAC ikawa chini ya Dkt. Willibrod Peter Slaa. Ilikuwa ni Bunge lenye meno kweli kweli.

Spika Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake ulimpelekea kufanya maamuzi ambayo wakati mwengine yalimweka kwenye matatizo na wananchi. Mfano mzuri ni masuala ya 'Hoja Binafsi ya Buzwagi' na 'Hoja ya Wizi wa Fedha Benki Kuu (EPA)'. Mwanzoni, Spika alikuwa upande wa Wabunge wenye hoja hizo, yaani mimi na Dkt. Wilbroad Slaa kiasi cha kuziboresha hoja zile kwa kalamu yake mwenyewe. Wabunge wa chama chake hawakuwa wanapenda hoja hizi na hivyo Waziri Mkuu Edward Lowasa akamweka kwenye wakati mgumu sana wa kuegemea upande wa Serikali.

Hoja ya dkt Slaa akaitupa kuwa 'Ni makaratasi ya kuokoteza'. Hoja yangu akaiingiza Bungeni na akasimamia kusimamishwa kwangu Bungeni baada ya kuwasilisha hoja hiyo. Wananchi walimkasirikia sana. Siku moja usiku, nikiwa nyumbani kwa ndugu Freeman Mbowe Mikocheni, Spika Sitta akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi wangu wanamtukana kwa ujumbe wa simu (sms), akanitaka niwakataze. Nilimkubalia tu, lakini sikuwa na uwezo huo. Nchi ilikuwa imevimba. Ilikuwa Oktoba 2007. Samwel Sitta alijua namna ya kuisoma nchi, na akamua kuwapa wananchi watakacho, wakati mwengine.

Mwezi Novemba, katika kujibu kiu ya wananchi kuhusu uwajibikaji na kufuta makosa ya Buzwagi na EPA, Spika alisimamia kuundwa kwa Kamati Teule kuchunguza suala la Mkataba wa Richmond. Yaliyofuata yalikuwa historia. Taarifa ya Kamati Teule husika ilipelekea kuanguka kwa Serikali kwa mara ya kwanza katika hsitoria ya Tanzania. Waziri Mkuu Edward Lowasa alilazimika kujiuzulu ndani ya Bunge, Baraza la Mawaziri likavunjika na Serikali mpya kuundwa chini ya Waziri Mkuu mpya, ndugu Mizengo Pinda. Spika Samwel Sitta akawa ni Spika wa pili wa nchi yetu aliyeshuhudia uundwaji wa Serikali mbili ndani ya miaka mitano ya uspika wake.

Mzee Msekwa yeye alikaa kwenye Uspika kwa miaka 13. Miaka 10 na Waziri Mkuu mmoja, ndugu Sumaye. Akianzia Uspika Mwaka 1993. Mwaka mmoja mbele akishuhudia mabadiliko ya Mawaziri Wakuu, kutoka mzee John Malecela kwenda kwa mzee Cleopa Msuya. Baada ya kujiuzulu kwa Lowasa, Samwel Sitta hakurudi nyuma tena. Aliendelea kuwa Spika wa Viwango mpaka alipomaliza muda wake katika Bunge la Tisa.

Sifa nyengine ya Spika Sitta ni Uungwana, alikuwa mwepesi mno wa kuomba msamaha pale alipokosea. Nakumbuka siku moja mwaka 2009 alimfukuza Bungeni Mzee mwenzake John Cheyo kwa makosa ambayo Mzee Cheyo hakufanya. Baadhi yetu tukakasirishwa sana na kitendo kile. Nikaenda kumwona Mzee Sitta ofisini kumwuliza kulikoni amdhalilishe mwenzake namna ile. Akanieleza kuwa hakuwa sawa na atamwomba radhi John Cheyo. Tukiwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge, kwa ajenda zake za kawaida tu, Mzee Sitta akamwomba radhi Mzee Cheyo.

Nikikumbuka kisa hiki hutabasamu, maana Jaji Werema, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alicheka mpaka kuanguka chini. Sababu? Mzee Sitta aliketi kwenye kiti chake, wenyeviti wote wa Kamati tukiwa tumetulia tuanze kikao. Mzee Sitta akasema "John, naomba radhi kwa tukio lililotokea Bungeni wiki iliyopita. Sijui nilikuwa nina nini siku hiyo?, nadhani nilisumbuliwa na watu wanaopitapita jimboni kutaka kunitoa, nisamehe Mzee mwenzangu".

Kicheko ukumbi mzima na mzee John Cheyo akamkubalia radhi yake huku naye akicheka na yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika pamoja Kitabu "Bunge lenye Meno".

Nimwelezeje zaidi Babu? Nimwelezeje zaidi Spika wa Kasi na Viwango Samwel John Sitta? Mwanasiasa Shupavu, Jasiri, Mwenye Ngozi Ngumu, Mbabe, Mnyenyekevu inapobidi na mwenye Uthubutu. Tangulia Babu. Tangulia Mjukuu wa Fundikira. Tangulia Mtemi wa Unyanyembe Samwel John Sitta. Ingawa umeondoka duniani, bado unaishi kupitia kazi zako za Kizalendo kwa Nchi yetu.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Novemba 7, 2016
Dodoma

0 Responses to “BURIANI BABU: NIMJUAVYO SAMWEL JOHN SITTA”

Post a Comment

More to Read